9 Desemba Rais John Magufuli aliongoza watanzania katika kilele cha maadhimisho ya Miaka 55 ya Uhuru wa Tanzania Bara, yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, ikiwa ni mara yake ya kwanza kushiriki sherehe hizo.
Kaulimbiu katika maadhimisho hayo ni “Tuunge mkono jitihada za kupinga rushwa na ufisadi na tuimarishe uchumi wa viwanda kwa maendeleo yetu.”
Maadhimisho hayo yalifanyika kwa mara ya kwanza tangu Dk Magufuli kuingia madarakani kutokana na mwaka jana kuzisitisha na kutaka kuadhimishwa kwa kufanya usafi katika maeneo mbalimbali nchini; aliagiza fedha zilizokuwa zimetengwa kwa maadhimisho hayo zaidi ya Sh bilioni nne kutumika kufanya upanuzi wa barabara ya Mwenge hadi Morocco jijini Dar es Salaam yenye urefu wa kilometa 4.3 kwa kuongeza njia mbili za barabara za lami.
Katika maadhimisho hayo yalihudhuriwa na marais wa nchi jirani na viongozi wastaafu.
Wakati sherehe zilipambwa na gwaride la heshima lililoandaliwa na Vikosi vya Ulinzi
na Usalama ikiwemo Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Kujenga
Taifa (JKT), Polisi na Magereza.Vilevile kulikuwa na maonesho ya kwata la kimya kimya
pamoja na makomandoo wa JWTZ, burudani za vikundi vya muziki wa kizazi kipya na kizazi
cha zamani pamoja na ngoma za asili kutoka mikoa ya Mbeya, Pwani, Lindi na Zanzibar.
Akikaririwa katika maadhimisho hayo, Spika wa Bunge mstaafu, Pius Msekwa aliwataka
Watanzania kusherehekea sikukuu hiyo kwa kumuenzi Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu
Julius Nyerere kwa kuzingatia na kuendeleza misingi aliyoacha ambayo marais wote waliomfuata
waliisimamia.
Msekwa ambaye pia aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), alisema
katika maadhimisho hayo ni vema kumkumbuka Nyerere na wenzake walioshiriki kupigania
kwa kutambua kuwa haukuja kama mvua na bila wao katika nyakati hizi hali ingekuwaje?
Aidha alisema ni vema kuangalia kwa jinsi alivyopambana na changamoto mbalimbali wakati
wa kugombania uhuru na jinsi alivyokuwa akitumia busara na kuona mbali kuwashauri
wenzake na kutoa mfano katika moja ya kikao, wenzake walishauri kususia, lakini yeye
aliona mbali kwa kuwataka kushiriki kwani kususia kwao kungetoa mwanya kwa wakoloni
kuzidi kuwatawala.
Na Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican Inaungana na watanzania wote walioko
ndani na nje ya nchi kutakiana Baraka na Amani ya nchi na kumuenzi Mwasisi wa Taifa
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
All the contents on this site are copyrighted ©. |