2016-12-16 11:32:00

Wananchi wa Siria kwa miaka 5 hawajawahi kusherehekea Noeli!


Kardinali Luis Antonio Tagle, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis katika ujumbe wake wa Noeli kwa Mwaka 2016 anasema, kwa miaka mitano sasa wananchi wa Siria hawajawahi kuadhimisha Sherehe ya Noeli na wanaendelea kuteseka kutokana na vita, utupu na baridi. Watoto wanaendelea kuteseka kwa magonjwa na hali ngumu ya maisha kutokana na baridi kali, vita, kinzani na mipasuko ya kijamii kiasi kwamba wanashindwa hata kwenda shule, jambo ambalo ni haki msingi katika maisha yao!

Wanawanchi wengi wa Siria wanalazimika kutembea mwendo mrefu ili kutafuta hifadhi na usalama wa maisha yao, kiasi kwamba, hata kile kidogo walichobeba, kinawawia vigumu kuendelea kuwa nacho na hivyo hata mambo msingi ya maisha yanaachwa pembeni mwa barabara ili kusalimisha maisha. Watoto, wanawake na wazee wanalazimika kuishi katika vyumba vilivyosheheni watu, bila kugusia wale wanaolazimika kuishi kwenye mahema au barabarani kwa kukosa eneo la kuwahifadhi, kwani wamegeuka kuwa ni wakimbizi na hata pengine watu wasiokuwa na makazi katika nchi yao wenyewe!

Caritas Internationalis inasema, kiasi cha fedha kilichokusanywa kutoka kwa wafadhili na wasamaria wema sehemu mbali mbali za dunia, kimetumika kwa ajili ya kununulia mavazi kwa watoto 500 wanaoishi Damasko na kwamba, wanaendelea kutoa huduma ya afaya, elimu, malazi na ushauri nasaha kwa watu hawa ambao wamejaribiwa, wameguswa na kutikiswa sana katika maisha na utu wao kama binadamu!

Wananchi wa Siria wanaridhika na kujawa na furaha hata kwa kiasi kidogo cha msaada wanaoupata. Kimsingi watoto wanahitaji msaada wa hali na mali ili kuwawezesha kwenda shule, ili kuweza kuwa na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Juhudi hizi za huduma kwa wahanga wa vita na kinzani za kijamii zinawezeshwa na wasamaria wema kutoka Caritas Internationalis wanaotembea na kuishi na wananchi wa Siria katika mazingira magumu na hatarishi.

Hii ni changamoto kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko ya kuonesha mshikamano wa huruma na upendo ili kuwasaidia wananchi hawa kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia kwamba, kila mmoja wao, amehifadhiwa katika sakafu ya moyo na utume wa Kanisa. Vita, kinzani na mipasuko ya kijamii nchini Siria imekuwa ni kielelezo cha hali ngumu ya maisha kwa wananchi wa Siria.

Caritas Internationalis sehemu mbali mbali za dunia, imeendelea kujielekeza katika mchakato wa kutafuta amani nchini Siria na kwamba, Baba Mtakatifu Francisko amekuwa mstari wa mbele katika kuenzi na kuwatia moyo wale wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya amani ya kudumu nchini Siria kwani katika kampeni ya Caritas anasema, amani inawezekana nchini Siria. Waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa kuendelea kusali kwa ajili ya toba na wongofu wa viongozi wenye dhamana katika Ukanda huu, ili waweze kujizatiti zaidi katika kutafuta na kudumisha amani ya kweli nchini Siria, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Kanisa linaombea amani ncini Syria anasema Kardinali Luis Antonio Tagle katika salam na matashi mema ya Noeli kwa ajili ya familia ya Mungu nchini Siria.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.