2016-12-27 11:17:00

Huruma na haki: Jengeni utamaduni wa kusikiliza Neno la Mungu!


Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, ni wakati mwingine tena wa kuendelea kutafakari kiundani, ule ujumbe wa  Barua ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko,  ijulikanayo kama “Misericordia  et misera”, yaani Huruma na amani. Katika barua   hii, Baba Mtakatifu anatuasa kwamba,  kusikiliza Neno la Mungu  ni kitu muhimu sana katika maisha ya mkristo na mwanadamu  kwa ujumla.  Anatuambia kila Jumapili Neno la Mungu   linatangazwa  kwa kila Jumuiya  ya wakristo ili Siku ya Bwana ipate kuangaziwa na mwanga wa Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo!

Katika adhimisho la Ekaristi  Takatifu, anendelea kutuambia Baba Mtakatifu, ndiyo sehemu muhimu ambapo  tunashuhudia  mahaojiana ya ndani baina  ya mkristo na Mungu, yaani mahojiano ya kiliturujia  na hapa mkristo, hupata kuingia  ndani katika kutafakari Neno la Mungu na kuisikia sauti ya Mungu inenayo ndani yake na hivyo,  kutuwezesha kutafakari zaidi safari yetu ya wokovu,  katika kutangaza kazi ya huruma ya Mungu isiyokuwa na mwisho.

Mungu anendelea kuongea nasi leo hii kama rafiki, na hasa katika Maandiko Matakatifu  ili tu apate kutusindikiza  katika safari ya maisha. Na ni  katika  Maandiko Matakatifu,  tunaona na kujifunza  matendo makuu ya Mungu yahusuyo huruma, na hivyo kila mmoja wetu anapata kushiriki  upendo wa kimungu toka mwanzo wa  Uumbaji,  na hii ndiyo  alama ya upendo wa Mungu kwa ulimwengu. Kupitia maneno ya  Manabii na Maandiko ya Hekima, Roho Mtakatifu anafanya upya historia ya Wana wa Israeli kama alama ya kutambua   Huruma ya Mungu  na ukaribu wa Mungu kwa mwanadamu, ingawa mara nyingi mwanamu huyu amekuwa ni mdhambi na hata kutokuwa mwaminifu katika njia ya kumcha  Mungu.

Hivyo, hakika ujio wa Kristo  na mafundisho yake, umeanzisha  historia mpya  katika Jumuiya ya mwanadamu. Katika ujio huu wa Kristo tunatambua maana ya juu kabisa ya Huruma ya Mungu na msamaha, na hii  inatuletea amani nafsini mwetu kwani, kupitia kwa Kristo tunapanishwa na Mungu na kuwa wana wa  Mungu.  Kupitia Maandiko  Matakatifu  ambayo daima yamewekwa hai katika  Kanisa,  Kristo  anaendelea kuongea na Kanisa  na hivyo kuendelea kuliwezesha Kanisa kufikisha Injili kwa kila kiumbe. Injili hii ndiyo Habari Njema, habari iletayo matumaini, habari iletayo wokovu na habari  iletayo  amani nafasi mwetu. Katika kusikiliza Habari Njema yaani Injili,  hasa  kila Jumapili ambapo pia ni  jukumu la kila mkristo, tunapata utajiri wa neema za  Huruma ya Mungu nafsini mwetu, na kuendelea kutufanya tuwe  na  hamu ya kusonga mbele na  kutaka kutafakari kila wakati Maandiko Matakatifu, Anasema  Baba  Mtakatifu.

Hivyo ndugu yangu, barua hii ya kitume ya Baba Mtakatifu, ifufue upya ndani mwetu  hamu ya  kupenda  kusoma, kusikiliza na kutafakari tena zaidi na zaidi Neno la   Mungu ili kupata kufanywa wapya katika  Bwana. Nakutakia heri na baraka katika kuzidi kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika matendo, kielelezo cha imani tendaji. Kwa namna ya pekee, kabisa Baba Mtakatifu Francisko anawataka Mapadre kuandaa vyema mahubiri yao ili kutangaza Ukweli na Uzuri wa Injili unaowafunuliwa waamini huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Mahubiri na Katekesi ambayo kimsingi ni muhtasari wa: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha adili na Sala inapaswa daima kuchota utajiri wake kutoka katika Maandiko Matakatifu.

Kutoka katika studio za Radio Vatican ni mimi, Padre, Agapiti Amani, ALCP/OSS.








All the contents on this site are copyrighted ©.