2017-01-05 16:40:00

Uingereza jengeni umoja na mshikamano wa kitaifa!


Askofu mkuu Justin Welby, wa Jimbo kuu la Cantebury ambaye pia ni Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani katika ujumbe wake wa Mwaka Mpya wa 2017 anawataka wananchi wa Uingereza katika ujumla wao, kuhakikisha kwamba wanatenda kwa subira na ujasiri mchakato wa kujitoa katika Umoja wa Ulaya, kadiri ya utashi wa wananchi wenyewe kutokana na kura ya maoni. Ni wakati wa kuvuka kinzani na mipasuko ya kijamii, ili kujenga na kuimarisha umoja wa Kitaifa; upatanisho, haki na amani jamii; kwa kufumbata tunu msingi za maisha ya Kikristo zinazojikita kwa namna ya pekee katika mshikamano na ukarimu! Mwaka 2016 wananchi wa Uingereza walipiga kura ya maoni na kuamua kujitoa katika Umoja wa Ulaya, maamuzi ambayo yanaanza kuonesha makali yake katika maisha, kwani kampeni iliyofanywa na wapinzani wa Serikali imeacha mipasuko mikubwa ya kijamii nchini Uingereza!

Sasa ni wakati wa kuzama katika utamaduni na Mapokeo ya Kikristo kwa kujikita katika mchakato wa upatanisho katika ukweli na uwazi! Mchakato wa mageuzi ya maisha ya wananchi wa Uingereza, ufambatwe kwa namna ya pekee na Amri za Mungu na tunu msingi za Kiinjili zinazojikita katika upendo kwa Mungu na jirani; utu na heshima ya binadamu; ustawi na mafao ya wengi. Tunu hizi zikimwilishwa kwa ujasiri, zitawasaidia kwa kiasi kikubwa wananchi wa Uingereza kuvuka mipasuko ya kijamii, kwa kujenga na kudumisha mafungamano na haki jamii, tunu msingi katika kukoleza mchakato wa maendeleo endelevu!

Uingereza haina budi kugundua tena ndani mwake zawadi na chemchemi ya matumaini kwa watu waliokata tamaa kutokana na sababu mbali mbali duniani. Uingereza, iwe ni nchi ya matumaini kwa wale wanaotaka usalama, amani na utulivu na fursa ya maisha bora zaidi. Wakimbizi na wahamiaji ni rasilimali na amana ya maendeleo, ikiwa kama watapewa fursa ya kushirikisha karama na vipaji walivyokirimiwa na Mwenyezi Mungu katika maisha yao. Askofu mkuu Justin Welby anasema, kwa mfano Bwana Sabir Zazai alikuja Uingereza kama mkimbizi kutoka Afghanstan kunako mwaka 1999, leo hii anamiliki na kuendesha Kituo cha kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji. Kuna watu kama Zazai ambao wamekuwa ni baraka, neema na utajiri kwa nchi ya Uingereza.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.