2016-12-19 10:50:00

Mafuriko ya salam na matashi mema kwa Papa Francisko!


Baba Mtakatifu Francisko katika kumbukumbu ya maadhimisho ya Miaka 80 tangu alipozaliwa, Jumamosi tarehe 17 Desemba 2016 amepokea bahari ya salam na matashi mema kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Ni salam kutoka kwa maskini wa kawaida wanaosema, kweli ni Baba anayewasikiliza na kuwajali. Amepokea salam na matashi mema kutoka kwa waamini na watu wenye mapenzi mema, wakimtakia furaha, amani na afya njema ili kweli aweze kuendelea kuwaimarisha ndugu zake katika imani, matumaini na upendo kadiri ya mwanga wa Injili. Aweze kupata uzee wenye amani na utulivu, daima akijitahidi kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha na utume wake.

Viongozi wakuu wa Makanisa ya Kikristo nao wamejitokeza kumpongeza na kumtakia Baba Mtakatifu Francisko ujumbe wa matashi mema. Patriaki Cyrill wa Moscow na Russia nzima katika salam zake anamwelezea Baba Mtakatifu Francisko kuwa ni kiongozi ambaye katika maisha yake yote amejisadaka na kujitosa kimasomaso kwa ajili ya huduma kwa Mungu, Kristo na Kanisa lake. Kuchaguliwa kwake kuliongoza Kanisa Katoliki ni mwendelezo wa huruma na upendo wa Mungu katika maisha ya Baba Mtakatifu Francisko anayeendelea kujipambanua kuwa ni chombo na shuhuda wa upendo, amani, huduma kwa maskini na mchakato wa umoja wa Wakristo unaofumbatwa katika: sala, damu, huduma na ushuhuda wa Habari Njema ya Wokovu.

Patriaki Cyrill anaendelea kumshukuru Mungu kwa kumwezesha kukutana, kuzungumza na kusali pamoja na Baba Mtakatifu Francisko nchini Cuba mwezi Februari 2016. Tukio hili la kiekumene limeendelea kuimarisha majadiliano ya kiekumene kati ya Kanisa la Kiorthodox la Russia na Kanisa Katoliki. Kwa sasa Makanisa haya kwa pamoja yanaendelea kujizatiti kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, haki na amani sanjari na kukuza tunu msingi za maisha ya Kikristo, kanuni maadili na utu wema ili hatimaye, Wakristo kwa pamoja waweze kuwa ni watangazaji na mashuhuda wa Habari Njema ya Wokovu, kwa kuvuka mipaka ya kinzani na kutoelewana iliyojitokeza katika historia, maisha na utume wa Kanisa.

Kwa upande wake, Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli pamoja na salam na matashi mema kwa Baba Mtakatifu Francisko, lakini pia amemzawadia Msalaba uliotengenezwa kunako karne ya XVIII na Wamonaki waliokuwa wanaishi kwenye mlima Athos. Ni Msalaba ambao umechorwa ndani mwake historia nzima ya maisha ya Kristo Yesu. Zawadi hii imewakilishwa kwa Baba Mtakatifu Francisko na Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo baada ya kurejea kutoka katika maadhimisho ya Siku kuu ya Mtakatifu Andrea Mtume, iliyoadhimishwa hapo tarehe 30 Novemba 2016 huko Istanbul, nchini Uturuki.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Justin Welby, wa Jimbo kuu la Cantebury na kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani, amemtumia salam na matashi mema Baba Mtakatifu Francisko kupitia kwenye mitandao ya kijamii, akimhakikishia sala zake mbele ya Mwenyezi Mungu, ili aendelee kumbariki na kumtegemeza katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.