2016-12-09 08:54:00

Mbinu mkakati wa maandalizi ya Ujio wa Papa Jimbo kuu la Milano!


Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kufanya hija ya kichungaji Jimbo kuu la Milano, tarehe 25 Machi 2017, wakati wa Sherehe ya Bikira Maria kupashwa habari kuwa atakuwa ni Mama wa Mungu. Hii itakuwa ni fursa makini kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro kuwaimarisha ndugu zake katika imani. Jimbo kuu la Milano, limeanza maandalizi kamambe kwa ajili ya ujio huu kwa kutoa ratiba elekezi pamoja na kuchapisha barua ya kichungaji kwa familia ya Mungu mkoani Lombardia ili kuweza kupokea neema na baraka zinazoletwa kwao na Baba Mtakatifu Francisko.

Kipindi hiki cha Majilio ni fursa nzuri kwa waamini kujikita katika maandalizi haya kwa kuimarisha imani katika Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, kwa kutambua kwamba, Bikira Maria ni kielelezo cha imani na matumaini kwa waamini. Ujio wa baba Mtakatifu Francisko uendelee kuwaimarisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema Jimbo kuu la Milano, ili waweze kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Furaha ya Injili, daima wakiendelea kufundwa katika shule ya Kristo, ili kweli mafundisho ya Yesu yaweze kuwa ni kiini moyo na mtima wa maisha ya Jumuiya ya waamini Jimbo kuu la Milano.

Hiki kiwe ni kipindi cha sala, tafakari na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, mahali pa kukutana na kuzungumza na Kristo Yesu sanjari na kuimarisha katekesi ili waamini waweze kujifunza kujitosa kimasomaso kwa ajili ya huduma kwa jirani zao. Familia ya Mungu Jimbo kuu la Milano, inajiandaa pia kumshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuitisha, kuzindua na kuadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Sasa ni wakati wa kuendelea kumwilisha matunda ya Mwaka wa huruma ya Mungu katika maisha ya kila siku kwa kujikita katika matendo ya huruma kiroho na kimwili; kukimbilia huruma na upendo wa Mungu katika Sakramenti za huruma ya Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume, “Misericordia et misera” “Huruma na amani” anawaalika waamini kuendelea kuwa ni vyombo vya huruma na haki ya Mungu katika maisha ya watu, kwa kuendelea kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha, kielelezo makini cha imani tendaji! Hii inatokana na ukweli kwamba, huruma ya Mungu inawaweza waamini kupata maisha mapya na kuendelea kuyaboresha kwa matumaini. Ni mwaliko wa kuendelea kutubu na kujikita katika wongofu wa kimissionari kwa njia ya ushuhuda huku wakisukumzwa na Neno la Mungu “Kwa maana mimi nina watu wengi katika mji huu”! Kumbe, hakuna sababu ya kukata wala kukatishwa tamaa. Matendo ya huruma: kiroho na kimwili yaendelee kumwilishwa katika maisha ya watu.

Kipindi cha Kwaresma kwa Mwaka 2017 kitakuwa na umuhimu wa pekee kabisa, kwani kitakuwa ni msaada kwa waamini kujiandaa kikamilifu kuadhimisha Fumbo la Pasaka kwa ari na moyo mkuu, kwa kuwa na huruma kama Baba yao wa mbinguni alivyo na huruma na kwamba, hakuna mtu awaye yote anayeweza kuwapoka furaha ya Uinjilishaji inayogeuzwa na kuwa ni hija ya wongofu wa kila siku; katika malezi na majiundo ya imani na utu wema kwenye familia, kwa kumwilisha imani na ushuhuda wa tunu msingi za Kiinjili katika medani mbali mbali za maisha. Kimsingi, umati mkubwa wa watu kama Jimbo kuu la Milano unahitaji kutangaziwa na kushuhudiwa Injili.

Ratiba elekezi ya Ujio wa Baba Mtakatifu Francisko Jimbo kuu la Milano inaonesha hamu na shahuku yake ya kukutana na umati mkubwa wa familia ya Mungu Jimboni Milano, ili watu wengi zaidi waweze kumwona na kumsikia pasi na upendeleo wa mtu awaye yote, bali neema na baraka zake ziweze kuwagusa na kuwaambata watu wote wa Jimbo kuu la Milano!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.