2016-12-27 12:36:00

Tunzeni mbegu ya wito na maisha ya Daraja Takatifu!


Wito wa Daraja Takatifu ya Upadre ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambayo inapandikizwa katika baadhi ya nyoyo za waamini. Hii ni changamoto inayopaswa kufanyiwa kazi na Mama Kanisa ili kuhakikisha kwamba, wale wanaotamani kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake wanapata majiundo makini na endelevu katika maisha na utume wao, ili kuzaa matunda ya ukomavu katika maisha na wito wa Kipadre. Baba Mtakatifu Francisko anasema huu ni wito ambao hauna budi kulindwa na kukuzwa kwani ni sawa na dhahabu safi inayopaswa kung’ara katika maisha ya familia ya Mungu.

Askofu Bruno Pius Ngonyani wa Jimbo Katoliki Lindi, Tanzania amesema kuwa baada ya kupita miaka 100 tangu Uinjilishaji ufanyike kwenye eneo la Jimbo Katoliki la Lindi hatimaye, Wamisionari wa Waafrika maarufu kama “White Fathers”, wameingia Jimboni humo baada ya kumpata mmisionari wa kwanza wa Shirika hilo mzaliwa wa Parokia ya Nyangao Jimboni humo kuwa Padre. Hayo aliyaeleza kwenye sherehe za kutoa Daraja ya Upadre kwa Shemasi Kondrad Simon Milanzi zilizofanyika hivi karibuni katika Kanisa la Mtakatifu Walburga la Nyangao, sherehe ambazo zilihudhuriwa pia na idadi kubwa ya Wanashirika hilo wakiongozwa na Mkuu wa Shirika la Wamisionari wa Afrika nchini Tanzania, Padre Batholomew Mroso.

Akihubiri kwenye adhimisho hilo, Askofu Ngonyani alisema kuwa Kanisa ni la Kimisionari dhana inayopewa kipaumbele cha kwanza katika mchakato wa Uinjilishaji mpya; mazingira ambayo yanamfanya kila Mkristo awe Mmisionari kwa kuwa Kristo mwenyewe alikuwa mmisionari, changamoto ni kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya ushuhuda wa maisha! Alisema kupatikana kwa Padre mmisionari ambaye ni mzaliwa wa Parokia hiyo, ni changamoto kwao kwa kuwa nao wanapaswa kushiriki Umisionari wake kwa kumsaidia kwa hali na mali kusudi kumwezesha kutekeleza Utume wake huko ambako atatumwa na Wakuu wa Shirika lake.

“Ninyi waamini wa Parokia hii ya Nyangao mjitambue kuwa tangu Ukristo uingie kwenye eneo hili mwaka 1896, huyu Mwana wenu, Padre Kondrad atapelekwa sehemu mbalimbali, hivyo mkiwa wazazi fahamuni  nanyi mtashiriki huo Umisionari ndani yake”, alikazia Askofu. Alihitimisha nasaha zake kwa Wanaparokia ya Nyangao kwa kuwataka wazidishe mshikamano miongoni mwao wenyewe, mshikamano na wanajimbo lote la Lindi na hatimaye, akawahimiza kuwaombea Mapadre wa Jimbo na wa Ulimwengu ili watekeleze vyema maisha na wito wao kama Wamissionari wenye mvuto na mashiko katika maisha na shughuli zao za kichungaji! Aidha Askofu Ngonyani alimhusia Padre Milanzi afanye kazi ya Kristo aliye kichwa na mchungaji mkuu, huku akiwaunganisha waamini katika jamaa moja.Na kwamba, aige mfano wa Mchungaji mwema Kristo ambaye hakuja kutumikiwa bali kutumikia na kuokoa kilichopotea.

Naye Mkuu wa Wamisionari hao hapa nchini,Padre Mrosso amemshukuru Mungu kwa kuwajalia Padre mpya, alimshukuru Askofu Ngonyani na hatimaye aliwashukuru wazazi wa Padre Milanzi pamoja na wanaparokia wote wa Nyangao kwa kushiriki kwa namna moja au nyingine katika malezi ya Mwanashirika mwenzao na kumalizia kutangaza kuwa Padre huyo mpya amepangiwa kutoa huduma katika Jimbo Kuu la Durban, Afrika ya Kusini katika Jumuiya ya Wamisionari wa Afrika wanaohudumia Parokia za Henley KwaMzimba na Parokia ya Mtakatifu Vincent, Kwa Mphumuza. Kupatikana kwa Padre Milanzi wa Shirika la Wamisionari wa Afrika kunaifanya Parokia ya Nyangao kuwa na mapadre wawili Wamisionari baada ya Padre Titus Nkane,OSB kujiunga na Shirika jingine la Kimisionari la Mtakatifu Benedikto lenye makao yake Makuu huko Ndanda, Jimboni Mtwara. Pamoja na mapadre hao wawili wa Shirika, Parokia hiyo iliyoanzishwa kunako mwaka 1896  ina Mapadre wanne wa Jimbo.

Na Padre Anthony Chilumba.

Jimbo Katoliki la Lindi, Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.