2017-01-01 11:49:00

Bikira Maria: aliyahifadhi, akayatafakari na kuyamwilisha!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, tarehe Mosi, Januari 2017 amewakumbusha waamini na mahujaji waliofurika kwa wingi kutoka pande mbali mbali za dunia kwamba, hivi karibuni, Kanisa limeadhimisha Siku kuu ya kuzaliwa kwa Mwana wa Mungu huko mjini Bethlehemu. Tarehe Mosi, Januari, Kanisa linaadhimisha Siku kuu ya Bikira Maria Mama wa Mungu, ambaye anajihusisha kwa namna ya pekee na utume wake hapa duniani. Bikira Maria kwa kutambua utume huu, alijiweka wazi na kushiriki kikamilifu katika matukio mbali mbali yaliyojitokeza katika maisha ya Yesu Kristo.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Bikira Maria akabahatika kuyahifadhi, kuyatafakari na kuyamwilisha katika uhalisia wa maisha yake. Ni Mama aliyekubali kushiriki katika Mpango wa Ukombozi wa Mungu kwa kuwatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao, akawaangusha wakuu kutoka katika viti vyao vya enzi; na kuwakweza wanyonge na kuwashibisha mema wenye njaa na wenye mali amewaondoa mikono mitupu! Katika hali ya ukimya na umakini mkubwa, anatafakari kile ambacho Mwenyezi Mungu anamtaka katika maisha yake ya kila siku!

Mwenyezi Mungu alipenda kujifunua kati ya maskini na wanyenyekevu wanaodhihirishwa kwa uwepo wa wachungaji waliokuwa kondeni wakichunga mifugo yao. Mwinjili Luka, yuko makini sana kwa matumizi ya maneno anapolielezea tukio hili. Wachungaji wakaenda kwa haraka wakamkuta Mariam na Yusufu pamoja na yule Mtoto Mchanga! Walipomwona wakasimulia habari waliyoambiwa na Malaika juu ya Mtoto huyu. Wachungaji wakarudi, huku wakimtukuza na kumsifu Mungu. Bikira Maria akayaweka yote haya kwenye sakafu ya moyo wake. Hii ikawa ni chemchemi ya wokovu na Bikira Maria akawa tayari kutekeleza mpango wa Mungu katika maisha yake.

Baba Mtakatifu anasema, Bikira Maria akawa ni Mama wa Mungu na hivyo kushiriki kikamilifu katika Mpango wa Ukombozi utakaotekelezwa na Mwanaye Mpendwa na kwa njia yake Mtumishi wa Bwana, Mwenyezi Mungu anaweza kutenda matendo makuu ya huruma ya Mungu. Kutokana na Ukuu wa Bikira Maria, Baba Mtakatifu ametumia nafasi hii kumshukuru Bikira Maria Mama wa Yesu ambaye kwa njia ya unyenyekevu wake, Mwenyezi Mungu akaweza kumwangalia; kwa imani akalipokea Neno lake na kwa ujasiri mkubwa akakubali kuwa ni Mama wa Mungu, kiasi cha kujisahau mwenyewe na kuambata Upendo Mtakatifu uliojikita katika maisha na kuwa ni matumaini yake. Anamshukuru na kumwomba Bikira Maria ili aweze kuwaombea watoto wake wanaosafiri katika nyakati na awasaidie kutembea katika njia ya amani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.