2017-01-05 09:23:00

Ushuhuda wa huduma ya upendo kwa Familia ya Mungu Singida!


Askofu Edward Mapunda wa Jimbo Katoliki Singida, tarehe 6 Januari 2017 kwenye Parokia ya Itigi, Jimbo Katoliki Singida, anatarajiwa kutoa Daraja ya Ushemasi wa mpito kwa Mafrateri wawili wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu. Tukio hili linatanguliwa na Ibada ya kuingizwa rasmi kwenye Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi kwa Frt. Dominic Mavula, tarehe 5 Januari 2017 kwa Ibada inayoongozwa na Mheshimiwa Padre Chesco Peter Msaga, Mkuu wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Kanda ya Tanzania.

Ifuatayo ni historia ya Frater Alessandro Manzi nilizaliwa tarehe 17 Februari 1970 mjini Cesena, Italia. Baada ya masomo na majiundo yangu ya kitaaluma katika fani ya uhandisi wa majengo kati ya mwaka 1989 hadi mwaka 2001 kunako mwaka 2000 wakati wa maadhimisho ya Mwaka wa Jubilei kuu ya Ukristo nilibahatika kutembelea Tanzania ili kushiriki katika utume kwenye Mradi wa Maji unaoendeshwa na Shirika la Wamissionari wa Damu Takatifu ya Yesu nchini Tanzania. Kwa namna ya pekee kabisa, niliguswa na ushuhuda wa maisha, huduma na utume uliokuwa unafanywa na Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu nchini Tanzania.

Kunako mwaka 2003 niliamua kuacha kazi yangu kama mwandisi nchini Italia na kwenda Tanzania kufanya kazi na utume kwa mwamini mlei chini ya uongozi na usimamizi wa viongozi wakuu wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Italia na Tanzania. Nikapangiwa kufanya utume wangu na kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Hospitali ya Mtakatifu Gaspari iliyoko Itigi, Manyoni, Singida. Nikafanikiwa pia kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya cha Chibumagwa, ambacho kutokana na sababu mbali mbali Shirika limelazimika kukifunga kwa sasa.

Nilijifunza lugha ya Kiswahili, mila na tamaduni za Waswahili, ili niweze kuendelea kujitamadunisha. Nikabahatika kukutana na wamissionari kama Padre Dino Gioia aliyenionesha upendo, ukarimu, ari, moyo, sadaka na majitoleo kwa Kristo na Kanisa lake. Hapa pole pole nikaanza kugundua mpango wa Mungu katika maisha yangu, si tena kama Mhandisi, bali kama Mmissionari kwa ajili ya wokovu wa roho za watu! Kuanzia mwaka 2006 hadi mwaka 2009 nilibahatika kuwa ni Mratibu mkuu wa Radio Maria Barani Afrika, utume ambao niliuhitimisha kunako mwaka 2009 ili kuanza masomo na majiundo ya kipadre kama mmissionari wa Shirika la Damu Azizi ya Yesu kwenye nyumba ya Malezi, Miyuji, Jimbo kuu la Dodoma. Nilitoa huduma pia kwa Shirika la Masista wa Ursula wa Moyo Mtakatifu wa Yesu Mteswa, Mkiwa tangu kwa muda wa mwaka mmoja yaani kwa mwaka 2006.

Kunako mwaka 2011 nilianza masomo kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregoriani kilichoko mjini Roma na kuhitimu masomo yangu ya falsafa kunako mwaka 2013. Kunako mwaka 2015 nikapokelewa rasmi kwenye Shirika la Wamissionari wa damu Azizi ya Yesu, Kanda ya Italia na kunako mwaka 2016 nikahitimu masomo yangu kutoka kwenye Chuo Kikuu cha Gregorian kilichoko mjini Roma na kujipatia shahada ya uzamili katika masuala ya Kimissionari. Tarehe 6 Januari 2017 ninajikabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Mtakatifu Gaspar kama Shemasi, ili niweze kuwa ni chombo cha huruma, huduma na upendo wa Kristo unaojionesha kwa namna ya pekee kwa njia ya Damu yake Azizi, iliyomwagika ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Ninapewa Daraja ya Ushemasi nchini Tanzania na wala si Italia nilikozaliwa kwani ni kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto, ukarimu na upendo wa Watanzania nimeonja huruma ya Mungu katika maisha yangu, leo niko hivi nilivyo kwa sababu ya ushuhuda wa kimissionari kwa njia ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Ninawaomba mtusindikize mimi na Frt. Dominic Mavula, ili kweli tuweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa waja wake!

Fra. Alessandro Manzi, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.