2016-12-28 13:03:00

Sherehe ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu!


Mama Kanisa anatualika kuadhimisha Sherehe ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Ni familia ambayo kwayo, familia zote zinapaswa kuchota mifano ya jinsi gani familia za kibinadamu zinapaswa kuwa mbele ya macho ya Mwenyezi Mungu. Leo ni Sherehe ya Familia zote. Familia zetu zote zinaweza kujifunza kutoka familia hii takatifu na kuongezeka kimo katika hekima, nguvu na kuifanya neema ya Mungu kuwa ndani yake. Sherehe hii kwa kawaida huadhimishwa Dominika inayofuata baada ya Sherehe ya Noeli lakini pale Dominika hiyo inapokuwa ni siku ya mwanzo wa Mwaka mpya basi huangukia tarehe 30 ya mwezi Desemba.

Katika Somo la Kwanza, Yoshua bin Sira kwa ujumla anatuelezea wajibu wa watoto kwa wazazi wao. Neno lake kwao ni sawa na tuambiavyo katika amri ya nne kwamba, “waheshimu baba na mama yako upate miaka mingi na heri duniani” Yapo mengi ambayo sisi kama watoto tumeyapokea kutoka kwa wazazi wetu. Kwanza kabisa kutuleta duniani, kutulea, kutupatia mahitaji muhimu, kutupatia ulinzi wakati tukiwa hatujiwezi pengine kwa udhaifu wa udogo wetu au ugonjwa n.k. Hayo yote ni wajibu wake kwa mtoto wake, na kila mzazi anaona fahari na kamwe hasukumwi na lolote zaidi ya kufanya kwa hiari yake.

Kutokana na hili ndio maana Bin Sira anaandika hivi kuhusu wajibu wa watoto kwa wazazi wao. Waheshimuni wazazi wenu, wapeni nguvu, wapeni tena matumaini. Msiwahuzunishe wazazi wenu kwani mzazi kama mzazi anafurahia kuona mwanae anapata mafanikio na anazidi kuwa na heshima katika jamii. Pale mtoto anapofanya hivyo basi bin Sira anasema kuwa “atafanya malipizi ya dhambi, …atawafurahia watoto wake mwenyewe, …akiomba dua atasikiwa, …ataongezewa siku zake”  Lakini pale mtu anaposhindwa kuonesha heshima kwa wazazi atawahuzunisha, atawafanya wakate tamaa.

Katika Somo la Pili, maneno ambayo Paulo anawaambia Wakolosai ni ya msingi kabisa katika Ndoa zetu za Kikristo, katika familia zetu. Maneno mawili, yaani utii na upendo ndizo nguzo katika uimara wa familia. Mtume Paulo pia anaelezea kwa uzuri kabisa jinsi nguzo hizo mbili zinavyoweza kufanikishwa katika familia zetu, ni kwa vipi? Ni pale tu kila mmoja anapokwa tayari kujivika moyo wa rehema, yaani, kuwa na huruma kati yao, kuchukuliana na kusameheana, kila mmoja kuwa na unyenyekevu, kila mmoja kuwa tayari kujishusha na kumpatia mwenzie nafasi ya kutoa maoni na vipaji vyake, kuacha udikteta ndani ya nyumba, kuwa na fadhila ya upole, kuwa na uvumilivu na kujivika upendo kwani hiko ni kifungo cha ukamilifu.

Ni kana kwamba sisi wazazi ambao tupo tayari katika ndoa zetu tunarudishwa katika siku ile ambayo tulifunga ndoa zetu, nasaha na mawaidha mengi toka kwa wazazi wetu, ndugu jamaa na marafiki na hata mafundisho ya kanisani yalilenga katika hilo moja  la utii na upendo kwani vitawawezesha kufikia katika ukamilifu wa maisha ndani ya familia zetu.

Katika Somo la Injili tunapewa kwa vitendo hayo ambayo tumeyatafakari. Tunayaona katika Familia takatifu, familia ya Yesu, Maria na Yosefu ambapo kila mmoja katika familia anachukua nafasi yake kuimarisha familia hiyo ya Nazarethi. Kwanza ni familia ambayo ina uhusiano mwema na Mwenyezi Mungu na inajitahidi kumrithisha mtoto wao kushiriki katika shughuli zao zote za kidini. Pia familia hii inaonekana ni ile yenye umoja na inayopenda kukaa pamoja kama familia. Hili linadhihirishwa na kule kuwa pamoja wanapoelekea katika kuabudu.

Kwa upande mwingine wazazi katika familia hii wanautekeleza vema wajibu wao wa kumlea vema mtoto wao, Injili ya leo inamalizia kwa kutueleza kuwa mtoto huyu alirudi pamoja na wazazi wake nyumbani kwao Nazarethi na akaendelea kukua, kuongezeka nguvu na kuwa na neema ya Mungu. Haya yote bila shaka yamewezeshwa na malezi bora kutoka kwa wazazi wake. Kama tunavyosoma katika vitabu vya “apokrifa” vitabu vile vinavyoelezea maisha ya Kristo ambavyo havikuwa rasmi kuwa Yosefu alimuandaa Kristo kuwa Kijana mzuri wa Kiyahudi na kumfunza kazi mbalimbali ikiwemo kazi yake ya useremala na ndiyo maana sehemu nyingi anaitwa “mseremala” au “mwana wa seremala” (Mat 13:55)

Pengine leo tunapewa changamoto ya kuangalia tena jinsi familia zetu zinavyorandana na familia hii ya Nazareti. Sote tunashuhudia mmomonyoko mkubwa wa maadili katika familia zetu, kwa watoto wetu. Kwa watoto wengi wa jamii yetu leo tunaweza kushuhudia jinsi ambavyo mawaidha yale ya Bin Sira yalivyowapitia mbali. Heshima kwa wakubwa hakuna kabisa, na kana kwamba wao wenyewe ndio wamejileta duniani. Hakuna tena cha kuwasikiliza wakubwa. Inaleta huzuni kwa wazazi wengi na pia matokeo yake ni mabaya kwa watoto hawa.

Pale wazazi wetu wanapotuelekeza katika hili na lile hawana nia ya kutukomoa, wameona mbali, wanao uzoefu wa maisha, wanapenda sisi kama watoto wao kuwa na ufanisi katika maisha yetu ya kila siku kwani hiyo ndiyo pekee furaha katika maisha yao, ufanisi wa maisha ya watoto wao. Pata uhakika wa upendo wa wazazi wako, hebu fikiri wakati ukiwa bado ni mtoto mchanga walikujali vipi, walikuhangakia vipi, kwa vipi leo wasiwe na upendo kwako? Ni wakati mwingine leo sisi watoto kujipatia changamoto katika maisha yetu. Ni vipi unawajali na kuwatunza wazazi wako! Uwezo ulio nao vipaji ulivyo navyo ni kutoka kwa mwenyezi Mungu lakini vimepaliliwa na kukuzwa katika mikono ya wazazi wako.

Mbaya zaidi hata baina ya wazazi hivi leo hakuna maadili. Baba na mama ndani ya familia wana jukumu la kuzistawisha familia zao na kuzifananisha na na familia hii ya Nazareti. Pale baba na mama wanaposhindwa kuheshimiana na kupendana, yaani, kila mmoja kuwa na lake ndiyo mwanzo wa kusambaratika. Familia ya namna hii haitakuwa na umoja, uelewano wala kuonyana, na pengine wazazi watashindwa kuwa kielelezo cha maadili kwa watoto wao na hapo mmomonyoko wa maadili ni dhahiri. Kwa wazazi, Mtume Paulo anatupatia nyenzo katika somo la pili kuwa “…ninyi wake watiini waume zenu…ninyi waume wapendeni wake zenu…” (Kol 3:12-21).

Kuwa na utii na upendo ndani ya familia kunaonekana pale wazazi wanaposikilizana baina yao, wanapoheshimiana baina yao na kwa hakika hapa wanakua mfano kwa watoto wao na jamii kwa ujumla. Kwa upande mwingine wapo wazazi ambao wanakimbia wajibu wa malezi, wajibu ambao kila mmoja kati ya wanandoa aliukubali siku ndoa, “…Je, mko tayari kuwalea watoto mtakaopewa na Mungu na kuwalea kama ilivyo sheria ya Kristo na Kanisa lake”  Lakini ni wangapi wapo tayari kudhihirisha hili katika jamii yetu ya leo? Wazazi wengine hukimbia wajibu huu ama kwa kutolea kabisa au kuwalea si kama tunavyoelekezwa na sheria ya Kristo na Kanisa lake. Tunakuwa tayari kuwarithisha watoto wetu hekima za dunia hii, starehe za dunia hii na kushindwa kuwarithisha maadili ya kidini, kupenda mambo ya kimungu n.k.

Kwa kuhitimisha tafakari hii ni vema tukaipembua kidogo familia ya mwanadamu katika ulimwengu mambo leo. Mwelekeo wa kidunia leo hii unahatarisha uwepo wa familia ambayo inapaswa kuwa chimbuko na msingi wa utu wa mwanadamu. Propaganda za kijinsia ambazo zinaenezwa na wapinga imani au na mirengo ya kisiasa ya kisoshalisti au kwa ujumla propaganda ambazo zinapigiwa chapuo na malimwengu zinajitahidi kuwasawazisha binadamu katika usawa. Tofauti zetu za kijinsia zinaondolewa kwa makusudi na kuwataka watu wajisikie kuwa wote wapo sawasawa, kinyume kabisa cha mpango wa Mungu katika kazi ya uumbaji!

Juhudi hizi hufanywa kwa kuwaelekeza watoto wetu kupitia mifumo ya kielimu matokeo ambayo uharibu hata maana nzima ya familia. Matokeo yake ni kuzuka kwa mahusihano ya kijinsia yasiyo ya asili na yanayokinzana na ile hadhi ya ubaba au umama ambayo tumewekewa tangu asili na Muumba wetu. Kwa upande mwingine wanadamu wanabaki kushughulika na mambo ya ulimwengu zikiwamo kazi, biashara na starehe mbalimbali bila kutilia maanani majukumu yao ya kifamilia kadiri ya jinsia zao.

Zao linalotokana na muoenkano huu ni jamii tunayoiona leo hii. Akina mama wengine wanapoteza ile tunu ya umama ya kutoa malezi msingi ya kiutu kwa watoto wao. Inakuwa ni vigumu kwao kuicheza vema nafasi yao hii nyeti kwani wanazingirwa zaidi na shughuli za ulimwengu huu au kujitafutia usawa na wanaume hata katika majukumu yao ya kimama ndani ya familia. Kwa upande mwingine wanaume wengi wanapoteza ile hali ya kujisikia ubaba na hivyo kuwaacha watoto wao wakilelewa katika namna isiyo na uwiano wa kijamii wa kuwa na baba na mama.

Mazao haya tayari yameanza kuonesha atahari zake katika jamii zetu hasa kwa kuusambaratisha utu wa mtu. Leo hii mwanadamu anakuwa bila kuwa na msingi wa kifamilia iliyo shule ya upendo na chemchemi ya utu. Ubinafsi wetu utujengea chuki, tunakuwa watu tusio tayari kujitoa kuwahudumia wengine, hatuwezi kuiona nafsi yetu ndani ya watu wengine kwa sababu ya kuisambaratisha tunu hii ya familia. Hivi basi, katika adhimisho hili la leo, tuiombe hii Familia Takatifu ya Nazarethi iwe mfano na nguvu katika familia zetu, na kwa neema za Mwenyezi Mungu tuzifananishe familia zetu na Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Nawatakia Sherehe njema katika familia zetu.

Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha. 








All the contents on this site are copyrighted ©.