2016-12-16 08:46:00

Noeli inakaribia, jiandaeni vyema kumpokea Immanueli!


Tafakari ya Neno la Mungu katika Dominika ya nne ya Majilio inatuleta karibu zaidi katika adhimisho tunalotarajia, yaani kuzaliwa kwake Mwokozi wetu Yesu Kristo na kutufanya kuwa tayari kuliadhimisha fumbo hilo. Wimbo wa Mwanzo wa Liturujia ya siku hii inaupambanua vema utayari huo. Nabii Isaya anaualika uwepo wa Mungu katika mazingira hayo ambayo tayari yameandaliwa: “Dondokeni, enyi mbingu, toka juu”. Hii inamaanisha kwamba matayarisho yetu tangu kuanza kwa kipindi cha Noeli yanatarajiwa kuwa yametuivisha vema kumpokea huyo Mwokozi: “Nchi ifunuke, na kumtoa Mwokozi”.

Somo la kwanza la Dominika hii linaweka wazi kwetu kuwa ujio huo wa Mkombozi kwetu ni mpango wa Mungu. Mwenyezi Mungu kwa jicho lake la huruma anatuangalia sisi wanadamu katika hali yetu ya udhaifu katika dhambi zetu na kung’amua kuwa tunashindwa kujikwamua kutoka katika hali hiyo. Maadui wengi wanatuzingira na kutishia uwepo wetu katika ramani ya dunia. Mfalme Ahazi anawakilisha jamii hiyo ambayo tunaweza pia kuileta katika mazingira yetu ya leo. Mara nyingi ama kwa kujidanganya kwetu sisi wanadamu, kwa kutegemea au kujishebedua na uwezo wetu wa kibinadamu tunashawishika kama Ahazi kuuona huo msaada wa Mungu hauna nafasi katika juhudi zetu. Matendo yetu daima yanasema “sitaitaka, wala sitamjaribu Bwana”.

Huu ni ujinga kiasi gani? Haya ni majigambo au majivuno ya wapi? Hata kama unao uwezo katika jambo fulani kwa nini ukatae msaada ambao unaletwa mbele yako ili kukupatia auheni na kufanikiwa katika juhudi zako? Hakika tunakosa jibu sahihi. Tunapoyatafakari mazingira hayo ya Ahazi tunaweza kuyaona pia katika jamii yetu ya leo. Misaada mbalimbali ya kimbingu inatujia kwa ajili ya kujinasua katika kongwa la utumwa wa ulimwengu huu lakini tunajikuta tunaitupilia mbali kabisa. Changamoto nyingi za kimaadili na kiutu zinatafutiwa suluhisho katika mwono na maelekeo ya kibinadamu tu. Wakati mwingine mambo yanapozidi kwenda kombo na sauti ya Mungu kupitia watumishi wake inapotujia kama suluhisho huwa tunaona kana kwamba wanatuwekea kiwingu, tunawaona kana kwamba wanajiingiza katika yale yasiyowahusu. Tunajibu kama Ahazi: “sitaika, wala sitamjaribu Bwana”.

Lakini pengine huwa tunakosa kuelewa vema huo ukombozi ambao Bwana ananuia kuuleta kwetu. Ahazi alifikiri kwamba Mwenyezi Mungu atakuja na kupigana kama afanyavyo yeye kwa mikono yake. Hapana, huko si mahali pake na hiyo si nia ya msaada au ukombozi anaotuletea. Vita na machafuko, chuki na kutokuelewana kati ya wanadamu kunasababishwa na kupotezwa kwa tunu ya utu ndani mwetu; tunashindwa kuiona sura yetu ndani ya wenzetu ambao wameumbwa kama sisi kwa sura na mfano wa Mungu. Ndiyo maana tunakuwa tayari kuwafanyia matendo yasiyo ya kiutu kama kuwanyonya, kuwatesa na hata kuwaua. Matokeo ya haya yote ni mtawanyiko katika jamii ya wanadamu na kuiharibu ile sura nzima ya ubinadamu wetu ambao umeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Lakini huu ni mpango wa Mungu kwa wanadamu. Yeye mwenyewe katika hekima yake ya kimungu ameng’amua umuhimu huo wa kushiriki katika kumokomboa mwanadamu. Upinzani wetu haumzuii kuendelea kuonesha upendo wake. Yeye anatuahidia huo ukombozi, ahadi ambayo tunapaswa kuipokea katika jicho la kimungu na si katika jicho la kibinadamu.

Yusufu, Baba Mlishi wa Yesu ni kinyume na Mfalme Ahazi. Pamoja na kwamba hapo mwanzoni anatawaliwa na mawazo ya kijamii na kukusudia kumuacha kwa heshima na kwa siri mchumba wake mwishoni anafikia kukubaliana na mpango wa Mungu: “Naye Yusufu alipoamka katika usingizi, alifanya kama malaika wa Bwana alivyomwagiza; akamchukua mkewe”. Ni wazi kwamba, mwanzoni Neno la Mungu linapotujia kwa njia mbalimbali tunaanza kwa kuhoji na pengine kufikiri katika namna njema ya kulipokea. Fundisho tulipatalo kutoka kwa Yusufu ni ule utayari wa kuiacha neema ya Mungu ifanye kazi ndani mwetu ili kulipokea vema Neno la Mungu na kulitekeleza kadiri ya mpango wake. Neema ya Mungu inapokosekana ndani mwetu tunashindwa kupiga hatua na kuzipokea changamoto mbalimbali za kimaisha katika jicho la kimungu na hivyo kujikuta tunaishia kusema “sitaitaka, wala sitamjaribu Bwana”.

Masiha anayezaliwa ni Imanueli, yaani Mungu pamoja nasi. Bikira anachukua mimba na kumzaa Imanueli ambaye ni Mungu kweli na mtu kweli. Ni mtu kama sisi isipokuwa dhambi. Anakuwa na hisia kama sisi, anatenda kama sisi na anakuwa na ukamilifu wote wa kibinadamu. Anakuwa kwetu ni mkombozi kwani ubinadamu wetu unapatiwa tena hadhi yake ya asili. Tunaumbwa tena upya katika namna ile njema Mungu aliyonuia tangu awali. Hivyo kutoka kwake huyu ndipo mwanadamu ataurejesha tena uhusiano mwema na Mungu na pia uhusiano wa kindugu na wenzake. Hapo ndipo vita na machafuko yatakoma na amani itaenea. Hakutakuwa tena na vita kama jibu kwa yule aliye kukosea bali jibu halisi litakuwa ni upendo na kutafuta amani itokayo kwa Mungu pekee.

Huyu ambaye anazaliwa kama sisi anazaliwa katika jamii ya wanadamu. Somo la kwanza linadokeza hilo kwamba atazaliwa na Bikira. Bikira huyo anathibitishwa na somo la Injili kuwa ni Mariamu aliposwa na Yusufu wa ukoo wa Daudi. Ndiyo maana pia Paulo anamtaja katika somo la pili kuwa ni Yeye “aliyezaliwa katika ukoo wa Daudi”. Haya yote yanawekwa mbele yetu ili kuufahamu ubini wake na pia kuuthibitisha ubinadamu wake kwamba anayo sehemu inayofahamika katika jamii ya kibinadamu. Yusufu anagundua kwa njia ya ujumbe wa malaika wa Mungu juu ya mpango huu wa Mungu na anaupatia nafasi na utii wake huu unamshirikishisha kwa namna ya pekee katika ukombozi wa mwanadamu. Masiha anayezaliwa anatambuliwa katika ukoo wake kwani kwa mila na desturi za kiyahudi anapokubali kumchukua Maria kama mkewe anampatia pia hadhi ya uzao wake wote kujumuishwa katika jamii yake hiyo ya kiyahudi.

Somo letu la Injili linaweka bayana pia kuingia kwake katika ukoo huu si kwa njia au nguvu za kibinadamu bali ni “kwa uweza wa Roho Mtakatifu”. Kristo ni nafsi ya pili ya Utatu Mtakatifu, ni Neno la Mungu anayetwaa mwili wetu wa kibinadamu. Katika muktadha wa kitelojia tunaona matendo ya Mungu katika historia ya mwanadamu. Mungu anaingia katika historia yetu. Ubinadamu wetu unapokea cheo kikubwa namna hii. Pengine tunaweza kujiuliza Je! ni Mungu anayeingia katika historia yetu au ni mwanadamu anayerudishwa katika uhusiano na Mungu? Hapa ndipo tunaweza kutupia jicho historia nzima ya wokovu na kuona kwamba mwanadamu alifukuzwa katika himaya ya Mungu kwa sababu ya dhambi zake. Mungu kwa upendo wake mkubwa alianza kumtayarisha taratibu katika pedagogia yake ya kimbingu kupitia mababu, waamuzi na manabii hadi kufikia nyakati za Masiha ambaye ameutwaa ubinadamu wetu, amekuwa kama sisi ili nasi tushirikishwe tena umungu wake.

Hivyo Dominika hii ya leo kwa hakika inatuzidishia shahuku ya kuisubiria Sherehe hiyo kubwa. Shahuku hii inasababishwa na ukweli wa hicho ambacho tunakipokea, yaani ukombozi ambao sisi binadamu tunaupokea. Prefasio ya Dominika hii inatualika ikisema “Yeye aliyetujalia kungojea kwa furaha fumbo la kuzaliwa kwake, atukute tukikesha katika sala na tukimshangilia kwa nyimbo za kumsifu”. Tuweke kando majigambo yetu na kiburi chetu cha kibinadamu kwani kwa hivyo tunamzuia Masiha kuzaliwa na kupenya katika historia ya maisha yetu.

Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.