2016-12-22 14:57:00

Mshikamano wa upendo na Khalifa wa Mtakatifu Petro!


Kardinali Angelo Sodano, Dekano wa Makardinali kwa niaba ya viongozi waandamizi wa Sekretarieti kuu ya Vatican maarufu kama “Curia Romana” , Alhamisi, tarehe 22 Desemba 2016 ametumia fursa hii kumtakia heri na Baraka Baba Mtakatifu Francisko wakati huu wa maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli na Mwaka Mpya 2017. Kanisa linamshukuru na kumpongeza kwa kuchaguliwa kwake kuliongoza Kanisa la Kristo katika kipindi hiki maalum cha historia ya Kanisa la Kristo. Anamshukuru Baba Mtakatifu kwa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu iliyoacha chapa ya kudumu katika maisha na utume wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia!

Siku kuu ya Noeli inawakumbusha waamini ufunuo wa huruma ya Mungu kwa njia ya ujio wa Yesu Kristo Mkombozi wa Ulimwengu kati yao. Hiki ni kipindi pia cha kuonesha moyo wa upendo na mshikamano wa dhati na Khalifa wa Mtakatifu Petro, kwa kumshukuru Mungu kwa ujumbe wa upendo unaoendelea kutolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya familia ya Mungu duniani kote!

Wanapenda kumuunga mkono katika jitihada zake za kukuza na kudumisha mchakato wa majadiliano ya kidini ili kutafuta haki, amani na maridhiano kati ya watu huko Mashariki ya Kati, lakini kwa namna ya pekee kabisa nchini Siria. Wanapenda pia kumhakikishia Baba Mtakatifu kwamba, wataendelea kutekeleza dhamana na wajibu wao kama watumishi wema na waaminifu wa neema ya Mungu, kila mtu kwa kadiri ya karama ya Roho Mtakatifu, ili kumwezesha kutekeleza kikamilifu dhamana na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, Mchungaji mkuu na Msamaria mwema. Wote wanamtakia heri na baraka kwa Siku kuu ya Noeli!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.