2016-12-24 07:23:00

Noeli ilete maisha mapya na kujenga mshikamano!


Leo ni Sherehe ya kuzaliwa Bwana wetu Yesu Kristo, Ni Sherehe ya Noeli. Mwokozi Bwana wetu Yesu Kristo amezaliwa Bethlehemu, pangoni katika hori la kulishia Ng’ombe. Pamoja na kwamba katika Kalenda ya Mwaka wa Liturjia ya Kanisa kipindi cha Pasaka ndicho kinachowekwa kama kilele cha maadhimisho yote, sherehe ya leo inapata pia umaarufu mkubwa kwani Ukombozi wetu huo ambao tunausherehekea katika Majira ya Pasaka unakuja baada ya Mkombozi huyo kuja duniani na tukio hilo ndilo tuliadhimishalo katika sherehe ya leo.

“Miisho yote ya dunia imeuona wokovu wa Mungu wetu”. Kiitikio hiki cha wimbo wa katikati wa liturujia ya leo kinaweka mbele yetu kwa muhtasari maadhimisho yetu ya leo, yaani kufunuliwa kwa ukombozi wa mwanadamu wakati Mungu mwenyewe aliposhuka na kuuchukua ubinadamu wetu. Mwana wa Mungu amezaliwa, amekuwa ndugu yetu ili sisi tuupate uzima wa milele. Amekuwa ndugu yetu na hivyo pote pote ulimwenguni ambapo ubinadamu umeenea wokovu huo unapenyezwa.

“Naye Neno alifanyika Mwili, akakaa kwetu” (Yoh 1:14). Mungu ameshuka chini, amejivika asili yetu ya kibinadamu kusudi tupate kuinuliwa, ameuchukua udhaifu wetu kusudi tupewe nguvu. Tuungane na mama yetu Bikira Maria kuimba Magnificat kwa Mwenyezi Mungu, “…kwa kuwa ameutazama unyonge wa mjakazi wake” (Lk 1:48). Kwa hakika tumeinuliwa na kukweza na Mwenyezi Mungu. Mtoto huyu anayezaliwa kwetu tunaambiwa na mwinjili Yohane leo kuwa ni Neno la Mungu, ambaye anachukua mwili na kukaa kwetu.

“Neno” lina kazi ya kutoa ujumbe ambao mtu amekusudia kuwapa watu Fulani, kuelezea yale yaliyo moyoni mwake, kuelezea mipango yake na jinsi ambavyo hao anaowaambia anavyopenda washiriki katika hayo aliyo nayo. Ndivyo anavyokuwa Kristo, mtoto aliyezaliwa leo kwetu, kwamba yeye ni Neno la Mungu. Katika fumbo hili la Umwilisho anajivika ubinadamu wetu, anaongea kama sisi, kuishi kama sisi na kufanya kama sisi isipokuwa hakutenda dhambi ili atueleze kuhusu Baba, sisi ni nani kwa Baba na mipango yake aliyonayo kwa ajili yetu sisi. Tunaitwa tena na Mungu katika upendo wake mkuu kuitambua tena hadhi yetu ambayo ilichakazwa na dhambi kama mahubiri ya Papa Leo Mkuu kwa siku hii yanavyotuhasa: “Ewe mwanadamu, kitambue tena cheo chako”.

Ubinadamu unaunganika na umungu na kufanywa kuwa washiriki katika amana za kimbingu. Mungu hayupo tena mbali nasi. Anakuwa ndugu yetu. Mtakatifu Ireneo anasema: “Ni kwa namna gani mwanadamu angeweza kwenda kwa Mungu kama si Mungu mwenyewe kuja chini katika ubinadamu wetu? Ni namna gani mwanadamu anaweza kujikomboa kutoka katika hali yake ya kifo kama si kwa njia ya kuumbwa tena kwa njia ya imani kunakotujia bila malipo kutoka kwa Mungu wetu, ujio huo unatufikia kupitia tumbo la bikira”.

Neno la Mungu amefanyika mwili kusudi mwanadamu afanywe kuwa mwana mrithi wa Mungu. Huu ni muunganiko wa ubinadamu wetu na umungu, muunganiko ambao uliharibiwa na dhambi. Mungu anakuwa raia mwenzetu, akiishi pamoja nasi na kutuwekea ngazi yake ya kimungu kusudi nasi tuweze kuwa kama yeye. Ni uwepo gani wa kimungu tunaoweza kuwa nao ndani mwetu unaopita hali hii ya kufanyika wana wa Mungu? Ni kwa njia ya fumbo hili tunaloliadhimisha leo ambalo kwalo mwanadamu amewezeshwa kuwasiliana tena na Mungu kwa njia ya neema.

Matendo yote ambayo yanatutenga na Mungu hujeruhi mahusiano yetu na Mungu na hivyo hadhi yetu ya kibinadamu husambaratishwa. Hivyo tunapaswa kuisherehekea siku hii ya leo kwa shukrani na furaha kuu. Neno la Mungu, Bwana wetu Yesu Kristo amefanyika mwili. Yeye ni Yule Yule jana, leo na hata milele. Ni muujiza mkubwa katika historia ya mwanadamu; tunaumbwa tena si kama viumbe vipya bali tunarudishiwa tena hadhi yetu ya tangu kale. Sherehe hii inauthibitisha ukamilifu wetu, inaturudisha katika asili yetu.

Mwanadamu anapaswa kuuacha utu wake wa kale na kuuvaa utu mpya, kwa hakika kila mmoja wetu sasa anapaswa kusema kama asemavyo Mtume Paulo kwamba “kwangu mimi kuishi ni Kristo na kufa ni faida….” (Fil 1:21). Na kama tunavyoaswa na Baba Mtakatifu Leo Mkuu katika mahubiri yake ya Sherehe ya leo kuwa “tuuvue utu wetu wa kale na yale yanayoendana nayo, tushiriki sasa katika kuzaliwa kwake Kristo, tuvunjilie mbali matendo ya mwili …..tusimfukuze Roho Mtakatifu aliye ndani yetu kwa matendo ya giza na kujikabidhisha tena kwa shetani. Kwa sababu tumenunuliwa kwa thamani ya Damu Azizi ya Kristo”.

Sherehe hii ya Noeli inatudai sisi kuwa mashahidi wa upendo wa kindugu kwa wengine. Tunapompokea Kristo kwa imani na kuzaliwa kweli ndani mwetu tunakuwa ni habari ya furaha kwa wengine. Nabii Isaya katika somo la kwanza anaionesha hali hiyo kuwa ni jambo la heri kwa ubinadamu wote: “Jinsi ilivyo mizuri juu ya milima miguu yake aletaye habari njema … aiambiaye Sayuni, Mungu wako anamiliki! Hivyo sherehe hii haipaswi kuishia kuwa furaha binafsi bali ni furaha inayoenea kwa watu wote. Neno la Mungu anapotwaa mwili ndani mwako anaendelea kuwaangazia wengine kwa matendo ya furaha na neema.

Tunafanywa kuwa vyombo vya kuieneza furaha hiyo kwa wote au kama tulivyoaswa na Nabii Isaya wakati wa Dominika ya tatu ya Majilio kuwaambia wenye mioyo ya hofu wasiogope na wajipe moyo. Hivyo tutafakari mahusiano yetu katika ngazi mbalimbali: katika familia zetu, jamii yetu na hata kati ya wana Kanisa. Tafakari yetu hiyo ilifanye adhimimisho ili kutufikisha katika roho wa kimisionari ya kuufunua wokovu wa Bwana kwa watu wote. Hili linatimilizika katika mambo madogo na ya kawaida kwa kutimiza nyajibu zetu mbalimbali kadiri ya miito yetu.

Mwanadamu anapotenda lile linalotarajiwa na jamii nzima na kwa faida ya jamii nzima hapo ndipo anapokuwa mmisionari wa kweli. Lakini hilo linalotarajiwa na wote kwa ajili ya wote linapaswa kuwa na asili yake kwa Mungu aliye Baba wa wote na ambaye Mwana wake wa pekee leo hii amevaa ubinadamu wetu na amekuwa ndugu yetu. Tuifurahie siku hii ya leo kwa namna hii na hakika “ncha zote za dunia zitauona wokovu wa Mungu wetu”.

Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.