2016-12-21 08:16:00

Papa Francisko: Endelezeni huruma na utume!


Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Jubilei ya huruma ya Mungu limekuwa ni tukio muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa, kwani waamini wengi wameweza kugundua na kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao, tayari kuimwilisha katika uhalisia wa maisha kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo cha imani tendaji!

Baba Mtakatifu Francisko kwa kutambua na kuthamini mchango mkubwa uliotolewa na Baraza la Kipapa la kuhamasisha Uinjilishaji mpya lililopewa dhamana ya kuandaa na kuratibu maadhimisho ya Mwaka wa huruma, Jumanne, tarehe 20 Desemba 2016 alitembelea Makao Makuu ya Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji mpya na kukutana na viongozi wake wakuu pamoja na wafanyakazi wa Baraza hili. Baba Mtakatifu amepata nafasi ya kuzungumza na wafanyakazi wa Baraza hili katika hali ya amani, utulivu wa ndani, utu na heshima kwa wote.

Amewashukuru na kuwapongeza kwa kazi kubwa walioifanya wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu anasema Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Rais wa Baraza hili. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwatakia heri na baraka wafanyakazi wote hawa katika maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli na Mwaka Mpya. Kwa hakika anasema Baba Mtakatifu ulikuwa ni Mwaka wa huruma na utume wa Kanisa kwa sasa ni kuendelea kumwilisha huruma ya Mungu katika maisha ya watu kama kielelezo cha imani tendaji.

Askofu mkuu Fisichella anakaza kusema, uwepo wa Baba Mtakatifu miongoni mwao, umeonesha udugu na upendo wa hali ya juu kwa kuguswa na kuthamini kazi kubwa iliyotekelezwa na wafanyakazi wa Baraza hili kwa ajili ya kufanikisha maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwashirikisha yale yaliyojiri moyoni mwake wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Amewataka kuendeleza dhamana na wajibu wa wamissionari wa huruma ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia kama kielelezo cha uwepo endelevu wa huruma ya Mungu kwa waja wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.