Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, neno Huruma ya Mungu limesika mara nyingi sana masikioni mwako, na bado linaendelea kukujia, ila leo linakujia katika ujumbe mzito uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko , ambapo analeta kwetu mwito wa kusherekea huruma ya Mungu. Hapa anasema awali ya yote tunaitwa kusherekea huruma ya Mungu, na kwa hilo tutapata utajiri wa neema zitokanazo na huruma hii ya Mungu. Katika waraka wake wa kitume “Misericordia et misera” yaani Huruma na amani, Baba Mtakatifu anasema, Huruma ya Mungu hujitokeza kiundani kabisa hasa katika adhimisho la Liturujia, anatuambia toka mwanzo wa adhimisho la Ekaristi Takatifu, Huruma ya Mungu hujitokeza kwa wingi hasa katika mwitikio na ushiriki wa sala za waamini na Mungu mwenyewe.
Ujumbe huu, Huruma na amani ya kimungu, ni ule mwitikio utokao kwa Mungu na Mwanaye Yesu Kristo. Ambapo amani hii ni utulivu wa ndani wa moyo na roho ambao umwadhimisha Kristo ndani yake bila kujali mazingiza au watu. Baba Mtakatifu anatuambia, amani hii tunaweza kuipata zaidi katika adhimisho la Liturujia takatifu , pamoja na Sakramenti nyingine za kanisa ikiwemo Sakramenti ya upatanisho, kwani Huruma na amani ni matokeo ya muunganiko wa kiundani baina ya mwamini na Mungu Mwenyezi kupitia sadaka ya Yesu Kristo Msalabani. Mtakatifu Paulo anatuambia, amani iletayo furaha ya ndani, yapatikana tu kwa wale wanao mwamini Kristo (Warumi 15:13), mwamini yeyote anayeguswa na huruma na amani ya Mungu atapata kutambua mamlaka ya Kimungu na hivyo, kumrudishia Mungu sifa na shukrani, kwani Mungu ndiye atujaliae, huruma na amani ya kweli.
Adhimisho la huruma ya Mungu hupata utulivu wake katika Ibada takatifu , ambapo Fumbo la Pasaka uadhimishwa , na chanzo cha wokovu wa mwanadamu huonekana katika historia na zaidi katika ulimwengu mzima. Baba Mtakatifu anatuambia, Kila neno katika adhimisho la Fumbo la Ekaristi takatifu lina umaana wa huruma ya Mungu, huruma iletayo amani na furaha moyoni. Na hii ndiyo ile amani tuipatayo kupitia sadaka ya Yesu Msalabani , ikituunganisha katika Amani ya Mungu Baba, na amani hii itokayo kwa Mungu isingwezekana bila huruma ya Mungu. Katika hilo twashuhudia ukuu wa Huruma ya Mungu katika maisha ya mwanadamu. Hivyo, mwanadamu aliyeumbwa katika hali ya upendo na amani ya kimungu, analo jukumu la kuishi hii amani ya kimungu na pia kuieneza kwa wengine kama ushuhuda wa imani tendaji!
Baba Mtakatifu Francisko anatualika kuwa na muunganiko wa ndani na Mungu na huko ndiko kujipatia amani nafsini mwetu. Na amani hii itapatikana hasa katika maisha ya Sala na maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa. Katika hilo, adhimisho la Ekaristi takatifu lamjia mwanadamu kwa hadhi ya juu kabisa katika kumpatia mwanadamu amani na furaha moyoni. kwani ni katika tendo hili, tunakutana na kuunganika na sadaka ya Yesu msalabani, ambaye kwa kifo na ufufuko wake tumepatanishwa na Mungu na hivyo kuinuliwa na kupewa hadhi ya kuitwa wana wa Mungu. Ninakutakia, heri na baraka, jitahidi kuwa kweli ni chambo cha amani na furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake!
Kutoka studio za Radio Vatican ni mimi, Padre, Agapiti Amani, ALCP/OSS.
All the contents on this site are copyrighted ©. |