2016-12-24 08:35:00

Amezaliwa Kristo Bwana kwa ajili yenu!


Leo katika mji wa Daudi amezaliwa kwa ajili yenu mkombozi, ndiye Kristu Bwana. Kwa haraka haraka unaweza kuona kwamba matukio ya kibinadamu na ya kimungu yanafanana kabisa. Yesu amezaliwa katika mazingira yanayonuka ufukara. Kuna watoto wengine wa familia maskini wanazaliwa katika mazingira kama hayo hayo ya kimaskini. Yesu alihukumiwa bila haki na kusulibiwa msalabani na kufa juu ya kilima cha Kalvari. Hapo Kalvari unakuta watu watatu wamesulibiwa, yaani Yesu na wengine wawili. Kwa macho ya kibinadamu, matukio haya yanalingana kabisa. Kwa hiyo, kuna kitu gani kinachotofautisha kuzaliwa kumoja na kule kwa mwingine, na kuna kitu gani cha pekee kinachotofautisha kifo kimoja na kingine? Ni kitu gani kinachotofautisha aina moja ya maisha na mengine, au kazi moja ikajulikana kuwa ni takatifu kwa mtu huyu na kazi nyingine ni dhambi kwa mwingine?

Ndugu zangu, kitu kinachotofautisha mambo yanayoonekana kwa nje kuwa ni sawa ni ufunuo. Halafu mambo yanayoonesha tendo gani ni takatifu zaidi kuliko jingine ni matunda au matokeo yake kwa maisha ya milele. Na kinyume chake mambo yanayoonesha matendo gani yametenda na mdhambi au na mtu mbaya, asiye mtakatifu ni matunda au mapato mabovu. Mungu ni ukweli, Mungu ni utakatifu, Mungu mhaki na mwenye hekima kuu. Yeye hadanganyi na hadanganyiki. Yeye ni mwanga wa milele. Kwa hiyo neno la ufunuo ni ushahidi unaotolewa na Mungu.

Kwa hiyo Yesu amezaliwa, na ukiangalia kwa nje, unaona kwamba yeye ni mtoto kama watoto wengine wanaozaliwa hapa duniani. Kumbe kwa watoto wengine wote wanaozaliwa Mungu haoneshi chochote. Wanazaliwa basi! Kumbe, kwa kuzaliwa mtoto huyu Yesu, unaona Mwenyezi Mungu anatuma Malaika kutoka mbinguni na kuwafumbulia wachungaji Fumbo hilo la kuzaliwa kwake. Watu wa dini zote wanaamini juu ya Malaika kuwa ni wajumbe wa Mungu ambao daima wako mbele ya Mungu!

Hao wanafika kwa wachungaji na kuwaangazia utukufu wa Bwana. Kwa hiyo unaona tupo mbele ya ufunuo wa kweli wa mbinguni. Kadhalika unaona woga na mshangao mkubwa na heshima ya uabudu wanayokuwa nayo wachungaji. Angalia malaika avyowaambia wachungaji juu ya mtoto: “Leo katika mji wa Daudi, amezaliwa mkomboni, ambaye ni Kristo Bwana. Leo Betlehemu amezaliwa Masiha, Kristo, mpakwa wa Mungu, amezaliwa kwa ajili yenu.

Ndugu zangu, nami naomba kuwathibitishia jambo ninyi nyote mnaomwabudu Mungu mmoja tu. Mwasema vyema kabisa na kuamini kwamba kuna Mungu mmoja tu na hakuna Mungu mwingine zaidi. Aidha ni vizuri kabisa mnaposema kwamba Mungu huyo hana mtoto. Ama kweli Mungu wetu ni mmoja tu ndiye mwumbaji wa mbingu na dunia. Mwanena vyema kwamba hakuna miungu wengine. Lakini sasa ebu jiulize: Kama Mungu wenu anakuthibitishia, anakufumbulia, anakushuhudia kabisa kwamba leo amezaliwa kwa ajili yenu Mkombozi, Masiha amefika duniani, ambaye ni Yesu na Bwana, kwa nini msisadiki ushuhuda wake? Mnadhani Mungu anaweza kubomoa uwongo?

La hasha Mungu hadanganyi wala hadanganyiki. Yeye ni ukweli, Yeye ni mwanga, Yeye ni utukufu. Katika yeye hakuna giza. Kwa hiyo kama ninyi mna imani kwa Mungu mmoja, yawabidi pia kusadiki kile anachosema na anachokifunua huyo Mungu mmoja. Vinginevyo, imani yenu si ya kweli, siyo kamilifu, siyo timilifu. Maana yake hamna imani na Mungu, kama mnayo basi ni imani ya bora kuishi nayo siyo imani kabisa. Bikira Maria, Mama wa ukombozi, Mama wa Mungu na Kanisa ndiye mwenye imani safi, takatifu na ya kweli. Malaika na watakaifu wa Mungu, muusaidie ulimwengu kusadiki juu ya Masiha wake na Kristo. Ama kweli “Leo katika mji wa Daudi amezaliwa kwa ajili yenu mkombozi, ndiye Kristo Bwana.”

Heri kwa sikukuu ya Noeli.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.