Baba Mtakatifu Francisko katika Ujumbe wa Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2017 anasema, anapenda kuihakikishia Jumuiya ya Kimataifa kwamba, Kanisa Katoliki litaendelea kuunga mkono mchakato wa juhudi za ujenzi wa amani duniani. Tarehe Mosi, Januari 2017, Baraza Jipya la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu linazinduliwa rasmi, ili kulisaidia Kanisa kukuza na kudumisha haki, amani na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.
Kanisa linataka kuwahudumia wakimbizi, wahitaji, wagonjwa, waliotengwa na jamii; wahanga wa vita na majanga asilia; wafungwa na wasiokuwa na fursa za ajira pamoja na waathirika wa utumwa mamboleo na mateso. Haya ni mambo yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu! Vitendo vyote vyenye kudumisha utu na heshima ya binadamu vinapania kujenga ulimwengu usiokuwa na vita, hatua muhimu katika haki na amani.
Baba Mtakatifu Francisko ili kutekeleza azma hii amewateuwa Mheshimiwa Padre Michael Czerny, SJ., aliyekuwa mshauri wa Baraza la Kipapa la haki na amani pamoja na Mheshimiwa Padre Fabio Baggio, Rais wa Taasisi ya Wahamiaji Kimataifa ya Wascalabrini kuwa ni Makatibu wakuu wasaidizi wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu. Uteuzi huu unaanza mara moja, tarehe 1 Januari 2017. Makatibu hawa watajihusisha kwa namna ya pekee na huduma kwa wakimbizi na wahamiaji; kundi ambalo lina upendeleo wa pekee katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko kwa wakati huu!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©. |