2017-01-02 14:09:00

Siku ya Kuombea Amani Brazili 2017: Amani na Matumaini!


Maadhimisho ya Siku ya 50 ya kuombea amani kwa Mwaka 2017 yanaongozwa na kauli mbiu “Kutotumia nguvu: mtindo wa siasa ya amani”. Baba Mtakatifu Francisko anaelezea kuhusu vita, kinzani na mipasuko ya kijamii duniani inavyoendelea kusababisha majanga makubwa kwa watu na mali zao. Anakazia umuhimu wa kutangaza na kushuhudia amani kama kiini cha Habari Njema ya Wokovu. Anawataka waamini kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa amani duniani.

Kwa upande wake, Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil linaialika familia ya Mungu nchini humo kwa kusema” .. hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu.” Kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Kuombea Amani Duniani ambayo huadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe Mosi, Januari. Huu ni ujumbe unaojikita katika amani na matumaini kwa kutambua kwamba, amani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na ni tunda la haki, upendo na huruma.

Huu ni msingi  wa maisha dumifu na endelevu ya kijami. Maaskofu wanasema, matumaini yanayofumbatwa katika imani yanashuhudiwa kwa njia ya mchakato wa ujenzi wa maisha na ulimwengu mpya unaosimikwa katika amani ya kweli na dumifu. Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil linawakumbusha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kwamba, nchi yao inajipambanua kwa kuwa ni watu wachapakazi, wakweli na waaminifu; wanaojenga na kudumisha udugu na mshikamano; watu wenye kiu ya amani na matumaini.

Maaskofu wanasikitika kusema kwamba, katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwepo na ukosefu wa haki hali ambayo imeitumbukiza nchi ya Brazil katika kashfa kubwa, kielelezo cha kumong’onyoka kwa tunu msingi za kimaadili na utu wema. Rushwa na ufisadi wa mali ya umma ni mambo ambayo yameleta athari kubwa katika maisha ya wananchi wengi wa Brazil, changamoto ni kuendelea kusimama kidete kupambana kufa na kupona na saratani ya rushwa kwa kuzingatia utawala wa sheria na demokrasia ya kweli!

Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil linawakumbusha wanasiasa na wapambe wao kwamba, siasa ni huduma kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na kamwe si kichaka cha watu wachache kujitafuta wenyewe na masilahi yao binafsi. Mwelekeo kama huu ndio unaoendelea kusababisha ukosefu wa haki jamii, changamoto ni kupyaisha mtindo wa kufanya siasa, ili kweli wanasiasa waweze kuaminiwa tena, katika mchakato wa ujenzi wa jamii inayosimikwa katika haki, udugu na mshikamano, kwa kuzingatia utawala wa sheria, demokrasia na mahusiano mema kati ya viongozi wa umma ili kuimarisha mafungamano ya kijami.

Serikali ina wajibu wa kuhakikisha kwamba, wananchi wake wanaongozwa na Katiba ya Nchi ambayo kimsingi ni ”Sheria Mama”. Wananchi wengi wa Brazil kwa sasa wanaogelea katika hali ngumu ya uchumi na maisha, kumbe, kuna haja ya kuibua mbinu mkakati wa kulikwamua taifa kutoka katika athari za myumbo wa uchumi kitaifa; kwa kuzingatia haki msingi za binadamu pamoja na kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kuna haja ya kusimama kidete ili kujenga na kudumisha jamii inayojikita katika haki, amani na umoja wa kitaifa kwa kukataa kishawishi cha kutumia nguvu, ili kukuza na kuimarisha utamaduni wa majadiliano. Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil linawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujikita katika tunu msingi za Kiinjili, demokrasia kadiri ya Katiba ya nchi ili kweli kila mwananchi aweze kuwa ni chombo na shuhuda wa Injili ya amani duniani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.