2016-12-13 14:13:00

Bwana Paolo Gentiloni ndiye Waziri mkuu mpya wa Italia!


Rais Sergio Mattarella wa Italia baada ya kuangalia changamoto zilizoko mbele ya Italia katika medani mbali mbali za kitaifa na kimataifa, amemteua Bwana Paolo Gentiloni kuunda Serikali mpya baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu Matteo Renzi kubwaga manyanga baada ya Serikali yake kushindwa kwenye kura ya maoni kuhusu mabadiliko katika Katiba ya Nchi! Waziri mkuu mpya Paolo Gentiloni, Jumatatu tarehe 12 Desemba 2016 alikuwa kiapo na tayari amekwisha unda serikali mpya.

Taarifa inaonesha kwamba, sehemu kubwa ya Baraza la Mawaziri lililokuwa kwenye Serikali ya Matteo Renzi wamerudishwa tena madarakani, lakini kukiwa na mabadiliko makubwa kwenye sehemu tete! Kuna mawaziri wapya watano. Aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani ya nchi Bwana Angelino Alfano sasa anakuwa ni Waziri wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa. Bwana Marco Minnitti ameteuliwa kuwa Waziri wa mambo ya ndani ya nchi, kabla ya hapo alikuwa ni waziri mdogo wa mambo ya ndani ya nchi na masuala nyeti ya nchi. Bwana Pier Carlo Padoan anaendelea kuwa ni Waziri wa uchumi.

Vyama vya upinzani vimeishutumu Serikali ya Matteo Renzi kwa kuwangoza Waitalia kwa ubabe na kwamba, hawana imani na Serikali mpya ya Bwana Paolo Gentiloni inayoonekana kuwa ni mwendelezo wa Serikali ya Matteo Renzi. Sehemu kubwa ya vyama vya upinzani vinataka wananchi wa Italia wapewe nafasi ya kupiga kura ili kuwachagua viongozi wanaowataka, kwani kwa mara ya mwisho, wananchi waliweza kupiga kura na kumchagua Bwana Silvio Belusconi kuwa Waziri mkuu. Lakini tangu wakati huo, kumekuwepo na kuanguka kwa Serikali na uundwaji wa Serikali mpya bila ya wananchi kushirikishwa kupiga kura ingawa wachunguzi wa masuala ya kisiasa wanasema, kuna sheria mbili za upigaji kura zinazosigana, hali inayokwamisha mchakato wa mageuzi yanayotarajiwa na wengi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.