2016-12-20 08:28:00

Tangazeni ni kushuhudia huruma ya Mungu kwa watu wa mataifa!


Wafanyakazi katika Sekretarieti ya Mawasiliano mjini Vatican wametakiwa kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu ili aweze kuwashangaza, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayofumbatwa katika huruma na upendo wa Mungu hadi miisho ya dunia. Hii ni changamoto iliyotolewa na Monsinyo Dario Edoardo Viganò, Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Mawasiliano mjini Vatican Jumatatu, tarehe 19 Desemba 2016 wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, ili kutakiana heri na baraka kwa Siku kuu ya Noeli kwa Mwaka 2016.

Katika mahubiri yake, Monsinyo Viganò amefanya rejea kwa wahusika wakuu katika Liturujia ya Neno la Mungu, watu ambao walikumbana na changamoto mbali mbali za maisha, lakini bado waliendelea kuwa na matumaini kwa Mwenyezi Mungu na hatimaye wakagundua kwamba, hakuna jambo lisilowezekana mbele ya Mwenyezi Mungu. Mapadre ishirini wameshiriki katika Ibada hii ya Misa Takatifu iliyohudhuriwa pia na viongozi wakuu wa vyombo vya mawasiliano vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican.

Wafanyakazi wa Sekretarieti ya mawasiliano wametakiwa kutangaza na kushuhudia Fumbo la Mungu anayeingia katika historia na maisha ya watu na hivyo kuwaletea mabadiliko makubwa. Changamoto kubwa iliyoko mbele yao ni kuhakikisha kwamba, wanatangaza huruma ya Mungu katika maisha ya waja wake kama ilivyojionesha kwa watu kama Manoa na mke wake ambaye alikuwa tasa, lakini kwa neema ya Mungu akabahatika kupata Mtoto alitwaye Samsoni, Mnadhiri wa Mungu na maana ya jina hili “Manoa” ni “mahali pa kupumzikia”.

Hapa, waamini wanaalikwa kumsikiliza Mwenyezi Mungu anayewatembelea katika historia na maisha yao kwa kutambua kwamba, sala ni ufunguo unaofungua moyo wa Mungu kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko. Mwenyezi Mungu anaendelea kumshangaza mwanadamu kwani anatenda nje kabisa ya mipango, taratibu na nyakati. Mwenyezi Mungu anamfunulia binadamu uwepo wake na siri ya mpango katika maisha yake na kwamba, binadamu anapaswa kukubali na kutekeleza mpango wa Mungu katika maisha yake.

Monsinyo Viganò  anawahimiza wafanyakazi wa Sektretarieti ya Mawasiliano kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikiliza kwa makini, ili kufahamu mapenzi ya Mungu na kuyajibu kwa ufanisi mkubwa. Hii ni sehemu ya kanuni msingi ya mawasiliano ya kijamii, yaani kusikiliza kwa makini, kufahamu na kutekeleza bila wasi wasi wowote. Kwa njia hii wataweza kuwa ni zawadi kwa wengine na hivyo kuonja uzuri wa mtindo wa kufanya kazi kama familia ili kuvuka kinzani, hali ya kutoelewana na kukata tamaa; matatizo na changamoto za kazi, daima wakijitahidi kuwa waaminifu kwa Mwenyezi Mungu mwaliko ambao uko mbele yao daima.

Monsinyo Viganò amemzungumzia Mzee Zakaria na maana ya jina hili ni “Mungu amekumbuka” pamoja na mke wake Elizabeth, maana yake “Mwenyezi Mungu ameapa” au kwa maneno mengine “Mungu ni mwaminifu”. Hawa ni wachamungu waliokita maisha yao katika sala na sadaka; wakajiaminisha mbele ya Mungu licha ya maneno na shutuma zilizokuwa zinatolewa dhidi yao kutokana na ugumba. Wengine walithubutu kusema kwamba, ugumba huu ulikuwa ni adhabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Zote hizi ni shutuma zilizoufedhehesha moyo wa Elizabeth!

Lakini, Mwenyezi Mungu ambaye ni mwaminifu katika ahadi zake, akaingia katika historia ya maisha ya Elizabeth na hivyo kumkirimia Mtoto aliyepewa jina Yohane, maana yake “Mungu ana huruma”. Elizabeth anapewa ujumbe wa huruma ya Mungu katika maisha yake na kwamba, Mungu anaendelea kuwa ni mwenye huruma na mapendo kwa waja wake daima na milele.

Monsinyo Dario Edoardo Viganò, amehitimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa kuwakumbusha wafanyakazi hawa kwamba, wao ni “Jumuiya ya Kimataifa” yenye utajiri mkubwa wa lugha, tamaduni na mapokeo ya watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Watambue kwamba, hakuna mgeni wala mtu wa kuja ndani ya Kanisa, wote ni watoto wapendwa wa Mungu, wanaotumwa kupeleka ujumbe wa Noeli sehemu mbali mbali za dunia.

Amewapongeza Wayesuit na Wasalesiani, mashirika makubwa ya kitawa yanayotoa sehemu kubwa ya huduma mjini Vatican. Wamemkumbuka na kumwombea Baba Mtakatifu Francisko heri na baraka kwa kuadhimisha kumbu kumbu ya miaka 80 tangu alipozaliwa. Noeli inawakumbusha waamini kwamba, Mwenyezi Mungu mi mwema, mwenye uwezo na nguvu anayetaka kuwaokoa watu wote na wala hataki mtu awaye yote apotee ndiyo maana amefanyika mwili na kuja kukaa kati ya watu wake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.