2016-12-24 15:42:00

Salam na matashi mema kwa Papa Mstaafu Benedikto XVI


Baba Mtakatifu Francisko anasema, Noeli ni Siku kuu ya Mwanga na amani; ni muhtasari wa ufunuo wa huruma ya Mungu katika umaskini wa binadamu; ni Siku kuu ya kuonesha upendo, umoja na mshikamano kati ya watu, kwa kutambua ule uzuri wa kupendwa na kuthaminiwa na Mungu katika maisha! Zawadi kubwa inayotolewa na Mwenyezi Mungu katika kipindi hiki cha Noeli ni Mtoto Yesu anayeganga, anayeponya na kuokoa! Ni wakati wa kudumisha upendo kwa jirani!

Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa jioni, tarehe 23 Desemba 2016 alikwenda kumtembelea na kumtakia heri na baraka ya Noeli na Mwaka Mpya 2017, Papa Mstaafu Benedikto XVI. Sasa huu umekuwa ni utamaduni wa Baba Mtakatifu Francisko wakati wa matukio makuu ya Kikanisa kwenda kumtakia heri na baraka mtangulizi wake ambaye kwa sasa “amejichimbia” kwenye Monasteri ya "Mater Ecclesiae” kwa sala na tafakari pamoja na kuliombea Kanisa katika hali ya utulivu na amani ya ndani! Papa mstaafu Benedikto XVI ni amana ya Kanisa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.