2016-12-22 08:23:00

Maaskofu USA: Wekezeni katika utume wa vijana!


Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa kulizawadia Kanisa Waraka wa Kitume “Misericordia et misera” yaani, “Huruma na amani” kama sehemu ya mchakato wa mwendelezo wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu katika uhalisia wa maisha ya waamini! Ni changamoto ya kukimbilia huruma ya Mungu katika: Liturujia, Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa zinazomkirimia mwamini huruma na upendo wa Mungu katika maisha yake, tayari kuwa ni shuhuda na chombo cha huruma na upendo wa Mungu unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Huu ni mwaliko wa kuendelea kutoa kipaumbele cha pekee kwa huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kuwaonjesha matunda ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu anakazia kwa namna ya pekee, umuhimu wa waamini kukimbilia huruma ya Mungu katika Sakramenti za huruma ya Mungu ambazo kimsingi ni Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, hapo wanapata nguvu ya chakula cha mbinguni, tayari kujimega na kujisadaka kwa ajili ya huduma makini kwa jirani zao kwani wanakuwa ni Ekaristi inayomegwa na kugawanywa kwa wahitaji.

Waamini wakimbilie huruma ya Mungu katika Sakramenti ya Upatanisho, ili kukutana na Kristo hakimu mwenye huruma na mapendo, anayesamehe; anayeponya na kuganga majeraha ya maisha ya mwanadamu, tayari kumpatia nafasi ya kuanza tena upya katika mwanga wa neema ya utakaso inayobubujika kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo. Kimsingi, waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa watu wa nyakati hizi!

Kardinali Daniel N. DiNardo, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani aliyechaguliwa hivi karibuni, anampongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kulijalia Kanisa Waraka wa Kitume “Huruma na amani” mwaliko na changamoto ya kuwa kweli ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu, kielelezo makini cha Imani tendaji katika ulimwengu ambamo watu wengi wanahitaji kuona miujiza ya huruma na upendo wa Mungu. Waamini wawe na ujasiri wa kuwasaidia na kuwahudumia maskini, wagonjwa, wakimbizi na wahamiaji bila ya kuwasahau wale wote wanaohitaji msaada wao wa kiroho na kimwili.

Kardinali Daniel N. DiNardo anakaza kusema, katika hali na unyonge wa binadamu, watu wengi wanaweza kudhani kwamba, wamesahauliwa na Mungu pamoja na jamii inayowazunguka. Kumbe, watu wa namna hii wanahitaji kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Yesu mwenyewe katika maisha na utume wake wa hadhara aliwaonesha watu huruma na upendo wa Mungu kwa kuwaondolea magonjwa na shida mbali mbali zilizokuwa zinawaaandama; akawasamehe dhambi zao na kuwarudishia tena utu na heshima yao kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu! Hii ndiyo changamoto iliyoko mbele ya waamini baada ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Katika mkutano mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki uliohitimishwa hivi karibuni, Askofu mkuu Christophe Pierre, Balozi wa Vatican nchini Marekan ambaye ameanza utume wake hivi karibuni, aliwataka viongozi wa Kanisa nchini Marekani kuhakikisha kwamba, linawekeza zaidi katika utume na maisha ya vijana ili kuwajengea matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Viongozi wa Kanisa wawe ni mashuhuda wenye mvuto na mashiko kwa maisha ya kiroho miongoni mwa vijana, ili kuwaimarisha katika kanuni maadili, tunu msingi za maisha ya Kikristo na utu wema, tayari kuwajibika katika maisha yao kama waamini na raia wema.

Askofu mkuu Pierre anakaza kusema, vijana wengi wanajikuta wanakosa dira na mwelekeo sahihi katika maisha yao kutokana na kukosa nafasi ya kurithishwa kweli za Kiinjili na Imani. Kumbe, Kanisa halina budi kuhakikisha kwamba, linajiwekeza sera na mikakati ya kichungaji, ili kuwajengea vijana msingi bora katika maisha yao, ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda wa imani miongoni mwa vijana wa kizazi kipya. Vijana watambue kwamba, wao ni wadau muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa na kamwe si watazamaji na wala wasindikizaji kama wasemavyo waswahili, “kwenye msafara wa mamba, kenge hakosekani”!

Askofu mkuu Pierre anasema, huu ndio mwelekeo wa Kanisa kwa wakati huu kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa mwaka 2018 itakayoongozwa na tema juu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya miito”! Ikumbukwe kwamba, vijana ni nguzo na jeuri ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Lakini, jambo la kusikitisha ni kuwaona vijana wamechoka na kuelemewa na changamoto za maisha, kiasi hata cha kujisikia kuwa wako pembezoni mwa maisha na utume wa Kanisa. Umefika wakati wa kuwaendea vijana, ili kuwatia moyo!

Katika mkutano wa Baraza la Maaskofu Katoliki uliohitimishwa huko mjini Bartimore hivi karibuni, Maaskofu kwa kauli moja waliamua kuwa na kamati ya kudumu kwa ajili ya Kanisa Katoliki Barani Afrika. Itakumbukwa kwamba, kunako mwaka 2004, Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani lilianzisha Kamati ya muda kwa ajili ya Kanisa Katoliki Barani Afrika.

Sasa Kamati hii itakuwa ni ya kudumu kama kielelezo cha mshikamano na familia ya Mungu Barani Afrika. Kwa njia ya Kamati hii, Maaskofu wataweza kufadhili huduma za majiundo ya viongozi Barani Afrika; kuendeleza mchakato wa Uinjilishaji wa kina; Mawasiliano, haki na amani. Taarifa zinaonesha kwamba, Baraza al Maaskofu Katoliki Marekani limetoa kiasi cha Dolla za Kimarekani millioni 20 kwa ajili ya kugharimia miradi mbali mbali Barani Afrika. Huu ni mchango unaotolewa na waamini wa Majimbo 69 yanayounda Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.