2017-01-06 13:33:00

Papa Francisko: Nguvu na uweza wa Mungu unaitwa huruma!


Yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake mashariki nasi tumekuja na zawadi ili tupate kumwabudu! Ni maneno ya Mamajusi kutoka Mashariki walioongozwa na nyota ili kwenda kumwona na kumsujudia. Mamajusi hawa waliongozwa na nyota iliyowatia shime kuanza safari ili kugundua tukio kubwa lililokuwa limejitokeza katika uso wa dunia. Ni wataalam wa nyota waliokuwa na moyo mpana, kiasi cha kuweza kuona kile ambacho mbingu ilikuwa ikiwaonesha kwani ndani mwao walikuwa wazi na hamu ya kutaka kuona mambo mapya!

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuadhimisha Siku kuu ya Tokeo la Bwana, Ijumaa, tarehe 6 Januari 2017 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Anasema, mwelekeo wa Mamajusi hawa ni kielelezo cha mwamini anayesikia kiu ya kutaka kuonana na Mwenyezi Mungu; mtu mwenye hamu ya kuwa nyumbani kwake, kuwa kwenye makao ya Baba wa milele, yaani mbinguni.

Hii ni sura ya watu wote ambao katika maisha yao hawakuruhusu nyoyo zao “zipigwe ganzi” kwa kutambua kwamba Injili si habari mfu na iliyopitwa na wakati, bali ni sehemu ya maisha ya kila siku, changamoto kwa waamini ni kuhakikisha kwamba wanaondokana na kishawishi cha kubeza maisha, bali kuwa huru dhidi ya manabii wa uwongo wanaotishia maisha ya watu. Hamu ya kutaka kuonana na Mwenyezi Mungu inapyaisha daima matumaini ya Jumuiya inayoamini kwa kuendelea kusali kwa ajili ya ujio wa Kristo Yesu!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwa kusema kwamba, ni matumaini haya yaliyomsukuma daima Mzee Simeoni kwenda kila siku Hekaluni, kwa matumaini ya kukutana na Mkombozi. Ni matumaini kama haya yaliyomsukuma Mwana mpotevu kuondokana na tabia ya kupenda anasa na hatimaye, kuamua kukimbilia na kuambata upendo wa Baba mwenye huruma; sawa na hekima ya Mchungaji mwema anayethubutu kuwaacha kondoo 99 ili kwenda kumtafuta kondoo aliyepotea. Hivi ndivyo alivyofanya Maria Madgalena, alipoamua kwenda kaburini asubuhi na mapema, ili kukutana na Mwalimu wake aliyefufuka kwa wafu!

Hamu ya kukutana na Mwenyezi Mungu inawasaidia waamini kuondokana na mazingira yanayowakatisha tamaa kwamba, hakuna kitu kinachoweza kubadilika! Ni mwelekeo chanya unaowasukuma waamini kujizatiti kikamilifu katika kuambata mabadiliko ambayo kimsingi anayahitaji! Hamu ya kuonana na Mwenyezi ina mizizi yake katika mambo ya kale yanayoendelezwa kwa ajili ya mambo yanayokuja mbeleni!

Mwamini kwa kusukumwa na imani yake anajitaabisha kumtafuta Mwenyezi Mungu hata katika maeneo yaliyofichama katika historia kwani anatambua kutoka moyoni mwake kwamba, huko ndiko anakopatikana Mwenyezi Mungu kama walivyofanya wale Mamajusi kutoka Mashariki. Mwamini anasukumwa kwenda pembezoni mwa jamii, katika maeneo ambayo bado hayajainjilishwa, ili kukutana na Mwenyezi Mungu huko! Anatekeleza yote haya katika moyo wa unyenyekevu pasi na makuu sanjari na kumthamini yule ambaye anatangaziwa Habari Njema ya Wokovu.

Huu ni mwelekeo tofauti kabisa na ule uliooneshwa na Mfalme Herode ambaye hakuguswa hata kidogo na matukio yaliyokuwa yanatendeka kumzunguka. Wakati ambapo Mamajusi walipokuwa safarini, kwa bahati mbaya Yerusalemu ilikuwa “inauchapa usingizi” pamoja na Mfalme Herode aliyekuwa na dhamiri inayoteseka na kuhangaika, kiasi cha kuzama katika hofu na wasi wasi. Akakosa amani mbele upya unaoleta mageuzi ya historia; akajifungia katika ubinafsi, matokeo yake, ufahamu pamoja na mafanikio yake.

Hii ni hofu ya mtu anayekalia utajiri wake kwa kuwa na mawazo finyu kiasi hata cha kushindwa kuona mbali zaidi, hiki ni kishawishi cha kutaka kudhibiti kila kitu! Ni hofu na wasi wasi wa mtu anayetaka kushinda kila jambo kwa gharama yoyote ile; kielelezo cha utamaduni unaowafumbata na kuwaenzi “washindi peke yao” kwa gharama yoyote ile! Woga huu ni wasi wasi wa kile kinachowatafakarisha watu kiasi hata cha kuhatarisha usalama, ukweli wao, jinsi wanavyojihusianisha na malimwengu pamoja na maisha. Herode alikuwa na wasi wasi iliyomtumbukiza katika mauaji ya kinyama.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Mamajusi kutoka Mashariki walifika ili kumwabudu Mfalme pamoja na kumtolea zawadi zao kwani kama Mfalme alikuwa na haki ya kuzaliwa katika Jumba la kifalme, akizungukwa na majeshi pamoja na watumishi wake, alama ya mamlaka, mafanikio na maisha yenye mafanikio. Mfalme anaweza kuheshimiwa, kuogopwa hata kuvikwa “kilemba cha ukoka” lakini si lazima kwamba, anapendwa! Hivi ni vigezo vya kidunia vinavyothaminiwa na wengi yaani: Ibada ya mamlaka, kujisikia na ukuu; mambo ambayo kimsingi yanawaachia watu wengi machungu moyoni pamoja na kuwageuza kuwa ni watumwa!

Baba Mtakatifu anasema, Mamajusi walianza safari ngumu na yenye changamoto nyingi kuanza kumtafuta yeye aliyezaliwa si katika Majumba ya kifalme bali katika mambo msingi yaliyowawezesha kumgundua Mungu anayepaswa kupendwa, jambo linalowezekana katika alama ya uhuru na wala si katika ukatili. Hii ni sura ya Mfalme asiyefahamika lakini anayetegemewa na wengi! Kwani si mfalme anayenyanyasa, anayewageuza watu kuwa watumwa au kuwatupa gerezani.

Huu ni mwaliko wa kuona sura ya Mungu inayowainua wanyonge, inayosamehe na kuponya! Ni changamoto ya kumgundua Mungu aliyezaliwa mahali ambako wengi hawakutarajia, hawakupenda wala kutamani. Hapa waamini wanapaswa kutambua kwamba, kwenye Uso wa Mungu kuna nafasi ya watu waliojeruhiwa, waliochoka, wanaoteseka na kunyanyaswa; watu wanaotelekekwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii! Nguvu na uweza wa Mungu unaitwa Huruma ambayo kwa baadhi ya watu iko mbali sana kama ulivyokuwa mji wa Yerusalemu na Bethlehemu. Ilikuwa ni vigumu kwa Mfalme Herode kumwabudu kwani hakubadili mtazamo wake wala kuacha ibada ya kujiabudu kwa kudhani kwamba, yeye ni mwanzo na mwisho wa yote! Herode alitamani kuabudiwa! Kwa bahati mbaya anasema Baba Mtakatifu Francisko hata Makuhani hawakumwabudu, ingawa walikuwa na ufahamu mpana, walitambua unabii lakini hawakuwa katika mwelekeo wa kutembea na kubadilika.

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha mahubiri yake kwa kusema, Mamajusi walikuwa na hamu ya kuona mambo mapya; walikwisha zoea na kuchoshwa na mambo yaliyofanywa na akina Herode wa nyakati zao. Lakini, mjini Bethlehemu palikuwa ni mahali pa ahadi ya upya na sadaka; huko kulikuwa kuna tukio jipya! Mamajusi waliweza kumwabudu Mtoto Yesu kwa sababu walikuwa na ujasiri wa kusafiri na kumsujudia huyo aliyejifunua katika hali ya umaskini, ambaye hakuwa na ulinzi wala usalama; wakamsujudia Mtoto wa Bethlehemu aliyekuwa hafahamiki na hapo wakagundua utukufu wa Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.