2016-12-31 12:37:00

Kipindi cha Noeli: Muda wa furaha, machungu na matumaini!


Askofu Juan Jose Aguirre wa Jimbo Katoliki la Bangassou, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati anasema, maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli na Mwaka Mpya 2017 yanabeba ndani mwake furaha, machungu na matumaini ya familia ya Mungu. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, hata katika maadhimisho ya Siku kuu hizi kuu, bado kuna watu wanaoendelea kufa maji kwenye Bahari ya Mediterrania na utupu kwenye Jangwa la Sahara.

Bahari imegeuka kuwa ni kaburi lisilo na alama kwa wahamiaji na wakimbizi zaidi ya 5,000 kupoteza maisha yao wakiwa njiani kutafuta hifadhi na usalama wa maisha huko Ughaibuni! Bado kuna watu wanaendelea kuteseka kutokana na vita na mashambulizi ya kigaidi huko Lebanon na Siria. Wafanyakazi wa Chama cha Msalaba Mweupe wanaendelea kufanya kazi usiku na mchana kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu huko Siria. Watoto hawana tena matumaini ya kwenda shule kwani shule nyingi zimebomolewa kutokana na vita!

Askofu Aguirre anaendelea kuorodhesha litania ya matatizo kwa kusema kwamba, Kaskazini mwa Nigeria, bado Kikundi cha Kigaidi cha Boko Haram kinaendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao! Kuna baa la njaa na utapiamlo wa kutisha kwa watoto wadogo. Hapa kinachonekana ni uchu wa mali na madaraka kwa gharama ya maisha ya watu wasiokuwa na hatia. Hata Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati mambo si shwari sana kwani watu bado wana wasi wasi ya machafuko na kinzani za kijamii.

Licha ya matatizo na changamoto zote hizi, bado Kipindi cha Noeli kinaashilia furaha na matumaini ya kupatikana kwa amani ya kudumu huko Amerika ya Kusini kwa nchi kama PerĂ¹, Colombia na Equador! Kipindi cha Noeli, iwe ni fursa pia ya kusimama kidete kulinda, kudumisha na kutunza mazingira nyumba ya wote kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko. Kipindi cha Noeli, iwe ni fursa ya kujenga na kudumisha upendo, mshikamano, haki, amani na maridhiano, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.