2017-01-04 11:40:00

Papa Francisko: Machozi ni mbegu ya matumaini mapya!


Matumaini ya Kikristo ndiyo tema inayofanyiwa kazi na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa katekesi zake kwa wakati hu; ni matumaini yanayofumbatwa wakati mwingine katika kilio na maombolezo kama ilivyokuwa kwa Raheli kwenye Agano la Kale “Bwana asema hivi, sauti imesikiwa Rama, kilio, na maombolezo mengi: Raheli akiwalilia watoto wake. Asikubali kufarijiwa kwa watoto wake kwa kuwa hawako” Lakini, anatulizwa na Bwana akimhakikishia kwamba, kazi yake itapata thawabu na kwamba, liko tumaini kwa siku zake za mwisho, kwani watoto wake watarajea tena!

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake ya kwanza kwa Mwaka 2017 amemzungumzia Raheli anayezungumziwa kwenye Maandiko Matakatifu, kwamba alifariki dunia wakati akiwa anajifungua mtoto wake wa pili. Nabii Yeremia anatumia mfano wa Raheli ili kuwafariji Waisraeli waliokuwa utumwani. Ni kielelezo cha mateso na mahangaiko ya watu, lakini mateso ambayo yanafumbatwa katika faraja ya maisha yasiyotarajiwa. Rama ni mahali ambapo wale waliotekwa na kupelekwa utumwani walikuwa wanakusanyika ili kuomboleza vifo vya watoto wao ambao kamwe hawatarejea tena.

Mateso, uchungu na masikitiko haya yanamfanya Raheli kutotaka kufarijiwa kama ambavyo inatokea kwa wanawake wengine wote. Huu ni uchungu ambao unaweza kulinganishwa na upendo wa dhati; unaofahamika na wanawake wengi. Baba Mtakatifu anasema, hata leo hii kuna wanawake wanaolalama na kuomboleza vifo vya watoto wao ambao kamwe hawatawaona tena maishani. Huu ni mwaliko wa kuguswa na uchungu na mahangaiko ya wengine. Ili kuzungumzia matumaini kwa wale walioguswa na kutikiswa na majonzi haya makubwa, lazima kushiriki mahangaiko yao; ili kukausha machozi kwa wale wanaoteseka, kuna haja ya kuunganika pamoja nao katika kilio. Ni kwa njia hii, watu hawa wanaweza kupata matumaini mapya. Lakini, Mwenyezi Mungu katika huruma na upendo wake anamjibu Raheli kujizuia kulia, maana atampatia thawabu, watoto na hata wao wenyewe watarejea kwao kwani kuna matumaini kwa uzao wake.

Baba Mtakatifu anasema haya ni matumaini ya mama kuwaona tena watoto wake walioko utumwani wakiwa na maisha mapya; Raheli anakuwa ni chombo na shuhuda wa faraja. Waisraeli wataweza kurejea tena kutoka utumwani, wakiwa huru, ili kumwilisha imani na kujenga mahusiano mema na Mwenyezi Mungu. Kwa hakika, machozi ya Raheli yamekuwa ni chemchemi ya matumaini. Hii ni sehemu ya Unabii wa Yeremia ambao Mwinjili Mathayo ameutumia kwa ajili ya kuelezea vifo vya watoto mashuhuda wa Kristo waliouwawa kikatili kwa upanga wa Herode mjini Bethlehemu.

Hii ni sehemu ya Maandiko Matakatifu inayoweka mbele ya waamini adha ya mauaji ya watu wasiokuwa na hatia sanjari na ukatili wa uongozi usioheshimu maisha, kwa kuyafutilia mbali kwa upanga kama “ndoto ya mchana”! Watoto wa Yerusalemu waliuwawa kikatili kwa sababu ya Yesu. Huu haukuwa ni mwisho kwani hata Yesu Kristo, Mwanakondoo wa Mungu kwa wakati wake atayamimina maisha kwa ajili ya wokovu wa wengi. Mwana wa Mungu aliingia na kuzama kabisa katika mateso ya binadamu; akashiriki na kupokea kifo na kwamba, maneno yake ni maneno ya faraja kwani yanabubujika kutoka katika machozi!

Baba Mtakatifu anahitimisha Katekesi yake kwa kukazia kwamba, Kristo Yesu alipokuwa Msalabani, huku akikaribia kuyamimina maisha yake kwa ajili ya wokovu wa wengi, akamzawadia Mama yake, uzao mpya, kwa kumkabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Mtakatifu Yohane na hivyo kumwezesha kuwa ni Mama wa wale wote wanao amini. Kifo kimeshindwa na huo unakuwa ni utimilifu wa unabii uliotolewa na Nabii Yeremia. Machozi ya Bikira Maria kama yale ya Raheli yamekuwa ni chemchemi ya matumaini na maisha mapya!

Baba Mtakatifu amewakumbusha waamini kwamba, tarehe 6 Januari, 2017 Kanisa linaadhimisha Siku kuu ya Tokeo la Bwana. Hii ni Siku ya Utoto Mtakatifu, kwani watoto watapita mitaani kama wale Mamajusi kutoka Mashariki wakitoa baraka na amani ili kuwakumbusha wote kwamba, Kristo Yesu aliyezaliwa mjini Bethlehemu yuko duniani na amejifanya kuwa jirani na wote, ili aweze kuwapatia wokovu; anataka kufanya makazi katika moyo wa kina mwamini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.