2016-12-22 08:01:00

Vita na mipasuko ya kijamii ni chanzo kikuu cha biashara ya binadamu


Jumuiya ya Kimataifa ikisimama kidete na kujizatiti barabara kumaliza vita, migogoro, kinzani na mipasuko ya kijamii, itakuwa imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kudhibiti biashara haramu ya binadamu kwenye maeneo ya vita na migogoro duniani. Hii ni changamoto ambayo imatolewa na Askofu mkuu Bernadito Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, Jumanne, tarehe 20 Desemba 2016 wakati alipokuwa anachangia mada kuhusu umuhimu wa kutunza amani na usalama wa kimataifa kama njia ya kudhibiti biashara haramu ya binadamu kutoka katika maeneo yenye vita, kinzani na migogoro ya kijamii.

Biashara haramu ya binadamu inadhalilisha utu na heshima ya binadamu, kwani mtu anageuzwa kuwa kana kwamba, ni bidhaa na watu ambao wamefilisika kimaadili, watu wenye uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka. Watu wanaouzwa kama bidhaa, wakati mwingine wanauwawa kikatili au kutelekezwa njiani, mambo yanayosababisha mateso na mahangaiko ya watu wasiokuwa na hatia. Biashara ya binadamu ni kashfa dhidi ya utu na heshima ya binadamu.

Umefika wakati kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba vyombo vya ulinzi, usalama na sheria vinatekeleza vyema wajibu wake kwa kuwashughulikia kikamilifu wahalifu wote wanaojihusisha na biashara haramu ya binadamu ambayo kwa sasa imegeuka kuwa ni kitaifa na kimataifa. Kumbe, kuna haja ya kuwa na ushirikiano kati ya Serikali mbali mbali na Mashirika ya Umoja wa Mataifa pamoja na wadau mbali mbali ili kuhakikisha kwamba, biashara hii inavaliwa njuga hadi itokomee kabisa.

Itakumbukwa kwamba, hata Kanisa limekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba linapambana na biashara hii kikamilifu sanjari na kuwasaidia wahanga na waathirika wa utumwa mamboleo. Baba Mtakatifu Francisko anasema, watu wote ni sawa kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; wana utu na heshima sawa, kumbe wanapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa utu wao kama binadamu na wala si vinginevyo! Ubaguzi wa aina yoyote ile ni kwenda kinyume cha utu na heshima ya binadamu! Biashara hii ni uhalifu dhidi ya ubinadamu kama ilivyo pia mifumo yote ya utumwa mamboleo kama vile: kazi za suluba, biashara ya ngono, biashara haramu ya viungo vya binadamu; yote hii ni mifumo dhidi ya utu na heshima ya binadamu!

Biashara haramu ya binadamu inawapoka watu utu na heshima yao anasema Askofu mkuu Bernadito Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa. Umaskini wa kutupwa, ukosefu wa maendeleo, ujinga, majanga asilia, rushwa na ufisadi; uchu wa fedha na mali; biashara ya haramu ya silaha na dawa za kulevya pamoja na vitendo vya utakatishaji fedha haramu ni kati ya mambo yanayochangia kuendelea kushamiri kwa biashara haramu ya binadamu.

Vita, kinzani na mipasuko ya kijamii ni kati ya mambo makubwa yanayoendelea kuchangia kukua na kukomaa kwa biashara haramu ya binadamu duniani. Kutokana na vita kuna mamilioni ya watu wanaojikuta wakilazimika kuyakimbia makazi yao kama wakimbizi na wahamiaji, makundi ambayo ni rahisi sana kutumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu. Vatican inaamini kwamba, diplomasia na majadiliano katika ukweli na uwazi ni msingi na suluhu bora zaidi katika mchakato wa kusitisha vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Vatican inapenda kulitia shime Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kujizatiti zaidi katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu, kwa kusitisha vita na kinzani za kijamii kwa njia ya majadiliano.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Idhaa ya Kiswahili. 








All the contents on this site are copyrighted ©.