2016-12-08 14:53:00

Watawa iweni ni mifano bora ya kuigwa na vijana wa kizazi kipya!


Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili ni mfano bora wa kuigwa katika maisha na majitoleo ya watawa kwa ajili ya huduma kwa familia ya Mungu. Ni Mama aliyeonesha kwa namna ya pekee moyo wa kusikiliza na kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yake, tayari kuwa ni chombo cha wokovu wa binadamu na hivyo akakirimiwa neema ya kuwa kweli ni Mama wa Mungu na Kanisa. Bikira Maria, mwombezi na msimamizi wa watawa, awe kweli ni mfano bora wa kuigwa kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia uwepo wa Ufalme wa Mungu katika maisha ya watu; kwa mfano wenye mvuto na mashiko.

Haya yamesemwa na Askofu Titus Joseph Mdoe wa Jimbo Katoliki Mtwara, Tanzania wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuadhimisha Siku kuu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili sanjari na Jubilei ya miaka 25 ya Maisha ya Kitawa kwa watawa tisa wa Shirika la Masista Wabenediktini wa Bikira Maria Msaada wa Wakristo, Ndanda, Alhamisi, tarehe 8 Desemba 2016 huko Ndanda, Mtwara.

Anasema, maisha matakatifu, manyofu na adilifu ni cheche za miito mipya ndani ya Kanisa kwani ushuhuda wa maisha una mvuto mkubwa kwa vijana wa kizazi kipya. Kumbe, watawa wanapaswa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa watu! Amekumbusha kwamba, kuna kundi kubwa la vijana ambao ni nguvu kazi na jeuri ya Kanisa na taifa katika ujumla wake, hawa wanahitaji kuoneshwa mifano bora ya maisha, ili hatimaye, waweze kuajibika barabara katika ujenzi wa Kanisa na Tanzania katika ujumla wake.

Askofu Titus Mdoe anatawaka watanzania kukuza na kudumisha Ibada kwa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Msimamizi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kumtegemea, ili kwa maombezi yake awasaidie kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi, kila mtanzania akijitahidi kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara. Watawa waliomwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kuadhimisha Jubilei ya miaka 25 ya maisha ya kitawa ndani ya Shirika la Masista wa Wabenediktini wa Bikira Maria Msaada wa Wakristo, Ndanda wanatoka katika: Jimbo kuu la Songea, Mtwara, Lindi na Tunduru-Masasi.

Kwa msaada wa Padre Anthony Chilumba! Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.