2016-12-09 15:50:00

Ni wakati wa kicheko na furaha ya kukutana na Mkombozi


Dominika ya tatu katika Kipindi cha Majilio hutambulika kama Dominika ya Furaha. Matini ya wimbo wa mwanzo wa Liturujia yanatualika katika furaha hiyo na kutuambia sababu za mwaliko huo wa furaha: “Furahini katika Bwana siku zote; tena nasema furahini. Bwana yu karibu”. Tunapewa mwaliko wa kuwa na furaha ya daima kwa kuwa kile tulichokuwa tunakitarajia au kukingoja kinakaribia: Bwana wetu Yesu Kristo, Masiha na Mkombozi wetu yu karibu. Ni mwaliko ambao unatufunulia kile ambacho kinapaswa kuonekana daima katika jamii ya wanakanisa na pia kuusimika utume wa Kanisa ambao ni kuieneza furaha itokayo kwa Kristo.

Somo la kwanza la Dominika ya leo inayaelezea hayo yatakayotokea na kusababisha furaha. Nabii Isaya anawapatia wana wa Israeli ujumbe huo wa furaha: “Waambieni walio na moyo wa hofu, Jipeni moyo, msiogope; tazama, Mungu wenu atakuja na kisasi, na malipo ya Mungu; atakuja na kuwaokoa ninyi”. Hali ya utumwa ambayo ilikuwa inawatawala kwa wakati huo itaondolewa. Wana wa Israeli wakiwa utumwani Babeli watarejeshwa tena katika nchi yao ya ahadi. Kitakachoshuhudiwa ni furaha: “Na hao waliokombolewa na Bwana watarudi, watafika Sayuni wakiimba; na furaha ya milele itakuwa juu ya vichwa vyao; nao watapata kicheko na furaha, huzuni na kuugua zitakimbia”.

Kristo, Masiha wetu anayekuja ndiyo hiyo furaha. Hili tunaliona vema katika somo la Injili. Tukijaribu kutafakari ni kwa nini Yohane Mbatizaji anatafuta uhakika kama Kristo ndiye au la tunaweza kupata mwanga zaidi ya kuielewa hiyo furaha inayotujia. Yohane Mbatizaji yupo gerezani na anasikia juu ya matendo ya Kristo. Dukuduku lake linachagizwa na makuu haya ya Mungu ambayo anasimuliwa. Katika sura ya kumi ya Injili ya Mathayo ambayo ndiyo inatangulia sehemu hii tuliyosikia leo tunasikia juu ya utume wa umisionari wa Yesu kwa mitume wake. Anapowatuma anawaagiza kwenda kuwaambia watu juu ya ufalme wa Mungu. Ni wazi hili linaongeza kujulikana kwake na anazidi kupata umaarufu katikati ya watu.

Kristo anaonesha ni namna gani ufalme huo wa Mungu unadhihirika, ni namna gani uwezo wa Mungu unashuhudiwa na ni namna gani makuu ya Mungu yanadhihirika katikati ya watu. Muktadha ule unaosimuliwa na Nabii Isaya katika somo la kwanza unadhihirika katika nafsi ya Kristo. Watu walio na hofu, mateso, wasiwasi, utengano, uhasama na hali nyingine nyingi zisizofaa wanaionja furaha hiyo inayoimbwa katika nafsi ya Kristo: “vipofu wanapata kuona, viwete wanakwenda, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, na maskini wanahubiriwa habari njema”.

Mrejesho huo kwa wanafunzi wa Yohane Mbatizaji ni dokezo kwetu kwamba furaha hiyo si ya kutamka tu kwa mdomo, si jambo la kutamka tu au kuandika kwa maandishi mazuri bali ni hali ambayo inapaswa kuonekana katika hali au maisha halisi. Haitoshi kwa tabibu kuwa bingwa kwa usomi wa darasani tu au mwalimu kuwa mweledi kwa alama nzuri toka chuoni ila ni katika kumpatia afya na ahueni mgonjwa au kumwelimisha yeye anayetarajia kutoka kwako wewe uliye na ujuzi fulani. Hilo ndilo dai na jukumu tunalobebeshwa kama Wakristo. Tuwapatie watu majibu ya furaha iliyopo ndani mwetu kwa matendo yetu ambayo yanamfikisha Kristo kwa wengine. Furaha yetu iguse nafsi za watu na wao wapate majibu ya furaha tuliyokuwa nayo kutokana na ukarimu wetu wa kindugu kwao.

Sisi Wakristo ambao tumembeba Yeye aliye furaha tunaipeleka vipi furaha hii kwa wengine? Wapo wengi wenye mioyo ya hofu mithili ya Waisraeli waliokuwa utumwani. Utume huu tutaufanikisha kwa sisi wenyewe kuanza kuionja hiyo furaha ya Kristo na maisha yetu kutoa miale yake na kuwaangazia wengine mithili ya jua ya alfajiri ambalo humletea mwanadamu matumaini kwa kuipokea siku mpya. Leo hii tunaishi katikati ya jamii ambayo imemweka kando Mwenyezi Mungu na hivyo ni aghalabu kwa jamii kama hii kuweza kumwona mwanadamu katika ukweli ambao asili yake ni Mungu mwenyewe. Changamoto inayokuja kwetu ni kuwa na ujasiri wa kuogelea tukikinzana na mkondo.

Tunaitwa kuitafuta furaha, si kama wanavyotaka walimwengu wasiomjua Mungu bali kama anavyotaka Mungu. Matayarisho yetu yasionekane kujikita katika mambo ya nje tu na kuifurahia kwa mapambo na starehe za nje tu bali ionekane katika utambulisho wetu wa maisha ambao unagusa nafsi za wengine walio na moyo wa hofu.

Mara ngapi tunashuhudia urasimishaji wa matukio au hata sheria za jamii ambazo hazimjali mwanadamu? Jamii katika ufinyu wa mawazo yako na kujidanganya katika kuyajua yote inajiamulia na kujipangia mambo yake ambayo badala ya kuleta furaha ya kweli kama wanavyojidanganya huleta huzuni, mgawanyiko, chuki au msongo wa mawazo. Watu hawa ni mimi na wewe na wale wanaotuzunguka. Kristo anatuambia katika Injili kwamba “naye heri awaye yote asiyechukizwa nami”. Hivyo tuitafute furaha yetu katika Kristo na kamwe tusione ukakasi katika kuisikia sauti yake kwa kuwa yeye ni “njia, ukweli na uzima”. Tuwe na uvumilivu kama anavyotuasa Mtume Yakobo akitualika kwamba “vumilieni, mthibitishe mioyo yenu ... watwaeni manabii walionena kwa jina la Bwana, wawe mfano wa kustahimili mabaya, na wa uvumilivu”.

Wimbo wa mwanzo kama tulivyodokezwa hapo juu unatuambia kuwa yu karibu na hivyo tunapaswa kufurahi. Tunaweza kuutafakari huu ukaribu katika namna mbili: kwanza kwa kuangalia kile ambacho kinakaribia kutufikia. Lakini kwa upande mwingine tunaweza kuuona huo ukaribu katika kile ambacho tupo nacho jirani. Hapa tunaweza kuona furaha hii inatuunganisha katika maandalio ya aina mbili tunayoalikwa kuyafanya wakati huu wa Majilio, yaani kujiandaa na ujio wa pili wa Kristo na kujiandaa na maadhimisho ya sherehe ya Noeli ambayo yamkini ipo karibu.  Maana hii ya pili inaweza kupata mashiko zaidi kwani inatukumbusha kwamba furaha yetu inapaswa kuwa ni ya siku zote kwa kuwa tunayemtamani au kumngojea yupo pamoja nasi, yupo jirani yetu.

Sherehe tunayoitarajia kuiadhimisha siku chache zijazo inaturudisha nyuma na kutuunganisha na ile siku ambayo nuru kuu iliuzukia ulimwengu na kuujaza furaha. Lakini pengine furaha hiyo haionekani tena au imefifishwa sababu ya uhaba wetu wa kiimani. Sisi waamini tunapoitarajia siku hiyo na zaidi ujio wake wa pili tunaendelea kupokea jukumu lile la kuamsha tena ule utajiri ambao umefichwa ndani mwetu, yaani kukitambua cheo chetu ambacho tumekipokea kwa njia ya Kristo. Hivyo, matarajio yetu yote yawe ni kwa ujio wa pili wa Kristo au maadhimisho ya sherehe ya Noeli yanalenga kutuhakikishia kwamba Bwana yu karibu na ni jukumu letu kuudhihirisha ukweli huo na kuijaza furaha ya Bwana.

Tuijaze mioyo yetu furaha hiyo ya kweli. Kristo Mkombozi wetu ndiye anayeithibitisha furaha hiyo. Hivyo tumngojee kwa furaha na kumwandalia makao kwa kuruhusu wajumbe wake ambao anawatuma mbele yetu daima, yaani Mama Kanisa Mtakatifu kwa ajili ya kuitayarisha yake kwa Sakramenti na Neno lake. Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iendelee kuwa nanyi siku zote na tuendelee kuwa na furaha na matumaini kwa kuwa Bwana yu karibu.

Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.