2016-12-30 10:21:00

Kanisa kuendelea kuwalinda na kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji!


Kardinali Antonio Maria Vegliò, Rais wa Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa ajili ya wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum ambalo, kuanzia tarehe Mosi Januari 2017 linafutwa na kuwa ni sehemu ya Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu anasema, Kanisa litaendelea kujizatiti kikamilifu kwa ajili ya huduma kwa wakimbizi na wahamiaji; kwa kulinda haki zao msingi na kuwapatia huduma: kiroho na kimwili.

Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji ni changamoto kubwa na janga la kimataifa linalopaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa kwa kulinda kwanza kabisa: maisha ya watu, amani na usalama; tunza na huduma makini. Kanisa linashiriki kikamilifu katika mchakato wa huduma na haki za wakimbizi na wahamiaji kwa kutambua kwamba hii ni sehemu ya maisha na utume wake ulimwenguni. Baraza hili ni matunda ya mateso na mahangaiko ya watu mara baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia!

Hii ni changamoto iliyovaliwa njuga na Papa Pio XII kuanzia mwaka 1944 na kunako mwaka 1952 akachapisha Waraka wa Kitume unaojulikana kama “Exsul familia” yaani “Familia ya Wahamiaji”; Waraka ambao kwa miaka yote hii umekuwa ni dira na mwongozo kwa ajili ya huduma ya kichungaji kwa wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum ndani na nje ya Italia. Baada ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, Mwenyeheri Paulo VI alilihamasisha Kanisa kushiriki kikamilifu katika majadiliano ya kitaifa na kimataifa mintarafu haki za wakimbizi, wahamiaji na watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa.

Mtakatifu Yohane Paulo II na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI walisimama kidete katika kukuza na kudumisha mchakato wa huduma ya mshikamano na upendo kwa wakimbizi na wahamiaji, bila kuangalia tofauti zao ya kitaifa, kidini, kiimani, kisiasa, kiuchumi na kijiografia! Jambo la msingi ni kuzingatia utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko tangu alipoingia madarakani, ametoa kipaumbele cha pekee kwa wakimbizi na wahamiaji; wahanga wa biashara haramu ya binadamu pamoja na utumwa mamboleo mambo yanayoendelea kudhalilisha utu na heshima ya binadamu na kwamba, huu ni uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji imekuwa ni changamoto pevu kwa Jumuiya ya Kimataifa, kwani kwa wakati huu kuna mambo mengi yanayochangia wimbi hili. Athari za mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha: ukame, mafuriko pamoja na majanga asilia ni kati ya mambo yanayopelekea wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani. Baba Mtakatifu anawahimiza Wakristo kujenga Uekumene wa huduma kwa wakimbizi, wahamiaji na maskini. Kwa Jumuiya ya Kimataifa anaitaka kuwa na sera ya wakimbizi na wahamiaji kimataifa inayojikita katika huduma na hifadhi; kwa kuwa na jicho la pekee: kwa makundi ya watoto, wanawake na wazeee ambayo yanalazimika kukimbia au kuhama nchi zao kutokana na sababu mbali mbali. Mwaka 2017, anasema Kardinali Antonio Maria Veglio’ uwe ni mwaka wa upendo na mshikamano na wakimbizi pamoja na wahamiaji, kwa kujitahidi kufuata mfano bora wa Baba Mtakatifu Francisko, anayetaka makundi haya kuhudumiwa kwa huruma na upendo; kwa haki na mshikamano; kama njia ya ujenzi wa utandawazi wa mshikamano, kwani kwa njia hii, watakuwa wanamhudumia Kristo Yesu, anayejionesha miongoni mwa watu kama hawa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.