2016-12-30 11:29:00

Siku kuu ya Bikira Maria Mama wa Mungu


Leo tunaadhimisha Sherehe ya Bikira Maria, Mama wa Mungu ”Theotokos” Pamoja na adhimisho hilo na sababu siku hii kuwa ni mwanzoni mwa mwaka mpya, sherehe hii huambatanishwa na siku ya mwaka mpya na hapo hapo Kanisa limejitengea siku hiyo kwa ajili ya kuomba amani ulimwenguni kote.

Antifona ya wimbo wa mwanzo inatuelezea sababu za Bikira Maria kupewa cheo hicho cha kuwa Mama wa Mungu: “Salamu, Mama mtakatifu wa Mungu, uliyemzaa Mfalme mwenye kutawala mbingu na dunia daima na milele”. Ni Mama wa Mungu kwa sababu ya utii wake katika mpango wa Mungu ameuzalia ulimwengu Mkombozi, Yesu Kristo ndugu yetu ambaye ni Mungu kweli na mtu kweli. Umungu na ubinanamu vinaungana katika fumbo la ajabu ndani ya nafsi ya Kristo na hivyo Mtaguso wa Efeso ulimtaja Maria kama Mama wa Mungu (Theotokos) kwa vile huyo ambaye ni uzao wa tumbo lake ni mtu kamili na pia ni Mungu kamili, namna ambazo haziwezi kutenganishwa bila kuathiri ukweli juu ya Kristo, Mwana wa Mungu ambaye hivi karibuni tumesherehekea kuzaliwa kwake.

Katika historia ya Kanisa fumbo hili la umama wa Bikira Maria limekumbana na ukinzani mkubwa, mfano tukirejea mtifuano wa mafundisho ya Kasisi Nestori katika karne ya 5, ambao umepelekea pia kuupokea ukweli juu ya Kristo kama Mungu kweli na mtu kweli kuingiwa na mushkeri kidogo. Yatokanayo na mitafaruku hiyo na mafundisho msingi yaliyothibitisha umama wa Bikira Maria tuwaachie Wana taaliMungu na pia kama yalivyoelezwa kwa muhtasari hapo juu.

Kwetu sisi inatosha kuyatafakari maneno ya Biblia hasa somo la pili la Sherehe hii ambalo linaonesha muunganiko huo wa kimama wa Bikira Maria kwa Kristo: “ulipotimia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke”. Kristo hazaliwi kama kiumbe cha miujiza bali anazaliwa na Mama kama binadamu wote na ujio wake katika jamii ya wanadamu ni kwa njia ya kawaida kabisa, yaani kwa kuzaliwa. Lakini sehemu hiyo ya Neno la Mungu linamtaja huyu anayezaliwa kama Mwana wa Mungu anayetumwa wakati ulipotimia kwa ajili ya kuwa komboa wanadamu walikuwa chini ya sheria. Hivyo tunauona muunganiko huo kwa urahisi kwamba anayezaliwa ni Mwana wa Mungu hivyo ni Mungu ambaye anazaliwa kama mwanadamu.

Kama ilivyoelezewa hapo juu linabaki kuwa ni fumbo na ni imani tu itakayotufikisha katika uelewa makini. Hapa ni vema kuungana na moja ya Manguli wa taalimungu Kasisi Malema Mwanampepo katika moja ya tungo zake akisema: “Pendo lako Bwana Yesu ni hazina ya wema wote, washuka kutoka juu waninjia hapa duniani, imani tu, imani tu, imani tu yaelewa!” Hii ndiyo njia sahihi ya kutufikisha katika kulielewa na kulikumbatia fumbo hili kikamilifu. Hii ni kwa sababu elimu hii kubwa ya kimungu ya namna muunganiko huu ulivyofanyika inaupita uwezo wetu wa kibinadamu wa kuelewa.

Sehemu hiyo ya Maandiko Matakatifu inazidi kumwelezea Kristo katika ubinadamu wake ili kuuthibitisha umama wa Bikira Maria. “amezaliwa chini ya sheria, kusudi awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupokee hali ya kuwa wana”.  Kuzaliwa huku chini ya sheria kunamaanisha kwamba alizaliwa chini ya jamii ya wanadamu na kufuata sheria na taratibu zote lakini si kama mtumwa wa sheria hizo bali kama mwana huru.

Uhuru huo ndiyo unamkomboa mwanadamu na kuzikumbatia sheria na taratibu zote kama nyenzo ya kumkamilisha katika kuitwa mwana mrithi wa Mungu. Kristo alizifuata sheria zote za Musa mfano kutahiriwa baada ya siku nane kama inavyoelezewa na Injili ya sherehe ya leo, kabla ya mateso na kifo chake aliadhimisha Pasaka ya Kiyahudi pamoja na mitume wake, yaani kwa ufupi kila hatua ya maisha yake ilitii sheria na taratibu za jamii yake ya Kiyahudi ambamo humo alizaliwa.

Utii wake mkamilifu kwa Mungu Baba yake kama Mwana wa Mungu aliyezaliwa na mwanamke kulimfanya kutimiza kikamilifu yote yaliyotakiwa na sheria. Mwana wa Mungu anaichukua nafasi yetu kama mwanadamu ili kutuonesha utii mkamilifu kwa Mungu kwa niaba yetu. Kuzaliwa kwake chini ya sheria pia kulimaanisha kwamba, alionja laana ya wale ambao wameshindwa kuitii sheria. Pamoja na kwamba, Yesu alitimiza matakwa yote ya sheria lakini bado hakuepushwa na kuionja hali ya mwanadamu mdhambi aliyekuwa chini ya sheria au mwanadamu ambaye alijifanya kuwa mtumwa wa sheria. Aliandamwa na vishawishi, mateso, upweke na kilele cha yote ni kuonekana kama aliyelaaniwa na Mungu kwa kifo cha msalabani. Maelezo haya yote ambayo yanauthibitisha ukweli juu ya ubinadamu wa Kristo ambao unaunganishwa kwa namna ya ajabu na umungu wake yanampambanua Mama yake Bikira Maria kama Mama wa Mungu.

Sherehe hii ya leo inaunganika vema na ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko anaotupatia katika siku ya 50 ya kuombea amani duniani unaobeba kichwa cha habari “Mazungumzo bila mapigano: mbinu ya kisiasa kwa ajili ya amani” ujumbe ambao unawaalika wanadamu wote kuitafakari hadhi ya ubinadamu wetu inayoangamizwa kila kukichwa katika maeneo yenye vita. Baba Mtakatifu amewakumbusha Mabwana vita na wengineo wanaohusika na machafuko kuepuka njia hizo za machafuko na kugeukika katika mbinu hii ya mazungumzano, mbinu ambayo itauhifadhi ubinadamu unaodhalilishwa na kungamizwa na matukio ya kivita.

Katika vita kinachoangamizwa ni ubinadamu na pengine tunaweza kudanganywa na ubabe au manufaa ya kisiasa tuyapatayo bila kukimbilia katika kuutunza na kuuthamini utu wa mtu. Matokeo yake ni kuzidisha chuki na mpasuko kati ya wanadamu. Utii wa Mama yetu Bikira Maria umeuwezesha ubinadamu wetu kuivaa tena hadhi yake ya asili, utii wake Mama huyu Mtakatifu wa Mungu unamuunganisha Mungu na mwanadamu. Na hivyo anaendelea kusisitiza Baba Mtakatifu kwamba hamu yetu ya kutafuta amani haitokani na machafuko bali ndani kabisa katika nafsi zetu kwani “kwa Mkristo mazunguzano ya bila mapigani si tu mbinu ya kitabia bali ni namna ya ndani ya utu wake, muelekeo wa yule ambaye anaamini kabisa katika upendo na uwezo wa Mungu kiasi ambacho kamwe haogopi kupambana na uovu kwa kutumia silaha za upendo na ukweli tu”.

Hivyo ni vema kuizingatia hadhi hii ya kuwa wana wa Mungu ambayo inavikwa kwa wanadamu wote. Baba Mtakatifu anamtaja Mtakatifu Mama Theresa wa Calcutta kama mfano kwetu wa yule ambaye amedhihirisha hilo si kwa maneno tu bali kwa matendo ya upendo. Wafuasi wa Kristo wanapaswa kushuhudia upendo na wema unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, kutokubali kutumia nguvu ni njia ya kuonesha utu unaodhihirisha upendo na nguvu ya Mungu ambayo inapambana na ubaya kwa kutumia upendo na ukweli.

Upendo kwa adui ni kielelezo cha mageuzi katika maisha ya Kikristo; kwa kujibu ubaya kwa wema na wala si kujisalimisha, ili kuvunjilia mbali mnyororo wa ukosefu wa haki msingi! Mama Theresa wa Calcutta anasema familia ya binadamu inahitaji kukaa pamoja na watu kupendana ili kujenga na kudumisha amani na wala si silaha za mahangamizi, kwani biashara ya silaha inaendelea kuwatajirisha wajanja wachache katika jamii wakati ambapo kuna mashuhuda wa amani wanaendelea kuwasaidia jirani zao kwa hali na mali. Hawa ni watu wanaosimama kidete: kushuhudia kulinda, kutetea na kudumisha uhai wa binadamu; wanaendeleza moyo wa ukarimu na mapendo; wanaohudumia kwa huruma na upendo; kwa kutambua utu na heshima ya binadamu.

Katika ujumbe wake huo, Baba Mtakatifu ameiweka familia ya mwanadamu kama msingi wa amani kwa wanadamu. Katika familia ndipo mmoja upata fursa ya kujifunza tunu za utu: namna ya kusameheana, kushirikiana, kujitoa kwa ajili ya kuwahudumia wengine na na upendo kwa wote. Katika ukweli wa mambo leo hii ambapo familia imejeruhiwa kwa kiasi kikubwa juhudi za lazima zinahitajika kwa ajili kujenga amani ya kudumu. Hakuna amani ya kweli katika jamii ambayo haithamini tunu ya familia ya mwanadamu, katika jamii ambayo imeigeuza maana ya familia ya mwanadamu.

Tunapoadhimisha sherehe hii na tunapokuwa mwanzoni mwa mwaka huu mpya wa 2017 tuungane na Wana wa Israeli kuipokea Baraka ya Mungu kama alivyowaagiza kupitia Musa na Haruni tukisema: “Mungu akubarikie, na kukulinda; Bwana akuangazie nuru za uso wake, na kukufadhili; Bwana akuinulie uso wake, na kukupa amani”. Ninawatakieni maadhimisho mema na mwanzo mzuri wa mwaka 2017.

Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.