2016-12-24 14:43:00

Mshikamano wa upendo na watu wanaoteseka Mashariki ya Kati!


Viongozi wakuu wa Makanisa Mashariki ya Kati katika ujumbe wao kwa Siku kuu ya Noeli kwa Mwaka 2016 wanasema, hali ya kisiasa, kijamii na kiuchumi huko Mashariki ya Kati bado ni tete sana kutokana na vita, kinzani na mipasuko ya kijamii na kidini inayoendelea kujitokeza kila kukicha katika eneo hili. Kuna makundi makubwa ya wahamiaji na wakimbizi wanaotamani kupata fursa ya kurejea tena kwenye makazi yao lakini bila mafanikio.

Kimsingi, familia ya Mungu huko Mashariki ya Kati ina tamani kuona misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu inatawala katika akili na nyoyo za watu kwani wamechoshwa na vita inayowaneemesha wajanja wachache katika jamii! Watu wanataka amani ya kudumu nchini Siria, Israeli na Palestina, ili kweli watu waweze kujenga na kudumisha utamaduni wa kukutana na kusaidiana katika maisha badala ya kuangaliana kwa “jino pembe”. Hii ni changamoto inayotolewa na Padre Francesco Patton, Mlinzi mkuu wa Maeneo Matakatifu nchini Israeli. Waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema huko Mashariki ya Kati wanataka kuonja na kugusa amani katika maisha yao!

Askofu mkuu Samir Nassar wa Jimbo kuu la Damasko katika ujumbe wake wa matumaini ya Noeli anasema, familia ya Mungu nchini Siria ina kiu ya misingi ya haki, amani na upatanisho, ili kujenga umoja wa Kitaifa. Siria inahitaji kwa sasa mambo makuu matatu: amani, msamaha na upendo, kwani kwa muda wa miaka sita sasa, Siria imekuwa chini ya mtutu wa bunduki, dhuluma, nyanyaso na utupu! Kuna watoto ambao wamewapoteza wazazi na walezi wao; watoto ambao hawana makazi tena kwani yameharibiwa na vita, wanaendelea kuishi katika: umaskini, mazingira magumu na hatarishi kama ilivyokuwa kwa Mtoto Yesu wakati wa kuzaliwa mjini Bethlehemu.

Kwa upande wake, Patriaki Louis Raphael Sako wa kwanza wa Kanisa la Wakaldei wa Babilonia katika ujumbe wake wa Noeli kwa Mwaka 2016 anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kujikita katika sala na kumlilia Mungu ili aweze kukomesha vita nchini Siria, Iraq, Yemen na Lybia. Anawataka viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kujifunga kibwebwe ili kumaliza vita huko Mashariki ya Kati kwani kuna watu wanateseka sana, kiasi hata cha kugeuka kuwa wakimbizi na wahamiaji katika nchi zao wenyewe! Noeli ni Siku kuu ya Amani, Upendo na Mshikamano, mwaliko wa kujikita katika amani ya kweli inayoimarishwa katika umoja, udugu na upendo. Noeli ya Mwaka 2016 iwe ni cheche ya matumaini kwa wale wanaoteseka na kukata tamaa.

Naye Askofu mkuu wa Gregory Laham wa III wa Kanisa la Kigiriki la Kimelkiti, anaishuruku familia ya Mungu nchini Yordan kwa kuonesha ushuhuda wa upendo na mshikamano kwa wakimbizi na wahamiaji waliokimbia ili kupata hifadhi, usalama na tunza nchini Yordan. Ukarimu wa wananchi wa Yordan umeacha chapa ya kudumu katika maisha na nyoyo za wakimbizi na wahamiaji wengi huko Mashariki ya Kati. Anaombea amani, ustawi na maendeleo kwa nchi Yordan ili iendele kuwa ni mfano bora wa kuigwa kwa ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi kwenye malango ya nchi yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.