2016-12-21 13:42:00

Kuzaliwa kwa Kristo Yesu ni chemchemi ya matumaini na wokovu


Kuzaliwa kwa Yesu Kristo ni chemchemi ya matumaini, tema ambayo ni muhimu sana wakati wa Kipindi cha Majilio na waamini wanaongozwa kwa namna ya pekee na Nabii Isaya. Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, matumaini yameingia ulimwenguni kama Nabii Isaya anavyosema, tazama Bikira atachukua mimba na kumzaa mtoto atakayeitwa Immanueli. Mwenyezi Mungu ametekeleza ahadi yake kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu alipotwaa mwili na kukaa kati ya watu, ili kuwaonesha mshikamano na wala hakuona kuwa sawa na Mungu ni kitu cha kung’angania sana, kielelezo makini cha uaminifu unaofungua Ufalme wa mbinguni na kuwakirimia wanadamu matumaini mapya: yaani maisha ya uzima wa milele!

Hii ni sehemu ya Katekesi iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano, tarehe 21 Desemba 2016, kama sehemu ya mwendelezo wa Katekesi kuhusu matumaini ya Kikristo, wakati huu wa Kipindi cha Majilio, kwani matumaini yanavuka hata matarajio ya kibinadamu. Kwa njia ya Siku kuu ya Noeli, yaani kuzaliwa kwa Kristo Yesu kunafungua njia ya ukombozi unaojikita katika matumaini thabiti, yanayoonekana na kushikika kwani Mwenyezi Mungu ndiye msingi!

Yesu Kristo kwa kuingia ulimwenguni anawakirimia waja wake nguvu ya kutembelea kumwelekea Mungu katika utimilifu wa maisha, ili hatimaye, kuishi pamoja naye milele yote. Matumaini ya Kikristo maana yake ni kuwa na uhakika wa safari pamoja na Kristo kuelekea kwa Baba wa mbinguni anayewasubiri kwa mikono miwili. Haya ndiyo matumaini yanayoletwa na Mtoto Yesu, kwa kuwaonesha watu dira na mwongozo wa maisha ya sasa, wokovu wa binadamu na heri kwa wale wanaojiaminisha kwa huruma ya Mungu. Mtakatifu Paulo anafupisha yote haya kwa kusema kwa maana tumeokolewa kwa taraja.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwa kusema kwamba, katika nyumba za Kikristo, waamini wanatayarisha Pango la Mtoto Yesu, mapokeo ambayo yalianzishwa na Mtakatifu Francisko wa Assisi, alama ya matumaini yanayoshuhudiwa na wahusika wakuu wanaowekwa kwenye Pango la Mtoto ya Yesu aliyezaliwa mjini Bethlehemu, mjini mwa Daudi, mchungaji aliyechaguliwa na kupakwa mafuta na Mungu. Bethelehemu ni mji ambao uko pembezoni mwa Israeli, mahali ambako Mungu anapendezwa kutenda kazi yake kati ya watu wadogo na wanyenyekevu. Hapa anazaliwa “Mwana wa Daudi” aliyesubiriwa na wengi, Yesu Kristo, hapa matumaini ya Mungu na binadamu yanakutana na kubusiana!

Baba Mtakatifu anasema, Bikira Maria ni Mama wa matumaini, kwa kukubali kwake amemfungulia Mungu mlango wa ulimwengu; Moyo wake mtakatifu ulikuwa umesheheni matumaini na kupambwa kwa imani, akateuliwa na hatimaye, kujiaminisha kwa Neno la Mungu. Kwa muda wa miezi tisa akawa ni “Tabernakulo” ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili; Sanduku la Agano la milele! Pangoni mwa kulishia wanyama akatafakari upendo wa Mungu unaomwokoa mwanadamu. Pembeni mwa Bikira Maria, alikuwepo Mtakatifu Yosefu, kutoka katika shina la Yese na Daudi ambaye pia aliliamini Neno la Malaika, akamwangalia Yesu katika holi ya kulishia wanyama, akamtafakari Mtoto aliyezaliwa kwa njia ya Roho Mtakatifu ambaye alitakiwa kumpatia jina la Yesu, chemchemi ya  matumaini kwa kila binadamu kwani kwa njia yake, Mwenyezi Mungu atawaokoa binadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Pangoni Bethelehemu walikuwepo pia wachungaji kutoka kondeni, wanao wawakilisha watu wanyonge na maskini! Hawa ni wale waliomtumainia Mwokozi, faraja ya Israeli na ukombozi katika Yerusalemu. Kwa njia ya Mtoto Yesu, wakaona utimilifu wa ahadi ya Mungu na kwamba, walitumaini kuona kuwa wokovu unawafikia hata wao pia. Kwa mtu anayejiaminisha katika usalama na utajiri wa mali za dunia hii, hawezi kamwe kutarajia wokovu wa Mungu. Ni watu wadogo na maskini wanaotumaini na kujiaminisha mbele ya Mungu sanjari na kufurahia uwepo wa Mtoto Yesu waliyeambiwa habari zake na Malaika! Baba Mtakatifu anakaza kusema, Malaika na wingi wa jeshi la mbinguni walikuwa wanatangaza mpango wa Mungu utakaotekelezwa na Mtoto Yesu: Yaani “Utukufu kwa Mungu juu mbinguni na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia”. Hii inatokana na ukweli kwamba, matumaini ya Kikristo yanashuhudiwa kwa njia ya masifu na shukrani kwa Mwenyezi Mungu aliyefungua Ufalme wake unaofumbatwa katika upendo, haki na amani.

Baba Mtakatifu anasema, kwa kutafakari Pango la Noeli, waamini wapate nafasi ya kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya kuadhimisha Siku kuu ya Noeli, yaani kuzaliwa kwa Kristo Yesu, mbegu ya matumaini inayopandikizwa na Mwenyezi Mungu katika historia ya maisha ya mwamini mmoja mmoja na jumuiya katika ujumla wake. Kila wakati waamini wanapomkubali na kumpokea Yesu, hiyo inakuwa ni mbegu ya matumaini. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewatakia wote Noeli ya matumaini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.