2016-12-23 14:10:00

Mh. Pd. Alexis Aly Tagbino ateuliwa kuwa Askofu wa Kankan, Guinea


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Mheshimiwa Padre Alexis Aly Tagbino kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo Katoliki Kankan, nchini Guinea. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mteule alikuwa ni Jaalimu na mchumi wa Seminari ya Majimbo nchini Guinea. Itakumbukwa kwamba, Askofu mteule Tagbino alizaliwa tarehe 17 Oktoba 1972 huko Jimboni Kankan. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, kunako tarehe 2 Machi 2003 akapewa Daraja ya Upadre.

Katika maisha na utume wake kama Padre, amewahi kuwa Paroko usu kuanzia mwaka 2003 hadi mwaka 2009 kwenye Parokia za St. Pierre et St. Paul na Notre Dame du Rosaire. Kuanzia mwaka 2009 hadi mwaka 2012 aketumwa na Jimbo kuendelea na masomo ya juu kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana na kujipatia Shahada ya Uzamili katika Sheria za Kanisa. Kuanzia Mwaka 2012 akarejea nchini mwake na kuendelea na shughuli za kichungaji kama Mchumi na Jaalim wa Sheria za Kanisa, Seminari kuu ya Benoit XVI huko Conakry na wakati huo huo, akaendelea kuwa Katibu mkuu wa Jimbo Katoliki la Kankan.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.