2016-12-22 14:20:00

Mchakato wa mageuzi ya "Curia Romana" kiini cha salam za Noeli 2016


Salam na matashi mema ya Noeli na Mwaka Mpya 2017, mchakato wa mageuzi ya Sekretarieti kuu ya Vatican; maana ya mageuzi haya katika maisha na utume wa Kanisa; vigezo kumi na viwili vinavyozingatiwa katika mchakato huo, mafanikio yaliyokwishakupatikana hadi wakati huu na mambo yanayotarajiwa kwa siku za usoni, ndiyo mambo makuu yaliyopewa kipaumbele cha pekee na Baba Mtakatifu Francisko Siku ya Alhamisi tarehe 22 Desemba 2016 alipokutana na kuzungumza na viongozi wakuu wa Sekretarieti kuu ya Vatican, kama sehemu ya utamaduni wa kutakiana heri na baraka wakati wa Noeli na Mwaka Mpya!

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwatakia wasaidizi wake wote wanaotekeleza dhamana na utume wao ndani na nje ya Vatican heri, baraka, neema na matashi mema kwa Siku kuu ya Noeli na Mwaka Mpya 2017. Waamini katika Siku kuu ya Noeli wanatafakari Fumbo la Umwilisho linalodhihirisha  wema, upendo na huruma ya Mungu, aliyejishusha kutoka katika utukufu wake na kujinyenyekeza katika hali ya ubinadamu inayoonesha kwamba, fadhila ya unyenyekevu inapendwa sana na Mwenyezi Mungu.

Kumbe, Noeli ni kipindi cha kushuhudia imani kwa Mungu anayependa unyenyekevu  kiasi cha kumwezesha mwanadamu kushangazwa na utukufu wake unaojionesha kwa namna ya namna ya pekee katika umaskini na unyonge, ili watu wote wasione aibu ya kumkaribia na hivyo kuondoa umbali kati ya binadamu na Mwenyezi Mungu. Lengo ni kumsaidia mwanadamu kujiaminisha, kuwa karibu, kumsikiliza na hatimaye, kumpenda Mungu. Baba Mtakatifu anasema, huu ndio muhtasari wa Ukristo wote! Mwenyezi Mungu amependelea kuzaliwa katika hali ya ubinadamu ili aweze kupendwa, changamoto kubwa katika kipindi cha Noeli kinachokinzana na mantiki ya ukuu wa dunia, tabia ya kutoa amri au kwa ajili ya mafao binafsi.

Baba Mtakatifu anasema, salam na matashi yake ya Siku kuu ya Noeli kwa Mwaka 2016 yanafumbatwa na tema ya mageuzi ya Sekretarieti kuu ya Vatican, maarufu kama “Curia Romana”. Kwa kuzingatia mzizi neno wa mageuzi “Ri-forma” ni kuthibitisha Habari Njema ya Wokovu inayotangazwa kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, changamoto ni kujikita katika mambo msingi ya maisha ya binadamu kwa njia ya huduma inayotolewa na Mama Kanisa.

Mageuzi haya yanapania kuboresha huduma inayotolewa na Khalifa wa Mtakatifu Petro katika maisha na utume wake kama kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki. Mageuzi haya ni sehemu ya mchakato wa maboresho ya wema na huduma inayotolewa na Papa kwa ajili ya Kanisa la Ulimwengu kwa kutambua kwamba, Kanisa daima liko katika safari, daima liko hai na linapaswa kujikita katika mageuzi yanayofumbatwa katika toba na wongofu wa ndani; katika maisha ya kiroho; majiundo na utakaso endelevu, ili kuondokana na magonjwa ambayo yanachafua huduma ya Kanisa.

Kumbe, hapa kuna haja ya kujikita katika huruma inayofumbata kanuni msingi kwa wahudumu wa Kanisa la Kristo, changamoto ambayo kimsingi ni endelevu ili kuondokana na “magonjwa, matatizo na changamoto” zinayokwamisha hutoaji wa huduma makini kwa Kanisa la Kristo! Kuna kinzani ambazo zinaweza kuwa ni msingi bora wa majadiliano katika ukweli na uwazi! Lakini, kinzani zinazojikita katika woga, wasi wasi na kutokubali mageuzi ni sawa na Mbwa mwitu waliojivika ngozi ya Kondoo, kwani hawa ni wale ambao wanakimbilia kujificha katika Mapokeo, mwonekano wa nje bila kutenganisha: kitendo na mtendaji, kielelezo cha kifo. Hata hivyo, Baba Mtakatifu anakaza kusema, mambo yote haya yanapaswa kusikilizwa kwa makini, kupokelewa na kufanyiwa kazi.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, mageuzi ya “Curia Romana” ni mchakato tete unaopaswa kujikita katika uaminifu kwa mambo msingi; mang’amuzi endelevu kwa kuwa na ujasiri wa Kiinjili; hekima ya Kikanisa; kwa kusikiliza kwa makini; kwa kufanya maamuzi mazito yanayosindikizwa kwa sala, unyenyekevu, mwono mpana na hatua makini! Pale mambo yanapokwama, kuna uwezekano wa kurejea tena nyuma, kwa kuonesha mamlaka ya uwajibikaji, utii usioshuruti, lakini zaidi kwa kujiachilia na kujiaminisha chini ya  msaada na uongozi makini wa Roho Mtakatifu.

Baba Mtakatifu amegusia vigezo kumi na viwili vinavyotumika katika mchakato wa mageuzi kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican, maarufu kama “Curia Romana”. Vigezo hivi ni wongofu wa mtu binafsi; wongofu wa shughuli za kichungaji; wongofu wa kimissionari kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo Yesu ili kuwatangazia watu wa Mataifa Habari Njema ya Wokovu. Vigezo vingine ni pamoja na utaratibu utakaosaidia kuleta ufanisi na tija katika huduma inayotolewa na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Upyaisho unaojikita katika kusoma alama za nyakati, Kiasi na Kanuni Auni; Dhana ya Sinodi, Ukatoliki, Weledi na hatimaye, Mang’amuzi yanayofanywa hatua kwa hatua!

Baba Mtakatifu anasema, katika mchakato wote huu wa Mageuzi ya “Curia Romana” kumekuwepo na mafanikio makubwa: Kati ya mafanikio haya ni kuundwa kwa Baraza la Makardinali Washauri; Kuundwa kwa Tume ya Kipapa ya Rejea kwa ajili ya Benki kuu ya Vatican, maarufu kama IOR. Kumekuwepo na maboresho ya Sheria za Vatican mintarafu adhabu zinazotolewa. Kumeundwa mfumo mpya wa uchumi na uongozi kwa ajili ya kufanya maboresho katika taratibu za uongozi na huduma za kiuchumi zinazotolewa na Vatican.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Vatican imeunda Tume ya Usalama wa Fedha ili kupambana na tatizo la utakatishaji wa fedha haramu, ufadhili wa vitendo vya kigaidi na ununuzi wa silaha za mahangamizi sanjari na kuzingatia sheria za kimataifa, ukweli na uwazi. Kumeundwa pia Mamlaka ya Habari za Fedha ili kupambana na uvunjwaji wa sheria katika masuala fedha. Sektretarieti na Baraza la Uchumi yameundwa ili kuratibu shughuli zote za fedha na uchumi mjini Vatican. Kunako Mwaka 2014 kumeanzishwa Tume ya Kulinda Watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia na masuala yote ya urithi wa Kiti cha Kitume yalihamishiwa kwenye Sekretarieti ya Uchumi.

Mwaka 2015 kumeundwa Sekretetarieti ya Mawasiliano ili kukabiliana na changamoto za maendeleo ya sayansi na teknolojia katika mawasiliano, ili kuliwezesha Kanisa kutekeleza vyema dhamana na wajibu wake na Katiba yake ikapitishwa kunako mwaka 2016. Kumekuwepo na mabadiliko yanayoharakisha mchakato wa kutengua kesi za ndoa zenye utata kadiri ya Sheria za Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko anasema, ametoa ruhusa kwa Maaskofu mahalia kushughulikia kesi za nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo.

Kunako Mwaka 2016 kumeundwa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha pamoja na Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu na mwishowe, Katiba ya Taasisi ya Maisha ya Kipapa imepitishwa! Baba Mtakatifu Francisko anakumbusha kwamba, kiini cha mageuzi yote haya ni Kristo Yesu! Kumbe, Noeli ni Siku kuu ya Mungu anayependa unyenyekevu; ni kipindi cha Sala na tafakari ili kuendeleza mchakato wa kumwilisha fadhila ya unyenyekevu na wema, ili kuona Ufunuo wa Utoto wake Mtakatifu katika nyoyo zao. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika wasaidizi wake wa karibu kuondoa ndani mwao kiburi na majivuno kwa kushuhudia unyenyekevu badala ya kuendelea kupigana vikumbo kwa kutafuta ni nani zaidi! Ni nani mwenye nguvu kuliko wengine, matokeo yake ni majanga yasiyokuwa na kikomo duniani! Kwa kumwambata Kristo Yesu, dunia inaweza kupata amani na wokovu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.