2016-12-19 10:20:00

DRC: Dumisheni majadiliano katika amani na mafao ya wengi!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 18 Desemba 2016 aliwashukuru mahujaji na waamini waliofurika kwa wingi katika tafakari ya Sala ya Malaika wa Bwana. Kwa namna ya pekee, amewaomba kushiriki naye katika sala ili majadiliano ya kisiasa yanayoendelea nchini DRC yaweze kufanyika katika hali ya amani na utulivu ili kuepuka vita, kinzani na mipasuko ya kijamii kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi.

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwashukuru watu wote pamoja na taasisi mbali mbali zilizomtumia salam na matashi mema wakati alipokuwa anasherehekea Miaka 80 tangu alipozaliwa, Jumamosi, tarehe 17 Desemba 2016. Amewakumbusha wote kwamba, Jumapili ijayo, yaani tarehe 25 Desemba 2016 ni Siku kuu ya Noeli. Anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kutumia kipindi hiki kilichosalia katika hali ya ukimya na tafakari juu ya safari ya Bikira Maria kuelekea Bethlehemu: Mateso, mahangaiko, uchungu na furaha aliyokuwa nayo Bikira Maria; changamoto na wasi wasi wa kupata mahali salama ni mambo yanayopaswa kuwafikirisha waamini wanapoangalia Pango la Mtoto Yesu.

Baba Mtakatifu kwa namna ya pekee, anawaalika waamini kuzama katika Fumbo la Umwilisho kwa kuzaliwa kwa Yesu, Mungu pamoja nasi ili kupokea neema na baraka ya Noeli; neema inayofumbatwa katika uwepo wa karibu wa Mungu kati pamoja na watu wake; uwepo wa upendo, unyenyekevu na wema.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.