2016-12-20 12:07:00

Dini katika mchakato wa ujenzi wa amani duniani!


Imani ya Kikristo inawachangamotisha waamini kuongozwa na tunu msingi za maisha ya Kikristo zinazofumbatwa katika upendo, utu na heshima ya binadamu na kwamba, dini zina mchango mkubwa katika kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu! Hii ni sehemu ya tamko lililotolewa na washiriki wa kongamano la kimataifa kuhusu “dini na ujenzi wa amani” huko Kadoma, nchini Zimbabwe. Kongamano hili liliandaliwa na Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani kwa kushirikiana na Baraza la Makanisa nchini Zimbabwe.

Washiriki wa kongamano hili la kiekumene walitoka katika Makanisa ya Afrika na Ulaya, kwa pamoja wakashikamana ili kujadili na kupembua kwa kina na mapana mchango wa dini katika kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na maridhiano kati ya watu, kama changamoto ya kukabiliana na vita, kinzani na mipasuko ya kijamii inayoongezeka kila kukicha! Wakristo wanatambua kwamba, wanayo dhamana kubwa mbele yao ya kuhakikisha kwamba, wanakuwa ni mashuhuda na vyombo vya amani duniani, dhamana inayowafungamanisha na Injili ya Kristo, kiini cha Habari Njema ya Wokovu!

Wajumbe wanakaza kusema, mchakato wa ujenzi wa haki na amani hauna budi kuwa ni sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kiekumene, ili kuwawezesha Wakristo kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na upatanisho. Makanisa hayana budi kuonesha msimamo wake kwa kulaani vita, kinzani na mipasuko ya kijamii inayoendelea kudhalilisha utu na heshima ya binadamu. Lakini, ikumbukwe kwamba, waathirika wakuu ni maskini, watoto na wanawake wasioweza kujitetea hata kidogo. Majadiliano ya kiekuemene katika ujenzi wa amani yalenge kwa namna ya pekee kuwajengea wanawake na vijana uwezo wa kusimamia na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu! Kutokana na sababu msingi za kihistoria, kiuchumi, kijamii na kisiasa, wanawake kutokana na mfumo dume, walijikuta wakitengwa katika mchakato wa kupanga na kutekeleza maamuzi mbali mbali katika maisha ya kijamii pengine haya na kifamilia.

Kumbe, wadau mbali mbali wanapaswa kushirikishwa katika mchakato wa majadiliano yanayopania kujenga na kudumisha amani duniani, lakini kwa namna ya pekee kabisa Barani Afrika anasema, Askofu Ambrose Moyo kutoka katika Kanisa la Kiinjili la Kiluteri, ambaye kwa miaka mingi amekuwa mstari wa mbele katika kukuza majadiliano ya kiekumene Barani Afrika. Wajumbe wamepata nafasi ya kushirikisha uelewa na mang’amuzi yao kuhusu mchakato wa ujenzi wa amani duniani. Zimbabwe katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni imekuwa mstari wa mbele katika kukuza na kudumisha majadiliano ya kiekuemene katika huduma, sala na maisha ya kiroho.

Makanisa yanaendelea kusimama kidete ili kulinda na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; upatanisho na mafungamano ya kijamii hasa kutokana na changamoto za kisiasa, kiuchumi na kijamii zinazoendelea kuikumba Zimbabwe katika ujumla wake. Haya ni mambo msingi katika ujenzi wa amani duniani. Wajumbe pia wamepata nafasi ya kusikiliza shuhuda zilizotolewa na wajumbe kutoka Bosnia-Erzegovina katika kukuza majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika huduma makini. Lengo ni kuondokana na athari za vita baridi vinavyoendelea kuwatumbukiza watu wengi katika utumwa na ukoloni mamboleo.

Wajumbe wa mkutano huu wa kiekumene kuhusu amani wameshutumu na kulaani vitendo vyote vya uvunjifu wa misingi ya haki na amani, Vitendo vya kigaidi pamoja na mambo yote yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu. Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani limeanzisha mradi wa Uekumene wa huduma kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta ulinzi na usalama wa maisha yao nchini Cameroon. Hawa ni watu wanaokimbia vita, mashambulizi ya kigaidi na nyanyaso za kidini na kijinsia. Mkutano huu wa Kadoma, imekuwa ni nafasi  nyingine tena ya kuendelea kuadhimisha Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri duniani kwa kuwa na mwelekeo mpya zaidi. Huu ni wakati wa kushirikiana ili kujenga na kudumisha Uekumene wa damu, maisha ya kiroho, sala na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Wakristo wanahamasishwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya amani inayomwilishwa katika maisha yao ya kawaida!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.