2016-12-22 15:12:00

Papa Francisko awapongeza wafanyakazi wa Kituo cha TV. RAI


Baba Mtakatifu Francisko kwa njia ya simu, Alhamisi, tarehe 22 Desemba 2016 amewapongeza viongozi wakuu wa Kituo cha Televisheni cha Italia, “RAI” waandishi wa habari, watangazaji pamoja na mafundi mitambo kwa kusherehekea miaka 30 tangu kipindi kijulikanacho kama “Unomattina” kilipoanzishwa, kipindi kinachorushwa kila siku asubuhi. Hiki ni kipindi kinachopembua tema mbali mbali kadiri ya changamoto za nyakati!

Wafanyakazi wa “RAI” wametumia nafasi hii pia kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuadhimisha hivi karibuni, kumbu kumbu ya miaka 80 tangu alipozaliwa. Wafanyakazi hawa wametumia nafasi hii kutoa kwa muhtasari kabisa maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko. Amewashukuru na kuwapongeza kwa kazi yao nzuri na mwishoni, amewatakia heri na baraka ya Siku kuu ya Noeli kwa Mwaka 2016. Baba Mtakatifu amewakumbusha kwamba, Mwenyezi Mungu katika unyenyekevu wake ameamua kujitwalia hali ya udogo na katika unyenyekevu, akazaliwa katika hali ya unyonge na umaskini, dhidi ya mantiki ya dunia hii inayoabudu mali na fedha. Noeli iwe ni fursa ya kuangalia ukuu wa Mungu unaogeuza yale mambo yanayopewa kipaumbele na walimwengu! Amewatakia Noeli yenye furaha na baraka!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.