2017-01-01 15:00:00

Tuheshimu viumbe na kuvitunza ni chapa ya muhuri wa uzuri na upendo wa Mungu


Kuheshimu Viumbe , na kuvitunza, ni kwa sababu kila kitu kilichoumbwa na Mungu ni chema na ni chapa ya  muhuri wa uzuri na upendo wake. Hayo ni maelezo ya ujumbe wa Baraza la maaskofu wa Congo Brazaville katika ujumbe kwa watu, wakati wa sikukuu ya kuzaliwa kwa Bwana. Ujumbe huo uliandikwa na Maaskofu wa Congo Brazaville  na kutiwa sahini  na Askofu Miguel Angel Olaverri wa Jimbo Katoliki Ponte – Noire mwakilishi wa Baraza la Maaskofu katika utume wa jamii na maendeleo, “ tutunze mazingira nyumba ya wote kwani Mungu alituzawadia nchi yenye utajiri wa ardhi yenye rotuba na mali ya asili kama misitu , mito, maji na bahari, vyote hivyo  ni upendo wa hajabu wa Mungu baba”.

Hata hivyo Askofu Miguel anatoa onyo juu utumiaji hovyo na  uharibifu wa mazingira na hasa ukataji  na uchomaji hovyo  wa mazingira na matokeo yake ni kusababisha jangwa ,halikadhalika siyo hiyo tu bali hata uchavuzi wa mazingira ambayo uleta  hathari za afya ya jamii.Hivyo maaskofu wanaonesha  athari gani za ukosefu wa kutunza mazingira ambapo usababisha uchafu na kuleta magonjwa kama vile Malaria, homa ya matumbo magonjwa ambayo husababisha kifo. Wakigusia juu ya Waraka wa Kitume "Sifa iwe kwako juu ya utunzaji wa mazingira"(Laudato si) wa Baba Mtakatifu Francisko na nyaraka nyingine zilizowahi kutolewa, (“Caritas in veritate”) ya Papa  Benedikto XVI, na na ( “Centesimus Annus”) ya Yohane Paulo II, Askofu Olaverri , anawataka waaamni kuwa na wongofu wa kweli  dhidi ya mazingira ambayo yanahitaji kuyaheshimu na pia kuelimishwa juu yake.

Ujumbe huo  ni wito pia  kwa Serikali kuchukua  hatua za ukusanyaji wa taka na kuwajibika katika kuelimisha watu watambue namna ya kutunza na kuheshimu mazingira. Halikadhalika msisitizo hasa wa Maaskofu ni ule wa kuelimisha jamii na shule  kwa kutumia mitandao ya kijamii , ili kundeleza jamii  katika kuwajibika. Na mwishoni, Maaskofu wa Congo Brazaville wanatilia  mkazo juu ya umuhimu wa maisha ya binadamu, utu wake ambao wanasema ni mtakatifu na hakuna yoyote aliye na haki ya kuugusa kwa sababu ni zawadi kutoka kwa Mungu , aidha suala la amani , ukweli na heshima katika mazingingira na kwa jirani ni muhimu sana!

 Sr Angela Rwezaula.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.