2016-12-24 08:06:00

Ujumbe wa Noeli kwa familia ya Mungu nchini Haiti!


Baraza la Maaskofu Katoliki Haiti baada ya maadhimisho ya Mkutano wake mkuu wa 123 hivi karibuni uliofanyika huko Lilavois, limetuma ujumbe wa Noeli na matashi mema kwa mwaka mpya wa 2017, kwa kuitaka familia ya Mungu nchini Haiti kuondokana na utamaduni wa kifo unaojikita katika kinzani, vurugu na mipasuko ya kijamii na kisiasa na badala yake, wajikite katika utamaduni wa haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa, ili kweli waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya furaha, amani na upendo!

Baraza la Maaskofu Katoliki Haiti linasikitika kusema kwamba, kwa muda mrefu familia ya Mungu nchini Haiti imejikuta ikiogelea katika mateso, kinzani na mipasuko ya kijamii na kisiasa kama ilivyojitokeza hivi karibuni baada ya kutangaza matokeo ya Uchaguzi mkuu na athari kubwa zilizosababishwa na tufani ya “Mathew”. Maaskofu wanawataka wanasisasa na watunga sera nchini Haiti kuwajibika barabara, kwani kwa muda mrefu familia ya Mungu nchini Haiti imedanganywa na kupuuzwa sana na viongozi wake wa kisiasa.

Matokeo yake ni hali ya watu kuchanganyikiwa, kukosa imani kwa viongozi wao wa kisiasa pamoja na kujikatia tamaa ya maisha kama ilivyoshuhudiwa wakati wa mchakato wa uchaguzi mkuu. Kwa mara ya kwanza katika historia, wananchi walioshiriki katika uchaguzi huu ni sawa na asilimia 21% ya wananchi wote waliokuwa na haki ya kupiga kura wakati wa uchaguzi mkuu, hii ni hali ya hatari sana katika mchakato wa ukuaji wa demokrasia, utawala bora, ustawi na mafao ya wengi nchini Haiti.

Baraza la Maaskofu Katoliki Haiti linawataka wanasiasa na watunga sera nchini humo kuweka kando ubinafsi na hali ya kujitafuta wenyewe na kuanza mchakato wa ujenzi na uimarishaji wa misingi ya haki, amani, upendo, umoja na mshikamano wa kitaifa ili kuwa na utulivu wa kisiasa na kijamii, kama chachu muhimu sana ya ukuaji wa uchumi na demokrasia ya kweli nchini Haiti. Viongozi wote walioshiriki katika mchakato wa uchaguzi mkuu, sasa waweke kando tofauti na mipasuko yote iliyojitokeza, tayari kushikamana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wote wa Haiti.

Ujumbe wa Noeli na Mwaka Mpya 2017 kutoka kwa Maaskofu wa Haiti unaitaka familia ya Mungu nchini humo kushikamana na kusaidiana kwa hali na mali kama ilivyojitokeza wakati wa kukabiliana na changamoto ya athari za tufani ya “Mathew”. Mwelekeo huu, uendelezwe na kudumishwa hata katika medani mbali mbali za maisha ya wananchi wa Haiti. Kweli, watu wametikiswa na kuchoshwa mno na mahangaiko ya kila siku, sasa wanataka mageuzi yatakayopyaisha maisha ya: kiroho, kiutu, kimaadili, kijamii, kiuchumi na kisiasa.

Ili mchakato huu, uweze kufanikiwa kama unavyokusudiwa na wengi, kuna haja ya kujenga hali na mazingira ya kuaminiana; kugundua na kumwilisha tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kijamii; kwa kusimama kidete kutetea na kumwilisha kanuni maadili, ustawi na mafao ya wengi na kwamba, kila mwananchi wa Haiti anawajibika barabara katika mchakato wa maendeleo endelevu kwa ajili ya Haiti bora zaidi, leo na kesho, sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.