2016-12-26 13:35:00

Mshikamano wa upendo kutoka kwa watoto wa Ujerumani!


Mama Kanisa anaadhimisha Siku kuu ya Tokeo la Bwana, maarufu kama "Epifania" kila mwaka ifikapo tarehe 6 Januari. Hii ni siku pia ya Utoto Mtakatifu, shule ya upendo, huruma, ukarimu, umissionari na mshikamano wa upendo miongoni mwa watoto wadogo kwa njia ya sadaka na majitoleo kwa watoto wenzao sehemu mbali mbali za dunia! Baba Mtakatifu Francisko anawaalika watoto kuwa ni mashuhuda wa huruma na mapendo kwa watoto wenzao ambao hawakubahatika kama wao, ili kuwaonjesha ule upendo na furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake!

Shirika la Utoto Mtakatifu nchini Ujerumani kwa muda wa miaka 59 limekuwa likikusanya fedha kutoka kwa wazazi, ndugu, jamaa na Wasamaria wema katika kipindi kuelekea kwenye Sherehe ya Tokeo la Bwana. Maadhimisho haya kwa Mwaka 2017 yanaongozwa na kauli mbiu “Kutoa baraka ili kupata baraka. Pamoja kwa ajili ya kutunza mazingira” nchini Kenya na sehemu mbali mbali za dunia”. Watoto kutoka Ujerumani wanataka kuonesha mshikamano wao wa huruma na upendo kwa watoto ambao wameathirika na mabadiliko ya tabianchi eneo la Turkana, nchini Kenya.

Watoto hawa kwa njia ya sadaka na majitoleo yao wanataka kujenga madaraja ya watoto kukutana na kusaidiana na watoto wenzao kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ili kudumisha mshikamano wa huruma na upendo unaowajibisha na kuguswa na mahangaiko ya wengine anasema Monsinyo Klaus Kramer, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Utoto Mtakatifu nchini Ujerumani. Watoto hawa wakiwa wamevalia kama Mamajusi kutoka Mashariki ya Mbali, katika kipindi hiki cha Noeli, watapita nyumba kwa nyumba wakiimba nyimbo za Noeli na kutoa baraka katika nyumba hizo kwa kuandika alama ya “C+M+B” kirefu chake “Christus Mansionem Benedicat” yaani “Kristo Bariki Nyumba hii” ili kuchangisha fedha kutoka kwa Wasamaria wema kwa ajili ya kugharimia miradi ya watoto wenzao wanaoteseka sehemu mbali mbali za dunia.

Shirika la Utoto Mtakatifu nchini Ujerumani maarufu kama “Star Singers” “Die Sternsinger” limekuwa ni mtandao mkubwa wa upendo na mshikamano miongoni mwa watoto wa Ujerumani kwa ajili ya kuwasaidia watoto wenzao sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu Francisko, hivi karibuni alipokutana na Timu ya Taifa ya taifa ya Mpira wa Miguu nchini Ujerumani aliipongeza kwa kuchangia juhudi zinazofanywa na Shirika la Utoto Mtakatifu nchini Ujerumani kwa ajili ya watoto maskini duniani. Hiki ni kielelezo makini cha jinsi ambavyo, familia ya Mungu duniani inaweza kuvunjilia mbali kuta za mambo yanayo nyanyasa watu kwa kujenga madaraja ya upendo na mshikamano na maskini pamoja na wahitaji. Kwa njia hii wachezaji hawa pia wanashiriki katika mchakato wa ujenzi wa jamii inayosimikwa katika haki, umoja na udugu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.