2016-12-24 07:47:00

Noeli: Mwenyezi Mungu anabisha hodi katika malango ya maisha yenu!


Askofu mkuu Cesare Nosiglia wa Jimbo kuu la Torino, Kaskazini mwa Italia anasema, Noeli ni Siku kuu ya Familia inayofumbatwa katika upendo, umoja, udugu, urafiki na amani, kwani Yesu, Mwana wa Mungu amefanyika mwili, ili kuwa ndugu yao, hivyo anapaswa kuwa ni chemchemi ya furaha na amani kwa kila familia. Noeli ni kipindi cha kutakiana mema na kupeana zawadi, ni kipindi cha mwanga, kwani sehemu kubwa ya miji inapambwa na taa za Noeli. Lakini, Noeli pia kinapaswa kuwa ni kipindi cha kukuza na kuimarisha imani kwa Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, chemchemi ya amani na upendo unaopaswa kuwa ni dira na mwongozo wakati wa maadhimisho ya Kipindi cha Noeli na Mwaka mpya 2017.

Ni wakati wa kuondokana na ubaridi wa imani, matumaini na mapendo, tayari kuwasha na kushuhudia Imani kwa Kristo na Kanisa lake, kwa kujikita katika imani tendaji na utakatifu wa maisha; mambo yanayohitaji toba na wongofu wa ndani, ili kukoleza na kudumisha upendo na ukarimu. Utajiri wa imani na utamaduni wa Kikristo uwe ni chachu ya ushuhuda wa maisha ya Kikristo anasema Askofu mkuu Nosiglia katika barua yake kwa familia ya Mungu, Jimbo kuu la Torino.

Walimwengu wanatamani kuona na kushuhudia utakatifu wa maisha ya Kikristo unaomwilishwa katika upendo kama sehemu ya kuwashirikisha wengine amana na utajiri mkubwa wa Kanisa unaofumbatwa katika maisha ya kiroho, sera na mikakati ya shughuli za kichungaji; pamoja na huduma ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Huu ni ushuhuda unaopaswa kufumbatwa kwa namna ya pekee katika imani, udugu na mshikamano wa dhati kwa watu wote bila ubaguzi. Kumbe, waamini wawe na ujasiri wa kusikiliza na kujibu changamoto inayotolewa kwao na Kristo Yesu anapowaambia kwamba, “Tazama mimi na simama mlangoni nikibisha hodi”. Kristo anataka kuingia na kushiriki katika maisha ya waamini wake.

Kristo Yesu ni Mwana wa Mungu, Nafsi ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, alikuwepo kabla ya kuumbwa kwa ulimwengu, alikuja kwa watu wake kama anavyosema Mwinjili Yohane, lakini kwa bahati mbaya, watu wake hawakumtambua! Mwana wa Mungu anakuja kati ya watu, lakini bado wanamfungia mlango wa maisha yao, hili ni Fumbo kuu wakati huu wa Noeli. Ni “Immanueli, yaani Mungu pamoja nasi” aliyejifanya mdogo, akazaliwa katika hali ya umaskini na kati ya maskini na wale waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii; anakuja katika hali ya mtoto mchanga asiyeweza kujitetea hata kidogo, changamoto na mwaliko wa kusimama kidete, kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo!

Noeli ni Siku kuu ambayo Mwenyezi Mungu anabisha tena katika malango ya maisha ya wanadamu, katika kila moyo wa mtu na katika kila mlango wa familia. Lakini ikumbukwe kwamba, Noeli kila mwaka inapaswa kuleta upya wa maisha, imani na matumaini. Jambo la msingi ni kumsikiliza kwa makini, kwa kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu kama kielelezo cha imani tendaji. Kipindi cha Noeli, iwe ni fursa ya kutafakari kwa pamoja Neno la Mungu pamoja na kujenga utamaduni wa kusikilizana ndani ya familia badala ya kutawaliwa na kelele za Televisheni na Mitandao ya Kijamii ambayo kwa sasa imechukua nafasi ya juu katika maisha ya watu wengi!

Kipindi cha Noeli kiwasaidie wanafamilia kukaa na kusherehekea kwa pamoja uwepo wa Mwana wa Mungu kati yao pamoja na kuonesha mshikamano wa upendo na maskini na wale ambao kutokana na sababu mbali mbali pengine, hawatapata nafasi ya kuadhimisha Fumbo la Umwilisho kwa furaha, amani na utulivu. Hawa ni wagonjwa, wazee, maskini, wakimbizi na wahamiaji. Ni wakati wa kumwilisha sala, kwa kumshukuru kwa zawadi ya Imani katika Fumbo la Umwilisho, kwa mafanikio na changamoto mbali mbali za maisha, ili kuomba tena huruma na upendo wake kwa ajili ya Mwaka Mpya wa 2017.

Noeli ni kipindi cha kukuza na kudumisha utamaduni wa upendo, umoja na mshikamano. Ni wakati wa kutoa zaidi zawadi na kupokea pale inapokuja kwa moyo wa upendo na ukarimu, Furaha ya kweli inabubujika katika sadaka na majitoleo ya mtu anasema Askofu mkuu Cesare Nosiglia katika barua yake ya Noeli kwa Mwaka 2016. Ni muda wa toba na wongofu wa ndani; kwa kusamehe na kutoa msamaha kwa wengine, ili kuendelea kusherehekea matunda ya Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa kujikita katika huruma, upendo na msamaha wa kweli.

Noeli iwe ni fursa ya kuonesha upendo na mshikamano wa dhati na mihimili ya Uinjilishaji yaani: Wakleri, Watawa na Makatekista ambao wanajisadaka kila siku ili kuhakikisha kwamba, familia ya Mungu inapata: Neno, Sakramenti na huduma ya upendo. Mwelekeo huu udumishwe pia katika umoja na ushiriki mkamilifu katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, furaha, upendo na sadaka na majitoleo yanayoendelezwa ndani ya familia ambayo kimsingi ni Kanisa dogo la nyumbani! Shule ya sala, upendo, ukarimu, msamaha na amani. Mwishoni kabisa mwa barua yake kama zawadi ya Noeli kwa Mwaka 2016, Askofu mkuu Cesare Nosiglia anawatakia heri na baraka kwa Siku kuu ya Noeli na Mwaka Mpya 2017. Noeli kiwe ni kipindi cha kuimarisha imani, upendo, matumaini na mshikamano, tayari kumfungulia Kristo Yesu, malango ya maisha yao ili aweze kutembea pamoja nao katika historia yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.