2016-12-10 15:11:00

Shughulikieni matatizo ya wakulima vijijini ili kuinua utu na maisha yao!


Shirikisho la Kimataifa la Wakatoliki Vijijini, ACRI, hivi karibuni limehitimisha mkutano wake wa mwaka uliokuwa unajadili pamoja na mambo mengine matatizo na changamoto za maisha ya vijijini, hasa matatizo wanayokabiliana nayo wakulima vijijini. Hii ni dhamana inayotekelezwa kwa jasho kubwa kwa ajili ya huduma kwa wengine na kwamba, uzalishaji wa mazao ya nchi mwaka hadi mwaka unaendelea kukumbana na changamoto nyingi mintarafu athari za mabadiliko ya tabianchi ambayo kimsingi yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na shughuli za binadamu!

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 10 Desemba 2016 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Shirikisho la Kimataifa la Wakatoliki Vijijini ambalo linaendelea kutoa kipaumbele cha pekee kwa matumizi na utunzaji bora wa mazingira kadiri ya Mafundisho Jamii ya Kanisa, ili kuendeleza kazi ya Uumbaji na kulinda mazingira nyumba ya wote. Kilimo ni uti wa mgongo kwa uchumi wa Jumuiya ya Kimataifa, lakini kwa bahati mbaya hakijapewa kipaumbele cha kutosha ili kuweza kukabiliana na ukosefu wa usalama wa chakula pamoja na kusaidia maboresho ya maisha ya wakulima vijijini.

Kilimo kwa baadhi ya maeneo duniani kinaweza kuwa ni suluhu ya kupambana na umaskini pamoja na baa la njaa duniani. Ili kufikia lengo hili kuna haja ya kuwa na sera makini za kilimo zinazotekelezwa na taasisi mbali mbali pamoja na usawa wa umiliki wa ardhi, vinginevyo, wakulima wadogo wadogo wanaweza kupokwa ardhi yao kutokana na ukosefu wa sera makini za kilimo: kitaifa na kimataifa! Soko la mazao ya kilimo ndilo mwongozo wa maamuzi na matendo yanayoathiri kimsingi maisha ya wakulima vijijini, kana kwamba, maisha ya wakulima vijijini hayana thamani sana.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, mshikamano wa kimataifa hauna budi kufumbatwa katika haki ya ugawaji na umiliki wa ardhi; mshahara wa wakulima pamoja na kuwa na fursa ya kushiriki moja kwa moja katika soko la mazao ya kilimo. Inasikitisha kuona kwamba, ushiriki wa wakulima wadogo wadogo katika maamuzi ya mazao ya kilimo bado ni mdogo sana kutokana ukosefu wa vyombo vya uwakilishi wa wakulima; ukosefu wa sheria na kanuni zinaozingatia tunu msingi za uaminifu, usahihi na ukweli wa mambo.

Wakristo katika mazingira ya maisha vijijini wanaweza kuchangia kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu; kwa kukazia tunu msingi za maisha ya kifamilia na kijamii zinazofumbatwa katika mshikamano kama chachu ya mapambano dhidi ya umaskini na ukosefu wa maendeleo. Shirikisho la Kimataifa la Wakatoliki Vijijini kwa vile lina uhusiano na Mashirika ya Kimataifa linaweza kusaidia mchakato wa kupambana na changamoto zote hizi kwa kufanya maamuzi magumu na yenye ujasiri, kwa kuendelea kuboresha ujuzi na maarifa; kwa kushirikiana na Taasisi za Kitaifa na Kimataifa ili kutafuta ufumbuzi wa changamoto za kiteknolojia ili kutoa suluhu ya changamoto hizi kwa mwono wa kibinadamu na kiutu sanjari na kusaidia Ulimwengu wa wakulima kushiriki katika maamuzi ya sera na sheria katika medani mbali mbali za maisha ya kijamii na kiuchumi.

Baba Mtakatifu anawataka wajumbe hawa kuhakikisha kwamba sera na mikakati yao ya majiundo ijikite si tu katika masuala ya biashara ya mazao ya kilimo bali ziangalie pia watu na mazingira yao, ili kuweza kuwa na hifadhi bora zaidi ya mazao ya kilimo kutoka kwa mkulima shambani hadi sokoni pamoja na kuzingatia utajiri unaojikita katika utofauti wa kibailojia, ili kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote hata kwa vizazi vijavyo! Shirikisho hili lisaidie mchakato wa kujenga madaraja kwa kutambua asili yake ili hatimaye, kushiriki kikamilifu katika mchakato wa mageuzi ya mbinu mkakati na miradi inayobuniwa.

Hapa kunahitajika weledi, utashi na sadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengine. Shirikisho la Kimataifa la Wakatoliki Vijijini linahamasishwa kuwa na maisha ya kiasi, kujenga utamaduni wa kazi ya kilimo unaozingatia misingi na malengo yake, daima mwanadamu akipewa kipaumbele cha kwanza; kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya jirani zake. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko ametoa baraka zake za kitume kwa wakulima vijijini pamoja na familia zao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.