2016-12-09 08:00:00

Papa akabidhi mahangaiko ya binadamu kwa Bikira Maria!


Katika maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, tarehe 8 Desemba 2016 Baba Mtakatifu Francisko majira ya jioni alikwenda kutoa heshima zake kwenye mnara wa Sanamu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili uliopo kwenye uwanja wa Spagna, mjini Roma, tukio lililoshuhudiwa na umati mkubwa wa watu wa Mungu kutoka ndani na nje ya Italia. Baba Mtakatifu katika sala yake, amemwambia Bikira Maria kwamba, mbele yake alikuwa amewabeba watu wote waliowekwa chini ya dhamana yake na Kristo Yesu, ili aweze kuwaombea na kuwalinda dhidi ya hatari zote za roho na za mwili!

Baba Mtakatifu anasema, moyoni mwake anapenda kumtolea watoto hasa wale walio pweke, waliotelekezwa na kutengwa na matokeo yake, wanadanganywa na kunyonywa. Anapenda kumpelekea familia; watu wanaojisadaka kila siku ili kuhakikisha kwamba wanaendeleza maisha na jamii katika ujumla wake; kwa majitoleo yao ya kila siku katika hali ya uficho; lakini kwa namna ya pekee, anamtolea familia zinazokabiliwa na hali ngumu ya maisha kutoka ndani na nje ya familia zenyewe.

Baba Mtakatifu anampelekea Bikira Maria wafanyakazi wote na kuwaaminisha wake, kwani kutokana na mahitaji yao msingi, wanajikuta wakifanya kazi kinyume cha utu na heshima ya binadamu; anapenda kumtolea wale wote waliopoteza fursa za ajira au kutokana na sababu mbali mbali wanashindwa kupata nafasi ya kazi. Wote hawa anasema Baba Mtakatifu wanahitaji kuona sura ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya asili, ili kuwa na uwezo tena wa kuwaangalia watu na vitu kwa heshima na kwa utambuzi, bila ya kuwa na masilahi binafsi au unafiki.

Baba Mtakatifu anaendelea kusali akisema, binadamu anahitaji Moyo Safi wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, ili kupenda na kujisadaka bila ya kuwa na masilahi binafsi, bali kwa kutafuta chema kwa ajili ya wengine, katika hali ya kawaida inayofumbatwa katika ukweli kwa kuondokana na unafiki au hali ya udanganyifu. Binadamu anahitaji mikono ya Bikira Maria Immakulata, ili kupenda kwa pendo la kweli, ili kugusa Mwili wa Kristo unaojionesha kwa namna ya pekee, miongoni mwa maskini, wagonjwa na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; binadamu anahitaji mikono ya Bikira Maria Immakulata, ili waweze kuwainua wale walioanguka na kuwategemeza wanaoyumba.

Binadamu anahitaji miguu ya Bikira Maria Immakulata, ili kuwaendea wale ambao hawawezi kunyanyua miguu yao na kuanza kutembea; ili kutembea na wale wote waliopotea na kuwatafuta wanaoishi katika upweke. Baba Mtakatifu anamshukuru Bikira Maria kwa kujionesha kati ya watu wake kuwa ni safi pasi na doa la dhambi. Anawakumbusha waamini kwamba, pamoja na mambo mengine yote, iko neema ya Mungu, upendo wa Yesu aliyetoa maisha yake kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu na nguvu ya Roho Mtakatifu inayopyaisha yote. Anamwomba Bikira Maria awasaidie watoto wake wasianguke katika kishawishi cha kukata tamaa, kwani wanatumaini msaada wake na kwamba, wanajibidisha kutoka katika undani wao ili kupyaisha maisha yao, maisha ya mji wa Roma na ulimwengu katika ujumla wake. Bikira Maria, Mama wa Mungu, Utuombee!

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya sala kwa heshima ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, alikwenda moja kwa moja hadi kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu lililoko mjini Roma, ili kutoa pia heshima yake kwa Bikira Maria, Afya ya Warumi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.