2017-01-03 10:08:00

DRC uchaguzi mkuu unatarajiwa kufanyika mwishoni mwa Mwaka 2017


Baraza la Maaskofu Katoliki DRC limeridhishwa na hatua iliyofikiwa mwishoni mwa Mwaka 2016 kati ya wawakilishi wa Serikali na vyama vya upinzani kwa kutia sahihi kwenye makubaliano kuhusu mchakato wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka 2017. Hii inatokana na ukweli kwamba, muda wa Rais Joseph Kabila kukaa madarakani ulimalizika rasmi tarehe 20 Desemba 2016.  Amekuwemo madarakani kuanzia mwaka 2011 na kwa mujibu wa Katiba, hana tena sifa ya kuwainia Urais kwa awamu ya tatu.

Katika kipindi hiki cha mpito kitakachodumu kwa muda wa miezi kumi na miwili, kutaanzishwa Baraza la Kitaifa litakalosimamiwa na Bwana Etienne Tshisekedi, gwiji la upinzani nchini DRC. Waziri mkuu atachaguliwa pia na Baraza la Kitaifa kutoka katika kambi ya vyama vya upinzani ambayo kwa sasa pia iko chini ya Bwana Tshisekedi.

Wachunguzi wa mambo ya kisiasa wanasema, makubaliano haya ni hatua muhimu sana kwa DRC kuweza kujikwamua kutoka katika machafuko ya kisiasa na kijamii yaliyosababishwa  kwa kiasi kikubwa na ubinafsi pamoja na uchu wa madaraka bila kutoa kipaumbele cha kwanza kwa demokrasia, ustawi na maendeleo ya wengi! Rais Joseph Kabila ataendelea kuwepo madarakani ili kuratibu shughuli zote za kipindi hiki cha mpito na kuhakikisha kwamba, wananchi wa DRC wanapata nafasi ya kupiga kura ili kuwachagua viongozi wanaowataka.

Haya ni mafanikio makubwa yaliyofikiwa chini ya utashi na usimamizi wa Baraza la Maaskofu Katoliki DRC ambalo halikukatishwa tamaa baada ya makubaliano ya kwanza kati ya Serikali na baadhi ya Vyama vya Upinzani kuingia dosari. Tarehe 8 Desemba 2016 likafanikiwa kuwakutanisha viongozi wote wakuu wa Vyama vya Upinzani pamoja na Viongozi wa Serikali iliyoko madarakani ili kuamua hatima na mustakabali wa familia ya Mungu nchini DRC.

Wakati huo huo, Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, inawapongeza wadau mbali mbali waliofanikisha mchakato wa makubaliano haya, ili kuanza mchakato wa kuelekea kwenye uchaguzi mkuu nchini DRC, mwishoni mwa mwaka 2017. Ni matumaini ya Jumuiya ya Mtakatifu Egidio kwamba, Serikali na Vyama vya Upinzani vitaheshimu na kuzingatia mambo msingi yaliyobainishwa kwenye Mkataba wa Amani nchini DRC, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu nchini humo!

Baraza la Maaskofu Katoliki DRC limeonesha ukomavu wa kisiasa kwa kujikita katika majadiliano ya ukweli na uwazi; haki na amani kwa ajili ya ustawi na maendele ya wengi. Wakati wote huu wa majadiliano ya kisiasa, kutokana na utete wake, Baba Mtakatifu Francisko amekuwa akifuatilia hatua kwa hatua pamoja na kuwatia shime kushikakamana kwa ajili ya amani; umoja na mshikamano wa kitaifa, kidemokrasia pamoja na kuguswa na mahangaiko ya wananchi wa DRC.

Jumuiya ya Mtakatifu Egidio inasema itaendelea kutoa mchango wake katika huduma ya afya kwa ajili ya familia ya Mungu nchini DRC, hasa kwa kutoa huduma ya dawa za kurefusha maisha kwa waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi pamoja na kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi, kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, maarufu kama “The Dream”. Amani na utulivu ni nyenzo msingi katika mchakato wa maendeleo endelevu nchini DRC.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.