2017-01-04 11:58:00

Lindeni na kudumisha maisha, utu na heshima ya wafungwa!


Mara tu baada ya Katekesi yake, Jumatano tarehe 4 Januari 2017 kwenye Ukumbi wa Paulo VI, Baba Mtakatifu Francisko aliyaelekeza mawazo yake nchini Brazil ambako kumekuwepo na machafuko na mauaji ya kutisha kwenye Gereza kuu la Manaus baada ya magenge ya kiuhalifu kupambana vikali, Jumanne tarehe 3 Januari 2017 na hivyo kusababisha zaidi ya watu 56 kuuwawa kinyama, wengi wao wakiwa wamekatwa vichwa na kuchomwa moto! Baba Mtakatifu ametumia nafasi hii kuonesha masikitiko na wasi wasi mkuu kutokana na matukio haya.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kuwaombea wale waliopoteza maisha; waliojeruhiwa vibaya pamoja na familia zao; wafungwa pamoja na wale wote wanaotekeleza dhamana na wajibu wao kwenye gereza hili huko Manaus, Brazil. Baba Mtakatifu anapenda kuchukua nafasi hii kukumbusha tena kwamba, magereza yawe ni mahali pa kuwafunda watu na kuwaingiza tena katika jamii; changamoto ni kuhakikisha kwamba, maisha, utu na heshima ya wafungwa vinalindwa na kudumishwa! Wachunguzi wa mambo wanasema haya ni mauaji ya kinyama zaidi kuwahi kutokea nchini Brazil tangu mwaka 1992.

Baba Mtakatifu Francisko, mwishoni akizungumza na mahujaji kutoka Italia amewatakia amani na usalama kwa Mwaka 2017. Amewapongeza wanachama wa “Chama cha Familia ya Sala na Upendo” kinachoadhimisha kumbu kumbu ya miaka 45 tangu kuanzishwa kwake pamoja na wawakilishi wa Kituo cha Kitume cha Mwenyeheri Vincenzo Romano kinachoadhimisha kumbu kumbu ya miaka 45 tangu kuanzishwa kwake. Amewatakia Wafranciskani walioweka nadhiri za kwanza kukuza na kudumisha moyo wa sala ili kujenga urafiki wa kweli na Kristo Yesu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.