2016-12-10 13:54:00

Habari kutoka Vatican kwa ufupi!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 10 Desemba 2016 amepokea hati za utambulisho kutoka kwa Mheshimiwa Agnès Adjaho, Balozi wa Benin mjini Vatican. Mheshimiwa Balozi alizaliwa kunako tarehe 21 Januari 1949 ameolewa na watoto watatu!

Baba Mtakatifu amemteua Mheshimiwa Padre Martin Wangue Bani kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Doba, chini Chiad. Askofu mteule alizaliwa tarehe 12 Februari 1963 na kupewa Daraja takatifu ya Upadre tarehe 8 Julai 1991.

Wakati huo huo, Papa Francisko amemteua Mheshimiwa Padre Richard Appora kuwa Askofu mwandamizi wa Jimbo Katoliki Bambari, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati. Kabla ya uteuzi wake alikuwa ni Mkuu wa Jumuiya ya Wadominikani mjini Bangui na Rais wa Shirikisho la Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya kati. Alizaliwa kunako tarehe 3 Aprili 1973 na kupewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe Mosi Novemba 2004.

Baba Mtakatifu Francisko amekubali ombi la kung’atuka kutoka madarakani lilikowasilishwa kwake na Kardinali Gabriel Zuberi Wako wa Jimbo kuu la Khartoum Sudan Kongwe. Na Papa amemteuwa Askofu mwandamizi Michael Didi Adgum Mangoria wa Jimbo kuu la Khartoum, Sudan Kongwe, kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Khartoum Sudan Kongwe.

Na habari zaidi kutoka Vatican zinasema, Vatican imeanzisha uhusiano wa Kiplomasia na Jamhuri ya Kiislam ya Watu wa Mauritania. Kutokana na mahusiano haya, Vatican sasa itatuma Balozi nchini Mauritania na Mauritania kwa upande wake itakua na Balozi wake mjini Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.