2017-01-01 14:15:00

Wamepigwa na butwaa!


Duniani kuna mambo!“Boxing day” ni siku zinapofunguliwa zawadi za Noeli. Siku hiyo watu wanapaparika kufungua zawadi ili kupigwa sapraizi wanapoona aina ya zawadi wanazofungua. Mtu unapata sapraisi unapokiona kitu au zawadi usiyotegemea. Leo tutawakuta watu kadhaa waliopigwa butwaa na kuishangaa zawadi wasiyoitegemea kuipata katika maisha yao. Kwa mfano wachungaji waliwekewa zawadi kizizini tena sehemu wanayolishia ng’ombe chakula:“Walikuwako wachungaji wakikaa makondeni na kulinda kundi lao kwa zamu usiku. Malaika wa Bwana akawatokea ghafula,akawaambia, Msiogope; kwa kuwa mimi ninawaletea habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote; Na hii ndiyo ishara kwenu; mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelala katika hori ya kulia ng'ombe.”

Malaika walipoondoka tu wale wachungaji wakahojiana wao kwa wao kabla ya kutoa uamuzi wa kwenda kuiona hiyo "sapraisi". Kwa kweli walichosikia kilikuwa ni sapraisi kwao kwa vile hawakutegemea kabisa kuwa siku moja watakuja kutokewa na malaika wa Bwana na kuambiwa maneno mazuri kama yale. Kwa sababu wao walisadikishwa na watu wote kuwa ni wadhambi na wameshalaaniwa na Mungu. Hivi wanajihoji kama kweli Mungu anawatakia mema. Huu ndiyo uzuri na sapraisi ya Noeli, yaani kujihoji kama ni kweli au sivyo kuwa Mungu anaweza kuzaliwa kwa ajili yetu binadamu.

Baada ya kujihoji kwa pamoja wanatoa uamuzi: “Twendeni Bethlehemu tukashuhudie kwa macho yetu tuliyoambiwa na Bwana.” Nasi tunaalikwa kufuatana na wachungaji kwenda kuhakikisha juu ya Mungu huyo anayeweza kutujaza furaha ya Neno la Injili. Twende tukamwone Mwana huyu aliyeviringishwa vitambaa na kulazwa pangoni. Kisha tuendelee tena na safari hadi tufike pale alipoviringishwa tena aina hiyohiyo ya vitambaa yaani sanda na kulazwa kwenye pango lililokutwa wazi asubuhi ya Pasaka.

Kisha wchungaji wakaondoka: “Wakaenda kwa haraka wakamkuta Mariamu na Yusufu, na yule mtoto mchanga amelala horini.” Hali ya kuondoka kwa haraka tunaikuta pia kwa Mama Bikira Maria alipoenda kumtembelea Elizabeti. Kadhalika Zakayo Mtoza ushuru baada ya kuambiwa na Yesu, shuka upesi toka mtini, naye akashuka haraka mi kwenda nyumbani. Kwa hiyo anayetambua kuwa Mungu ni upendo na anataka kuingia katika maisha yake anampokea kwa furaha na kwa haraka.

Malaika aliwaambia wachungaji kwamba, “mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelala katika hori ya kulia ng'ombe.” Kumbe wanapofika hapo wanamkuta Yusufu, mtu ambaye hawakuambiwa kabisa na malaika. Yusufu anaonekana amepigwa butwaa, amebaki anashangaa kwani naye amepata sapraisi badala ya kumwona Mungu yule aliyetangazwa na kutabiliwa na wakuu wa ulimwengu, kumbe anamwona mtoto mchanga tena wa kawaida kabisa. Kadhalika Maria mama ya mtoto, naye anashangaa tu haelewi kinachoendelea. Hii ni sapraisi ya mwaka. Kumbe Neno la Mungu ni kitu kinachotakiwa kukishangaa, kukitafakari kwani huyu anayeonekana kuwa ni mchanga ndiye upendo usio na mipaka. Yesu ni mmoja wetu hivi hana sababu ya kuwa na alama ya pekee. Kama Mungu amejifanya mtu hapo kweli anatupenda. Kuzaliwa kwake ni tangazo la upendo linalotutuliza sisi sote.

Wachungaji walipofika, nao wakabaki tu kushangaa na kutafakari sapraisi wanayoiona. Kumshangaa maana yake kumtafakari huyu Mwana yaani kufaidi kuuona uso wa Mungu. Nasi tunaalikwa, kutafakari, kufurahia na kufaidi sura ya Mungu, inayotuambia kwamba kumbuka kwamba “Mimi ninakupenda.” Nasi tukishajisikia tunapendwa basi tusikilize Neno lake.

Kisha tunaambiwa kuwa: “Wote waliowasikia wachungaji walishangazwa na kile walichokuwa wanakisema.” Hivi wote walishangazwa na ujumbe huu mpya unaomhusu Mungu. Hivi wachungaji, Maria, Yusufu na wote walianza kutambua sapraisi ya Mungu, na utume wa huyu Mwana. Wazazi hawa wanashangaa kile atakachosema Simoni, “mwanga wa kuwaangaza mataifa.” Kama inavyosemwa: “Wazazi wake wakashangaa yaliyokuwa yanasemwa juu ya mtoto.” Walishangaa pia pale Yesu alipobaki hekaluni alipokuwa na miaka kumi na mbili, yasemwa kuwa wazazi wake walishangaa na hawakuelewa maneno yake. Maana yake, Maria na Yusufu walikuwa daima tayari wanapokea neno la Mungu lakini walielewa polepole.

Kwa hiyo, kama sisi hatushangazwi na noeli hii, yaonekana hatujatambua bado upendo huu mkuu wa Mungu na kuupokea mioyoni mwetu, hapo yaonekana hatujamtambua Mungu huyu anayeshangaza na kutushangaza sote. Mtoto huyu anatuonesha picha ya Mungu anayetupenda na kutupenda. Maria aliyaweka maneno haya yote na kuyatafakari moyoni mwake. Hii ndiyo picha ya Maria, msichana wa umri mdogo tu, anayekusanya kila alama na kuweka pamoja alama hizi zote na vituko vyote vinavyoonesha mipango ya Mungu kwa mtoto wake.

Wachungaji walirudi, wakimtukuza Mungu kutokana na yale waliyoyasikia. Walirudi baada ya kupata habari zote za Mungu. Kumbe, kama Malaika waliorudi mbinguni wakimtukuza na kumwimbia Mungu utukufu, hapa duniani unawakuta wachungaji, watu wasio na thamani, ndiyo wanaoungana na malaika kumtukuza na kumwimbia Mungu utukufu. Hii ni "sapraisi" "mshtuko" mwiingine tena kuona kwamba hapa duniani wako watu wanaoimba wimbo mmoja na Malaika wa mbinguni wa kumtukuza Mungu: “Mtakatifu, mtakatifu, mtakatifu.”

Fasuli ya Injili inahitimisha juu ya kutahiliwa huyu mwana na kupewa jina la Yesu. Hilo ni jina lililoelekezwa na malaika, mwana lipokuwa bado tumboni mwa mama. Hali ya kupewa jina inatukumbusha suala la upendo, kwamba baada ya kupata sapraisi, unataka kujua kitu kilichokushangaza kinaitwaje. Kadhalika katika mazungumzo ya watu wawili, ni baada ya kuzoeana unakumbukwa kuuliza jina ili kuweza kujuana zaidi. Kwa hiyo, hapa tunadokezewa jina la mtu anayetupenda kuonesha hadhi yake. Katika agano la kale Mungu hakuweza kujulikana jina lake, lakini katika Agano jipya anaitwa jina Yesu, yaani mkombozi. Ni mkombozi mwenye upendo. Katika injili ya Luka jina la Yesu linatajwa karibu mara 566 tena linatamkwa na watu wa mwisho, wakosefu, wagonjwa, walio na pepo, vipofu, majizi wa msalabani, wakoma.nk.

Ndugu zangu, tunaalikwa kumpenda yule aliye na jina lenye hadhi ya kukomboa na mwenye hadhi ya kupenda hasa. Tujifunze kulipenda jina hili. Ee Yesu wewe ndiye yule anayeokoa, ninakupa maisha yangu. Tuwe waaminifu kwa pendekezo hili la upendo la Yesu kwetu.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.