2016-12-17 09:39:00

Uhuru wa kuabudu ni mhimili mkuu wa haki msingi za binadamu!


Uhuru wa kidini ni mhimili mkuu wa haki msingi za binadamu unaopaswa kusimamiwa kidete na wanachama wa Shirikisho la Ushirikiano wa Kimataifa, Usalama na Maendeleo Barani Ulaya, OSCE. Hii ni changamoto ambayo imetolewa hivi karibuni  huko Vienna, Austria na Monsinyo Antoine Camilleri, Katibu mkuu msaidizi wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican wakati wa ufunguzi wa mkutano kuhusu mapambano dhidi ya hali ya kutovulimiana na ubaguzi dhidi ya Wakristo!

Vatican itaendelea kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha uhuru wa kidini sanjari na kuenzi utu na heshima ya binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Uhuru wa kidini unafumbata na kudumisha haki msingi za binadamu, changamoto inayopaswa kufanyiwa kazi na wadau mbali mbali duniani. Hii inatokana na ukweli kwamba, dhamiri ya mtu ni mahali patakatifu ambamo Mwenyezi Mungu anazungumza na waja wake. Kumbe, mapambano dhidi ya ukatili, ubaguzi na kutowavumilia Wakristo ni njia muafaka kwa nchi wanachama wa OSCE kujizatiti zaidi katika kukuza na kudumisha haki msingi za binadamu kama alivyowahi kusema, Mtakatifu Yohane Paulo II.

Monsinyo Camilleri katika hotuba yake ya ufunguzi alijikita zaidi katika masuala ya kutovumiliana pamoja na uhuru wa kidini au uhuru wa kuabudu. Amepembua kwa kina na mapana mfumo wa ubaguzi na hali ya kutovumiliana kama ilivyo kwa nyakati hizi dhidi ya Wakristo sehemu mbali mbali za dunia. Anasema, kuna umuhimu wa kujizatiti kutafuta na kudumisha mafao ya wengi kwa njia ya dini au imani ya wadau mbali mbali, kwani hali ya kutovumiliana na ubaguzi ni vielelezo makini vya uvunjifu wa haki msingi za binadamu; mambo yanayogumisha pia mafungamano ya kijamii, haki na amani.

Ikiwa kweli OSCE inataka kukuza na kudumisha usalama na ushirikiano wa kimataifa kuna haja ya kusimama kidete kupambana na mifumo yote inayosababisha ubaguzi na hali ya kutovumiliana kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Baadhi ya mifumo hii ni ukandamizaji, dhuluma na mateso wanayofanyiwa Wakristo sehemu mbali mbali za dunia, lakini kwa namna ya pekee huko Iraq na Siria na kama vitendo vya kigaidi vilivyotokeza huko Misri na kusababisha uharibifu mkubwa  kwa Jumuiya ya Wakristo wa Kanisa la Kikoptik.

Wakristo na nyumba zao za Ibada wamekuwa wakishambuliwa sana kutokana pia na tabia ya maamuzi mbele. Ukanimungu na tabia ya kutaka kumwondoa Mwenyezi Mungu katika maisha ya hadhara duniani ni hatari sana katika kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya kiutu, kimaadili na kijamii. Leo hii, kuna baadhi ya viongozi wa kisiasa wanataka hata kufuta siku kuu kama Noeli kwa kisingizio kwamba, inaweza kuwa ni kikwazo kwa waamini wa dini nyingine. Wakristo wanalazimishwa kutenda mambo kinyume cha dhamiri nyofu, hali inayotishia uhuru wa dhamiri. Kumbe, hapa kuna haja ya kukuza na kudumisha mchakato wa majadiliano ya kidini katika medani mbali mbali za maisha ya kijamii, kisiasa, kiuchumi na kidiplomasia.

Tabia ya kuwapinga, kuwadhulumu na kuwanyanyasa Wakristo ni hali inayojitokeza hata katika nchi wanachama wa OSCE inayoundwa na Nchi 57. Kumekuwepo na vitendo vya kuharibu nyumba za ibada, kufuru kwa maeneo matakatifu pamoja na mauaji ya viongozi wa kidini. Hata Wakristo wanayo haki ya kutangaza na kushuhudia imani yao katika maisha ya hadhara pasi na kificho kwani hii ni haki yao msingi. Kuna sera na mikakati ya kisiasa inayopania kulikandamiza Kanisa, kwani imani na kanuni maadili zimekuwa ni tishio kubwa kwa uhuru usiokuwa na mipaka, mvuto wala mashiko kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, uhuru wa kidini unatoa fursa kwa waamini kuweza kumwabudu Mwenyezi Mungu kama mtu binafsi au jumuiya ya waamini; kwa kufuata dhamiri nyofu. Ni uhuru unaomwilishwa katika maisha ya mtu binafsi, familia na hata katika jamii, kwani dini ni sehemu muhimu sana ya maisha na utamaduni wa watu. Kumbe, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwashughulikia kisheria wale wote wanaovunja na kuhatarisha uhuru wa kuabudu.

Monsinyo Antoine Camilleri anakumbusha kwamba, Nchi wanachama wa OSCE zimetoa uhuru wa kuabudu kwa wanachama wake, lakini tamko hili linaonekana kana kwamba, halina makali wala uzito mkubwa. Kumbe, hapa kuna haja ya kujizatiti kulinda, kutetea na kudumisha uhuru wa kuabudu kama mhimili wa haki msingi za binadamu na kwa ajili ya mafao ya mtu binafsi na jamii katika ujumla wake. Uhuru wa kuabudu ni chachu muhimu sana katika kukuza na kudumisha haki msingi za binadamu, demokrasia, utawala wa sheria pamoja na kusaidia mchakato wa kutafuta na kudumisha ukweli, haki, amani na maridhiano kati ya watu! Mkazo zaidi unapaswa kuwekwa kwenye majadiliano ya kidini kama nyenzo ya kukuza na kudumisha usalama, hali ya kuaminiana na kuheshimiana; upatanisho, maridhiano na utulivu kama msingi thabiti wa amani duniani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.