2016-12-14 07:38:00

Askofu Javier Rodriguez alikuwa ni kiongozi mwaminifu na shuhuda!


Baba Mtakatifu Francisko amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya msiba wa Askofu Javier Echevarrìa Rodriguez, mwenye umri wa miaka 84 aliyekuwa mkuu wa Shirika la “Opus Dei”, yaani “Kazi ya Mungu” kuanzia mwaka 1994- 2016 aliyefariki dunia tarehe 12 Desemba 2016. Ni kiongozi aliyeonesha fadhila ya ubaba na ushuhuda wenye mashiko na mvuto kwa maisha na utume wa Kipadre na Kiaskofu. Itakumbukwa kwamba, alipewa Daraja ya Upadre hapo tarehe 7 Agosti 1955 na kunako tarehe 21 Novemba 1994 akateuliwa kuwa Askofu na kuwekwa wakfu hapo tarehe 6 Januari 1995.

Baba Mtakatifu ametuma ujumbe huu kwa Monsinyo Fernando Ocàris Brana, mkuu msaidizi wa Shirika la “Opus Dei”. Marehemu Askofu Javier Echevarrìa Rodriguez, amekuwa ni mfano bora wa kuigwa daima akijitahidi kufuata mifano ya watangulizi wake Mtakatifu Josemarìa Escrivà na Mwenyeheri Alvaro del Portillo walioiongoza familia ya “Opus Dei” kwa hekima na busara. Ni kiongozi aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma ya upendo kwa Kanisa na watu wake. Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia sala na sadaka yake, wale wote walioguswa na msiba huu mzito katika maisha na utume wao na anaiombea roho ya Marehemu Askofu Rodriguez iweze kupata furaha ya uzima wa milele.

Amefariki dunia wakati Kanisa linaadhimisha Kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Guadalupe na Ibada ya mazishi itaadhimishwa Alhamisi, tarehe 15 Desemba 2016 kwenye Kanisa la Mtakatifu Eugenio Jimboni Roma. Ni kiongozi anayekumbukwa na wengi kuwa ni mtu aliyekuwa na imani thabiti kwa Mungu, akaonesha kipaji cha uaminifu kilichojikita katika ugunduzi, alikuwa ni msaidizi mwenza wa wakuu wa Shirika kwa nyakati mbali mbali. Aliguswa na changamoto mamboleo, akajisadaka kwa ajili ya kujifunza teknolojia mpya ili kuwasaidia watu wa Mungu kupambana na changamoto za maisha.

Ni kiongozi aliyejipambanua katika mchakato wa Uinjilishaji wa familia, utume wa vijana sanjari na utamadunisho, ili kweli Injili ya Kristo iweze kuota mizizi katika maisha ya watu mbali mbali kwa kadiri ya mazingira yao pamoja na kusoma alama za nyakati. Alipania kuona majiundo makini na endelevu kwa majandokasisi waliopania kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani zao. Alikuwa ni shuhuda na chombo cha huduma kwa wahamiaji na wakimbizi; kwa wazee na wagonjwa, aliowaonesha upendo unaobubujika kutoka katika Fumbo la Msalaba, kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu.

Marehemu Askofu Javier Echevarrìa Rodriguez alikuwa ni kiongozi aliyekita maisha yake katika Sala na Tafakari ya Neno la Mungu lililokuwa linamwilishwa katika huduma makini katika familia, ili kweli familia ziweze kuwa ni mashuhuda wa tunu msingi za maisha ya ndoa na vyombo vya Injili ya familia. Ni kiongozi aliyependa kujenga na kudumisha umoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro, akawasindikiza kwa sala na sadaka yake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.