2017-01-04 14:57:00

Siku kuu ya Tokeo la Bwana!


Kanisa linatangaza: “Mataifa yote ya ulimwengu, yatakusujudia Ee Bwana”. Hiki ni kiitikio cha wimbo wa zaburi katika adhimisho la Sherehe ya Epifania, ambapo Kristo Yesu, Mtoto aliyezaliwa anajifunua kwa mataifa yote, anajifunua kwa binadamu wote. Neno “Epifania” ni muunganiko wa maneno mawili ya Kiyunani “epi” na “faino” na kuwa neno moja “epifaino” lenye kumaanisha “kujitokeza” au “kujifunua”. Ni adhimisho la tukio lile ambapo Mtoto aliyezaliwa alifunuliwa kwa mataifa yote. Wafalme watatu ambao kadiri ya mapokeo hujulikana kwa majina ya: Gaspari, Melchiori na Baltazari waliiona nyota upande wa mashariki na kuongozwa na nyota hiyo hadi Bethlehemu ambako walimwona “Mfalme wa Wayahudi aliyezaliwa” na kumwabudu. Mwinjili Mathayo anaongeza katika Injili ya leo kwamba: “Wakaingia nyumbani, wakamwona Mtoto pamoja na Mariamu mamaye, wakaanguka wakamsujudia”.

Safari ya Wafalme wa Mashariki  ilisukumwa na udadisi wao huku wakiongozwa na nyota inawafikisha kwa Mwokozi. Huu ni mwito kwetu kufanya safari ya kiroho kwenda kumtafuta Masiha aliyezaliwa kusudi tumpatie zawadi zetu na tumwabudu. Hamu yao ya kumwona Masiha haikuzuiwa na kikwazo chochote, walisafiri huku wakiulizia kila mahali walipofika hadi walipomfikia huyu aliye Mwanga wa Mataifa. Udumifu na uimara huu hasa katika imani haukuwajia hivi hivi tu bali ni kwa njia ya kujitoa sadaka na kwa njia hiyo tu, kwa utii wao katika kuifuata hiyo nyota ndipo wanafanikiwa kumfikia huyu aliye Mwanga wa Mataifa na wanajawa na furaha iliyo kuu: “Nao walipoiona ile nyota, walifurahi furaha kubwa mno”.

Wakati ujio huu wa Kristo Yesu, Mwanga wa Mataifa ukiwapatia furaha hawa Mamajusi upande mwingine tunapewa habari ya Mfalme Herode anayeweweseka kwa kupokea habari hii: “Basi mfalme Herode aliposikia hayo, alifadhaika, na Yerusalemu pia pamoja naye”. Hii kwao haikuwa habari njema. Yeye pamoja na watu wa nyumba yake na hata maafisa wake walianza kupata mashaka ya kuupoteza ufalme wao. Kristo anapofunuliwa kwao kama Mfalme wa wayahudi utamu wa madaraka yao ya kifalme unaingia shubiri. Hawana muda wa kutafakari maana ya habari hii na umuhimu wake katika jamii ya mwanadamu. Hawatoi nafasi kwa neema ya Mungu kupenya ndani mwao na kuiruhusu Nuru hii inayotuzukia sisi wanadamu ipenyeze miale yake katika jamii ya watu. Badala yake wanaisukumizia mbali na kutafuta mbinu za kuiondosha kabisa machoni mwao. Mfalme Herode anawakilisha jamii ya watu, mabwana na watawala wa jamii yetu ya leo ambao wanaposikia ukweli ukipenyezwa katika kuinusuru jamii na mabalaa yanayotokana na maamuzi yao dhaifu huanza kuingiwa hofu za ndani na kuonyesha kwa nje ukinzani kwa maongozi mbalimbali wanayopatiwa kupitia ufunuo wa kimungu.

Kimsingi hawakumwelewa vyema Mfalme huyu anayezaliwa ni Mfalme wa namna gani. Sababu za ujio wake kwa wale ambao watakubali kuangazwa na nuru yake kwani “wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndiyo wale waliaminilo jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu” (Yoh 1:12). Ufalme wake kama atakavyokuja kujifafanua huko mbele ni Ufalme wa Mungu, ufalme ambao umekuja kuusimika ukweli. Ufalme wake si wa ulimwengu huu: “Ufalme wangu sio wa ulimwengu huu. Kama ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, watumishi wangu wangenipigania ... lakini ufalme wangu siyo wa hapa ... Wewe wasema, kwa kuwa mimi ni mfalme. Mimi nimezaliwa kwa ajili ya haya, na kwa ajili ya haya mimi nalikuja ulimwenguni, ili niishuhudie kweli. Kila aliye wa hiyo kweli hunisikia sauti yangu” (Yoh 18:36 – 37).

Ujio wa Kristo ulimwenguni si kwa ajili ya kutunyanganya na kupindua madaraka na majukumu yetu ya ulimwenguni; si kwa ajili ya kutupora utajiri wetu bali ni kuusimika ukweli katika hayo tunayomiliki na kuyatenda kila siku. Hiyo ndiyo kiu na madhumuni ya Kristo, Neno la Mungu kutwaa mwili wetu wa kibinadamu. Ukweli huo anaokuja kuutawadha ndiyo huo mwanga unaokuja kuwaangazia Mataifa yote; kuwaonesha namna ambavyo Baba alikusudia tangu zamani shughuli zetu na mahusiano yetu ya kijamii yawe. Namna ambavyo tunapaswa kuratibu vema huu ulimwengu tuliokabidhiwa tangu uumbaji, kwani tangu mwanzo Mungu alisema: “zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha” (Mw 1:28).

Hivyo Mfalme Herode hakupaswa kuingiwa na kihoro bali furaha kwani kwa ujio wake Mfalme huyu ukweli unatawala na matokeo yake ni amani, upendo na furaha kwa jamii yote. Mwanadamu pia katika mamlaka zake za kidunia leo hii hapaswi kuingiwa na hofu. Muhimu ni kuukaribisha huu mwanga unaofunuliwa. Hii ni pamoja na kuwa na ujasiri wa kuisikiliza sauti ya Kristo inayotujia kila siku kwa njia ya mafundisho na miongozo ya mamlaka fundishaji ya Kanisa.  Mtakatifu Yohane Paulo wa pili katika Waraka wake wa kitume Centesimus annus anatuambia kwamba: “Kanisa linaheshimu mamlaka huru ya kidemokrasia na wala halina hadhi ya kuonesha upendeleo kwa mamlaka hii au ile au kutoa suluhisho la kimuundo au la kikatiba. Mchango wake kwa hizo mamlaka ni ule wa kutoa mwanga ili kwamba yote yajifunue katika ukamilifu wa fumbo la Neno aliyetwaa mwili” (CA 47).

“Inua macho yako utazame pande zote; wote wanakusanyana wanakujia wewe”. Mwaliko huu unaujia mji wa Yerusalemu na kufanywa kuwa tayari kuwapokea tena watoto wake ambao wanarudi kutoka utumwani; Yerusalemu anaalikwa kumlaki mwana wake ambaye amefanywa tena upya. Mwanaye huyu anamjia tena akiwa amejaa nuru, mwenye furaha na shangwe moyoni mwake. Hawa wanaokuja tunaambiwa ni kutoka pande zote za dunia. Hapa tunaona dokezo la ukombozi wa ubinadamu wote ambao unatimilika kwa ujio wa Kristo, Yeye ambaye anazaliwa na watu toka pande zote wanakusanyika kwenda kumsujudia na kumpelekea zawadi. Sherehe ya leo inathibitisha tukio hilo kwa Wafalme hawa, Mamajusi kutoka mashariki wanakusanyika kwenda kuutazama, kuusujudia na kuutolea zawadi mwanga huu unaoizukia dunia yote.

Yerusalemu hii mpya ni fumbo zima la Kanisa, ni mimi na wewe ambao tunaalikwa leo kupyaisha maisha yetu na kuwafanya wote kuiona nuru ya Kristo inayoangaza ndani ya mioyo yetu. Kristo, Neno la Mungu aliyetwaa mwili wetu wa kibinadamu na kuwa kama sisi anakuwa ni chachu ya muunganiko kwa wanadamu: “wote wanakusanyana”. Uwepo wake unapenyeza upya ambao unawavuta wote katika umoja kama wana wa Mungu; unawavuta wote pamoja kama taifa teule la Mungu linalowakilishwa na mji mtakatifu wa Yerusalemu. Hivyo sherehe hii ya leo inatupatia mualiko wa kuwa ishara ya mtoto huyu aliyezaliwa kwa maisha ya ushuhuda wa kikristo. Wakati wa ufunguzi wa mwaka wa Watawa Papa Francisko aliwaasa watawa na pia anatuasa waamini wote akisema: “Uangavu wa maisha yenu ya ushuhuda utakuwa kama taa iliyowekwa juu ya kiango ili kutoa mwanga na uwezo kwa watu wote wa Mungu ... utoeni ulimwengu kutoka usingizini, uangazeni kwa ushuhuda wenu wa kinabii wenye kukinzana na mwelekeo wa kidunia!”.

“Yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia”. Leo hii mimi na wewe tunazo fursa mbalimbali zinazotuonesha nyota hiyo ya mashariki. Fursa hizo zinatualika kwenda na zawadi zetu kumsujudia Masiha aliyezaliwa kwa ajili ya ukombozi wetu. Nyota hii tunaiona kwanza kabisa kupitia mafunuo ya makuu ya Mungu kupitia Neno lake na Sakramenti zake na zaidi tunazidi kufunuliwa nyota hii kupitia mafundisho mbalimbali ya Kanisa; tunaendelea kuiona nyota hii katika alama za nyakati na mashauri mbalimbali ya kiinjili yote yakituhitaji kuitikia wito huo wa kwenda na zawadi zetu kumsujudia Masiha. Adhimisho la sherehe hii litupatie ujasiri huo wa kuutafuta Mwanga wa Kristo; tubaki imara na wenye kujitoa kikamilifu kuutafuta mwanga na ukweli huo; tuupokee na kuumbatia Mwanga na ukweli huo ili nasi tuwe alama na njia ya kumfikisha Kristo kwa wengine.

Kutoka studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.